Leo ndio leo uchaguzi AUC Addis Ababa

Muktasari:
- Mataifa 49 ya Afrika leo yatachagua mwenyekiti na naibu mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), watakaoongoza tume hiyo kwa miaka minne.
Addis. Leo ndio siku iliyokuwa ikisubiriwa ya kumpata mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) kwa ajili ya kumrithi Mousa Faki, raia wa Chad, mwenyekiti anayemaliza muda wake.
Mgombea anayepewa nafasi kubwa ya kushinda ni Raila Amolo Odinga (79), kiongozi wa upinzani nchini Kenya an ayeungwa mkono nan chi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hata hivyo, Odinga amekuwa katika tishio la kupata upinzani mkali kutoka kwa Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Madagascar, Richard Randriamandrato, ambaye Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) imewaomba wanachama wake kumuunga mkono.
Mgombea mwingine ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti Mahamoud Ali Youssouf.
Muundo wa uongozi AUC
Kwa mujibu wa tovuti ya AU, Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) inajumuisha Mwenyekiti, Naibu Mwenyekiti na Makamishna, pamoja na wafanyakazi wengine.
Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali huchagua Mwenyekiti na Naibu Mwenyekiti, huku Baraza la Mawaziri likichagua Makamishna, ambao huidhinishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi. Wanachama wa Tume wanahudumu kwa muda wa miaka minne, na wanaweza kuchaguliwa tena kwa kipindi kingine kimoja.
Novemba 2018, kama sehemu ya mageuzi ya kimuundo, Mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali uliamua kuanzia mwaka 2021, Tume itakuwa na wanachama wanane – Mwenyekiti, Naibu Mwenyekiti, na Makamishna sita.
Pia, Mkutano uliamua kuboresha uwazi na misingi ya sifa katika mchakato wa uteuzi wa viongozi. Mchakato huu mpya ulianza kutumika Januari 2021.
Kanuni kuu za uteuzi ni pamoja na uwakilishi wa haki wa kanda, usawa wa kijinsia, mzunguko wa nafasi kwa utaratibu maalumu, kuvutia na kuhifadhi vipaji bora barani Afrika, uongozi wenye uwajibikaji na ufanisi, pamoja na uteuzi wa uwazi unaozingatia sifa.
Uchaguzi
Uchaguzi wa uongozi wa juu wa AUC unaofanyika leo, ni kwa mujibu wa uamuzi wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika, ambao unahakikisha mzunguko wa kijiografia wa majukumu kwa mfumo wa "Mzunguko kwa Kizuizi cha Sehemu."
Mfumo huu unasimamia nafasi za mwenyekiti na naibu mwenyekiti kwa kuzingatia mzunguko wa kanda kwa mpangilio wa alfabeti za Kiingereza, huku nafasi za makamishna zikishindaniwa kwa uwazi.
Kwa mujibu wa sheria za Umoja wa Afrika, ni mataifa ambayo hayakabiliwi na adhabu yoyote ndio yatakayopata fursa ya kupiga kura.
Kwa sababu hiyo, ni mataifa 49 pekee ambayo yana uwezo wa kuamua ni nani atakayemrithi Moussa Fakii kwenye nafasi ya mwenyekiti wa Tume ya AU.
Akizungumza na BBC kuhusu mchakato huo utakavyokuwa, Balozi Erastus Mwencha aliyewahi kuhudumu kama Naibu Mwenyekiti wa AUC, amesema mshindi atahitajika kuwa na uungwaji mkono wa theluthi mbili ya jumla ya kura zilizopigwa.
“Ikiwa hakutakuwa na aliyefikisha kiwango hiki, basi kengele itapigwa na kura kupigwa kwa raundi ya pili, ambapo wagombea wawili wa kwanza wataminyana.
“Ikiwa katika raundi hii hakuna mshindi wa moja kwa moja, basi uchaguzi wa maibu mwenyekiti unaendelea na akipatikana mshindi atashikilia wadhifa huo kwa muda wa miezi sita, ambapo uchaguzi wa uenyekiti utaandaliwa upya,” amesema.
Katika uchaguzi wa 2017 upinzani mkali ulikuwa kati ya Balozi Amina Mohammed aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya chini ya uongozi wa Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa zamani wa Chad, Moussa Fakii Mahamat.
Kutokana na ushindani huo, kura zilipigwa raundi saba na hatimaye kuamuliwa kwa kura moja tu, kati ya mashindi na aliyeshindwa na ndipo Mahamat alishinda.