Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, wadau waonyesha wasiwasi
Umebakia mwezi mmoja kufikia uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu katika nafasi mbalimbali ikiwemo mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa baraza la kijiji, mwenyekiti wa kitongoji na mwenyekiti wa mtaa.
Katika mchakato huo kuelekea siku ya uchaguzi, tayari hatua mbili zimefanyika ambazo ni uandikishaji wapigakura kwenye daftari la wakazi wa eneo husika huku uchukuaji na urejeshaji wa fomu ukiendelea.
Baada ya hatua hizo, zitafuata hatua nyingine ambazo ni pamoja na uteuzi wa wagombea, usikilizaji wa mapingamizi, kampeni za uchaguzi na hatimaye siku yenyewe ya uchaguzi kama ilivyotangwa na Serikali.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, Watanzania milioni 31 sawa na asilimia 94 wamejiandikisha katika daftari la wakazi kwa ajili ya kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.
Kati ya Watanzania waliojiandikisha, asilimia 48.71 ni wanaume huku asilimia 51.29 ni wanawake. Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri, mikoa yote 26 ya Tanzania imefanya kazi vizuri katika kuwaandikisha wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi huo.
Tathmini ya wadau
Wakitoa tathmini yao kuhusu mwenendo wa mchakato wa uchaguzi huo hadi kufikia sasa, wadau mbalimbali wa uchaguzi huo wamebainisha kwamba uchaguzi huo hautakuwa mzuri kutokana na hila zinazofanyika kwenye mchakato huo.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya akitoa tathimini ya hatua mbili zilizopita akisema hazileti taswira njema huku akitabiri uchaguzi ujao utakuwa mbaya kuliko uliofanyika mwaka 2019.
“Tatizo wasimamizi hawazingatii kanuni na miongozo iliyoweka, viongozi wa chama tawala wamekuwa wakihodhi michakato na tulitoa malalamiko kwa Waziri kwa kuandika barua mbili lakini alijibu moja tu,” anasema.
Sakaya anabainisha kuwa mchakato wa uchaguzi huo ulianza na uandikishwaji wa daftari la wakazi ili kupata orodha ya watu wanaotakiwa kupiga kura kupata viongozi makini wenye uwezo wa kuongoza.
“Uandikishwaji wenyewe ulikuwa mbovu na jambo la kusikitisha, CUF tulipaza sauti zetu kuanzia Oktoba 12, mwaka huu baada ya kuona hujuma kwenye vituo vilivyotengwa, na tuliwataka viongozi waiingilie,” anasema Sakaya.
Sakaya anasema walipaza sauti wakitaka 4R za Rais Samia Suluhu Hassan alizoanzisha zitekelezwe kwa vitendo na walienda hadi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuelezea namna utaratibu ulivyopokwa na CCM.
Sakaya aliyekuwa Mbunge wa Kaliua Mkoani Tabora anasema hadi walimu walikuwa wanaruhusiwa kupeleka wanafunzi ambao hawajafikia miaka 18 wanaveshwa nguo za kiraia kwenye vituo kwa ajili ya kuandikishwa.
“Mawakala wa vyama vya upinzani hawakuruhusiwa kuhoji chochote wala kufanya uhakiki wa majina wakati wa kuanza na kuhitimishwa, ulikuwa uchafuzi na hilo ni daftari linaloenda kutoa wapiga kura,” anasema
Naye, Spika wa Bunge la Wananchi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Suzan Lyimo anasema nia ovu imeanza tangu hatua za awali kwa kuweka vikwazo na vigingi vingi.
“Sioni kama kutakuwa na mwanga wowote hali ni tete,jambo nzuri linaanza tangu hatua za mwazo tumefikia kama hatua moja na nusu tumeona vikazo vingi katika hatua ya kwanza ambayo ni muhimu kuliko zinazokuja,” anasema.
Suzan ambaye kitaaluma ni mwalimu, anasema katika ufundishaji kama hujamjengea msingi mzuri mtoto kwenye hatua za mwanzo inakuwa haina maana.
