KONA YA MALOTO: Mawakili TLS wamechagua kuiweka siasa juu ya taaluma yao

Mawakili wakifurahia ushindi wa rais mpya wa chama chao (TLS), Boniface Mwabukusi. Picha na Hamis Mniha
Jumuiya ya Wanasheria Tanganyika (TLS), ilipata viongozi wake Ijumaa, Agosti 2, 2024. Wakili Boniface Mwabukusi, alichaguliwa kuwa Rais wa TLS kwa muhula wa miaka mitatu. Alimshinda mpinzani wake wa karibu, Sweetbert Nkuba.
Wengine ambao Mwabukusi aliwashinda ni Revocutus Kuuli, Ibrahim Bendera, Paul Kaunda na Emmanuel Muga. Uchaguzi huo ulifanyika kwenye Ukumbi wa CCM Jakaya Kikwete, Dodoma.
Joto la kisiasa lilikuwa kali kuelekea uchaguzi. Kwa tafsiri ya wengi, vyama viwili, CCM na Chadema, kila kimoja kilikuwa kinatafuta ushindi ndani ya TLS. Chadema wakionekana kuweka karata yao kwa Mwabukusi, wakati Nkuba, alibeba matumaini ya CCM. Uchaguzi wa TLS 2024, unafanana na ule wa mwaka 2017.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu, aliwania urais wa TLS. Wakati huo, Lissu alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Chadema, vilevile mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya chama hicho.
Mtu wa pili aliyegonganisha vyama mwaka 2017 ni Godwin Mwapongo, yeye ni mwanachama wa CCM na alikuwa mmoja wa watu 38 waliochukua na kurudisha fomu za kuomba tiketi ya kuwa mgombea Urais wa CCM mwaka 2015. Mwabukusi, kuelekea kushinda urais wa TLS, alikutana na vikwazo vingi, ikiwemo jina lake kuondolewa na kamati ya maadili. Hata hivyo, alipambana mpaka mahakamani, akashinda na jina lake kurejeshwa miongoni mwa wagombea.
Lissu naye alikutana na vikwazo. Aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe, alitishia kuifuta TLS. Mwisho, Lissu alivuka vikwazo, aligombea na kushinda.
Kwa nini michuano ya kisiasa ndani ya TLS? Kujibu swali hilo, nitaelekea kwanza kwenye asili na siasa Tanzania. Kutotambua mahali gani pa kutofautiana kisiasa, husababisha tofauti hizo ziibuke katika masuala nyeti, yenye kufaa kuwaweka watu pamoja.
Mathalan, mwaka 2020, kipindi cha janga la Covid-19, ulitokea mvutano baina ya CCM na vyama vya upinzani. Wabunge wa Chadema, walitangaza kuondoka bungeni kwenda kujifungia ili kukwepa maambukizi. CCM, wao wakang’ang’ana bungeni, na walipopata nafasi ya kuzungumza, waliwapiga vijembe wenzao.
Aprili na Mei 2020, vifo mfululizo vilitokea miongoni mwa wabunge; Gertrude Rwakatare, viti maalumu, Aprili 20, 2020. Richard Ndassa, jimbo la Sumve, Aprili 29, 2020. Augustine Mahiga, mbunge wa kuteuliwa na Waziri wa Katiba na Sheria, alifariki dunia Mei Mosi, 2020. Haikuelezwa kama sababu ya vifo vyao ilikuwa Covid-19, ila hali ilitisha.
Hivyo, asili na siasa Tanzania, husababisha malumbano ya kisiasa mahali pa kutoa sauti moja. Watu wanapotea au kupotezwa, badala ya kuungana kuwa na sauti moja kubwa kuhakikisha haki inatendeka, lakini sauti za malumbano zitasikika. Watanzania hawajui wapi pa kulumbana, mahali gani pa kuelewana.
TLS, kwa kuwa jumuiya ya mawakili, haipaswi kuwa jukwaa la kushindana kisiasa, badala yake inatakiwa kuwaunganisha wanasheria wa vyama vyote, hadi wasio na itikadi za kisiasa, kwa madhumuni ya kuhakikisha taaluma ya sheria inapata heshima yake stahiki.
