Prime
KONA YA MALOTO: UVCCM wanavyogeuka ‘wapangaji’ kwenye nyumba yao ya chama

Chama cha Mapinduzi (CCM), kimetawala mitandao ya kijamii. Uchukuaji fomu za kuwania ubunge na udiwani, ni mada ambayo inajadiliwa na wengi. Kuanzia aina waliojitokeza hadi idadi kubwa ya wanaoomba uteuzi wa kuwa wagombea.
Watu ni wengi na mseto ni mpana, maana wamejitokeza wa kila aina. Ni fursa nzuri kwa wajumbe wa CCM kuchuja na kupata walio bora. Kinachotakiwa ni uchujaji uwe wa haki. Watakaopitishwa wawe bora.
Mshangao mkubwa kwa mchakato unavyoendelea ni kuona watu wengi, wazee, watu wa makamo hadi vijana, wanachuana kuchukua fomu na kurejesha.
Vijana wanaofungamana moja kwa moja na Umoja wa Vijana Chama cha Mapinduzi (UVCCM), wanakuwa nyuma.
Mtazamo kuwa vijana wanapaswa kushika nafasi za uongozi, uiguse UVCCM. Mbona watu, tena vijana, ambao hawajapita UVCM, wanakuwa na uthubutu mkubwa wa kujitokeza kuwania ubunge na udiwani? Wao wana-UVCCM wanapokeaje?
Ingepaswa, baada ya kipyenga kupulizwa CCM, mlango kufunguliwa na watu kujitokeza kuomba uteuzi wa chama kuwa wagombea wa nafasi za uongozi, vijana wa UVCCM wangepaswa kuongoza msafara.
Ni kwa sababu UVCCM, ni jiko la kupika vijana kuwa viongozi. Hivyo, nafasi za uongozi CCM, vijana wa UVCCM ndiyo nyumbani kwao. Wanatakiwa kujipa na kupewa kipaumbele. Kukaa nyuma, halafu wengine wasio na historia na UVCCM kuchangamkua fursa, ni sawa na mtoto kugeuka mpangaji nyumbani.
Usahihi wa mantiki
Oktoba 2, 1920, Kiongozi wa zamani wa Urusi na Dola ya Umoja wa Kisovieti (USSR), Vladimir Lenin, alihutubia Jumuiya ya Vijana wa Kikomunisti wa Urusi na kueleza kuwa majukumu ya jumuiya yoyote ile ya vijana, yanapaswa kuwekwa kwenye neno moja; Kujifunza.
Lenin ambaye jina lake ndilo ambalo limebeba falsafa za Leninism, aliwaambia vijana wa jumuiya hiyo kwa wakati huo kuwa pamoja na kila kitu, wanatakiwa kujifunza na kuziishi itikadi za kikomunisti ili waweze kuutetea ukomunisti dhidi ya ubepari.
Aya hizo mbili, zinatosha kutoa tafsiri ya kile ambacho Lenin alikisema, ni kwamba jumuiya za vijana zipo kwa ajili ya maandalizi ya vijana kuwa viongozi bora kupitia itikadi na falsafa ambazo wanapitishwa katika makuzi yao ya kiuongozi.
Mwaka 1944, mashujaa wa wakati wote wa Taifa la Afrika Kusini, Ashley Peter Mda, Walter Sisulu na Oliver Tambo, walipokuwa wanaanzisha Jumuiya ya Vijana ya ANC (ANC Youth League), walieleza malengo yake kuwa jumuiya hiyo ifanye kazi kama kiwanda cha kuchakata fikra za vijana ili wawe viongozi bora wa kizazi kipya.
Kwamba pamoja na shabaha ya ANC Youth League kuwaunganisha vijana na kuchochea hamasa yenye wigo mpana katika mapambano dhidi ya makaburu na utawala wao wa ubaguzi wa rangi, muhimu zaidi ni kuwaandaa kuwa viongozi wenye busara na wazalendo kwa nchi yao.
Kitabu kuhusu uanzishwaji wa Jumuiya ya Vijana cha chama tawala cha Namibia, Swapo (Swapo Youth League), kinaeleza kuwa madhumuni yake ni kuwapika vijana kuwa wanajeshi imara wenye kujifunga mkanda kwa ajili ya kutetea itikadi za Swapo, vilevile kuwa viongozi wazuri nyakati zijazo.
Turudi kwenye tafsiri ya Lenin, ni kwamba palipo na kila jumuiya ya vijana, maana yake ni chuo cha mafunzo ambayo huwawezesha vijana kufuzu maono ambayo yanakuwa yamekusudiwa.
Hata Jumuiya ya Vijana ya Tanu (Tanu Youth League) na baadaye Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), shabaha yake ilikuwa ni kupika vijana kiitikadi, kiuongozi, vilevile kuwatengeneza kuwa wazalendo kwa nchi yao.
Hiyo ikawa sababu majukumu mengi yaliyokuwa yakitekelezwa na Tanu, wakati huo, kuingizwa kwenye mpango wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa wahitimu wa elimu ya kidato cha sita ili kuwajenga vijana kikakamavu, kuwa viongozi wazuri na wazalendo kwa taifa lao.
Kuna shida UVCCM?
Juni 4, 2015, Taasisi ya Utafiti ya Gallup, Marekani, ilitoa ripoti yenye kichwa; "Leadership Talent Is Scarce in Southeast Asia", yaani kipaji cha uongozi kinaadimika Kusini-Mashariki ya Asia.
Ripoti hiyo ilieleza kuwa ndani ya nchi kumi zinazounda Chama cha Mataifa ya Kusini-Mashariki ya Asia (ASEAN); Brunei, Cambodia, Indonesia, Laos, Malaysia, Myanmar, Ufilipino, Singapore, Thailand na Vietnam, kipaji cha uongozi kimekuwa adimu. Ripoti hiyo ni kabla ya Mahathir Mohamad kuchaguliwa Waziri Mkuu wa Malaysia kwa mara ya pili, akiwa na umri wa miaka 93, Mei 2018.
Tanzania hakuna ripoti yenye kuonesha kuchanua au kuadimika kwa vipaji vya uongozi. Hata hivyo, jinsi UVCCM inavyobaki nyuma dhidi ya makundi mengine, wasiwasi unakuja je, wajibu wa kupika vijana kuwa viongozi kupitia UVCCM umesahaulika, au jiko haliivishi kwa sababu vipaji vimekuwa adimu Tanzania?
Imani yangu ni kuwa vijana ambao wamepata maandalizi mazuri, wanaweza kuwa mfano bora wa uongozi, kuliko wanaojilea wenyewe. Haina maana nadharau vipaji, la hash! Wapo wengi wazuri, wasomi na wasio wasomi, lakini aliyeandaliwa na kuiva, hutoa ahadi njema zaidi.
UVCCM wanatakiwa wakati wote kuwa mstari wa mbele kufukuzia nafasi za uongozi, kwa sababu wao ndiyo lengo na lango la uongozi wa kesho kupitia CCM. Kubaki nyuma ni kuyaacha madhumuni ya uwepo wao yabebwe na wengine.
Vijana wa sasa UVCCM wanatakiwa kujitafakari wao ni nani na wana faida gani kwa chama chao na nchi, ikiwa hawajitokezi kuwania uongozi. Wajiulize kuhusu umuhimu wao, ikiwa wengi nje ya mkondo wa UVCCM ndiyo wanachangamkia fursa na kuwa viongozi, halafu wao wanakuwa watazamaji.