“Hakuta kuwa na nafasi ya watu kuwekewa mapingamizi katika maeneo mengi kwa sababu majina yalibandikwa katika vituo yamebanduliwa na watu watashindwa kwa kukosa ushahidi wa wazi,” anasema
Anasema watu watashindwa kuwakatia watu rufaa kwa kukosa ushahidi wa wazi hadi siku ya Uchaguzi huku akieleza hofu yake hawajui kama viongozi wao watateuliwa baada ya kuchukua fomu na kuzirejesha.
Hoja za wawili hao zilipigiwa chapuo na Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Bob Wangwe ambaye anasema haoni kama haki itazingatiwa hadi kwenye kuhitimishwa kwa uchaguzi huo ili kuwapata viongozi.
“Kumekuwa na malalamiko mengi, maeneo mbalimbali kuna mawakala walikuwa hawapewi idadi na waliokuwa wanaandikisha lakini vilevile baadhi ya maeneo wameandikisha majina ya watu marehemu na wengine kuzuiwa kuandikishwa,” anasema.
Wangwe ambaye ni mwanaharakati anasema kuna wakati mwingine viongozi wa umma kama watendaji wa serikali walikuwa wanaingilia michakato kiasi cha kuchangia dosari nyingi.
“Dosari hizo zinaonyesha huenda uchaguzi hautakuwa wa huru na haki, na uwezekano wa kutokea kuvurugika amani ni mkubwa kwa sababu ikitokea mmoja anamkandamiza mwingine kuna mvutano unajitokeza,”anasema.
Wange anasema inafahamika wazi Tamisemi weledi wake kwenye suala la kusimamia mchakato huo haurishishi lakini bado ilitakiwa kujitahidi katika kufuta makosa mengine ya wazi ambayo yanafanyika hasa kwa upande wa vyama vya upinzani.
“Kinachotakiwa kufanyika ni wananchi kutambua haina ya chombo kinachosimamia uchaguzi wenyewe, kina maslahi na hakijali kimejikita katika kukandamiza haki za wengine,”anasema
Wange miongoni mwa waliopeleka kesi Mahakamani kupinga Tamisemi kusimamia Uchaguzi huo anasema taasisi hiyo bado si chombo kinachojali na kinaweza kusimamia haki kutendeka.
“Kikubwa wananchi wanapaswa kuwa macho,katika kujitokeza kupiga kura na kulinda kura zao na pale wanapohitajika kutumia nguvu kulinda haki wasisite kufanya hivyo,”anasema Wangwe
Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, Haji Ambar Khamis anasema kwa kuwa viongozi wamejithatiti uchaguzi utakuwa na uhuru na haki anawaamini.
“Wito wangu kwa vyama vingine vishiriki uchaguzi kwa nia njema kwa lengo kuwa uchaguzi utakuwa wa uhuru na haki na utakuwa mfano wa kuigwa kwa nchi nzingine,” anasema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatibu anasema vinara wa kuvuruga michakato kiasi cha kuonekana dosari nyingi ni watendaji wa chini ikiwemo wakurugenzi.
“Uchaguzi ni jambo la wananchi wanatakiwa kuchagua viongozi wao wa kuwachangua katika maeneo yao ili kuwaletea maendeleo ni muhimu Tamisemi kuwasikiliza wadao wao vyama vya siasa na kuzitatua changamoto wanazolalamikia,” anasema.
Khatibu anasema katika kutatua dosari hizo wanapaswa kuwa karibu na vyama vya siasa na kuzichambua kwa njia ya mazungumzo huku akieleza imani yake Serikali ni sikivu.
“Tatizo liko chini kwa wakurugenzi wanaosimamia uchaguzi hawazingatii sheria na kanuni tulizozipitisha wote pamoja na wizara, lakini mitaani na vijijini kumekuwa na shida watendaji wanajiamulia tu cha kufanya,” anasema.
Khatibu anasema uchaguzi huo ni kioo katika uchaguzi ujao wa mwaka 2025 hivyo ni muhimu ufanyike kwa uwazi kwa kuzingatia uhuru na haki kwa kuondoa dosari zote.
“Shida ni baadhi ya watendaji kwa maksudi wamekuwa wakipindisha sheria kwa maslahi yao binafsi, wanatakiwa kufuata utaratibu na miongozo katika kuendesha uchaguzi huu hatutaki zitokee vurugu,” anasema.