Kwa kifupi, mawakili wanatakiwa kuiweka taaluma ya sheria mbele. Halafu, waitumie taaluma hiyo kunyoosha siasa za nchi. Tatizo, jinsi ambavyo mawakili huonekana kutekwa na siasa kuelekea uchaguzi, inatoa taswira wao wenyewe wanaiweka siasa juu ya taaluma yao ya sheria.
Baada ya Mwabukusi kushinda, ipo video ilimwonesha mtu akitamba ‘tumeshinda’ halafu Lissu anaongeza: “Siyo tumeshinda, tumeshinda kwenye ukumbi wao.” Ukumbi wa CCM Jakaya Kikwete, unamilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM). Kauli ya Lissu ilithibitisha uwepo wa ushindani wa siasa. Wanasheria kutanguliza siasa kuliko sheria ni hatari. Mawakili wanao wajibu mkubwa wa kuhakikisha siasa haziyumbishi taaluma yao.
Mawakili ni watu wenye hadhi kubwa Tanzania na jamii yoyote duniani. Mawakili ni daraja la tafsiri bora na sahihi ya kisheria.
Mawakili ni jamii inayorahisisha kuonekana kwa haki ndani ya mahakama, ni maofisa wa mahakama, kwa weledi, uzoefu na maarifa yao katika taaluma ya sheria. Wakili ambaye ameifanya kazi yake kwa miaka 10, ana sifa ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.
Katiba ya Tanzania, ibara ya 109, ibara ndogo za 7, 8 na 9, imechambuliwa vizuri.
Inaeleza Rais anaweza kumteua mtu kuwa Jaji wa Mahakama Kuu akiwa na sifa maalumu na sifa hiyo maalumu awe amekuwa nayo kwa kipindi cha miaka 10. Ibara ndogo ya 8, inafafanua sifa maalumu ya mtu kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, ni zile ambazo zimefafanuliwa kwenye Sheria ya Mawakili, kwamba lazima mtu awe nazo ili aweze kuandikishwa kama wakili Tanzania Bara.
Ibara ndogo ya 9, inatoa fursa kwa Rais kumteua wakili yeyote hata kama hajafikisha umri wa miaka 10 kazini, ikiwa anaona anafaa na imempendeza awe Jaji wa Mahakama, baada ya kushauriana na Tume ya Kuajiri ya Mahakama.
Ukisoma pia Sheria ya Mawikili Tanzania, wakili ili atambuliwe na kuruhusiwa kufanya shughuli zake za kiutetezi mahakamani (uofisa wa mahakama), lazima athibitishwe na Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu pamoja na kumwapisha wakili, ili kumthibitisha na kumpa cheti cha uwakili ni lazima wakili awe na vigezo vya kitaaluma vinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria, vilevile awe na leseni hai ya biashara lakini pia atambulike kuwa mwanachama wa TLS.
TLS ni Chama cha Mawakili Tanganyika. Hivyo, heshima ya chama hicho ni kuwa mtu hawi wakili bila kujiunga nacho. Na kwa vile Jaji wa Mahakama Kuu hapati sifa za kuteuliwa nafasi hiyo mpaka atimize vigezo vya uwakili, basi TLS ni sawa ikiitwa njiapanda ya ujaji. Siasa zimesababisha siku hizi vyama vya uwakili viongezeke. Wapo wanaoiona TLS ni ya wapinzani. Hata hivyo, wito kwa mawakili ni kuipenda, kuiheshimu na kuilinda taaluma ya sheria kwa wivu mkubwa. Ni kweli kwenye siasa kuna fursa, ila vema malengo ya TLS yabaki yaleyale yaliyopo kwenye nyaraka.
Serikali wala CCM, hawatakiwi kuitumia TLS kwa masilahi yao.
Wapinzani, hawapaswi kuiona TLS kama jukwaa la kuikabili CCM na Serikali. Uchaguzi TLS ubebe agenda za kisheria, masilahi ya wanasheria na Watanzania. Siasa zinapoendesha uchaguzi, inatoa picha kuwa taaluma ya sheria imewekwa chini ya siasa.