Prime
Kivuli cha Mbowe kinavyoitesa Chadema

Muktasari:
- Januari 21, 2025, wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walifanya uchaguzi wa viongozi mbalimbali ngazi ya Taifa, na Tundu Lissu akaibuka mshindi, akihitimisha safari ya miaka 21 ya uongozi wa Freeman Mbowe.
Dar es Salaam. Licha ya uamuzi wa kukaa kimya kwa aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kuhusu yanayoendelea ndani ya chama hicho, kivuli chake kimeendelea kuwa mwiba wenye athari lukuki.
Dhana na hisia kuwa yuko nyuma ya makundi yanayopingana mitazamo na uongozi wa sasa wa chama hicho zimeendelea kugubika fikra za wengi, huku ukimya ukiwa ndiyo uliobaki kuwa jawabu pekee la Mbowe kuhusu yote yanayoendelea.
Amebaki kimya hata katikati ya nyakati ambazo yuko nje ya uongozi wa chama hicho, lakini matusi, kebehi na mashambulizi ya kisiasa yanatupwa dhidi yake, jambo ambalo wadau wa siasa wanalihusisha na kubaki kwa kivuli chake ndani ya Chadema.
Ni kivuli cha Mbowe kwa sababu, licha ya ukimya wake, jina lake limeendelea kusikika katika ndimi za makundi yanayokihama chama hicho, wakisema hatua yao ya kumuunga mkono imewafanya waonekane kama wasaliti kiasi cha kuishi mithili ya watoto wa kambo ndani ya Chadema.
Mzizi wa yote hayo ni uchaguzi wa ndani wa chama hicho uliofanyika Januari 21, 2025, uliowakutanisha Mbowe na Tundu Lissu, aliyeibuka mshindi katikati ya hisia kuwa angeshindwa.
Dalili za kugawanyika kwa chama hicho zilianza wakati wa kampeni, Lissu akirusha vijembe mbalimbali kuonyesha udhaifu wa Mbowe, hatimaye kukawa na makundi mawili yaliyosigana vikali.
Makundi hayo kati ya lile la Mbowe na la Lissu yameendelea kuwepo hata baada ya uchaguzi huo, jambo linalosababisha kivuli cha mwenyekiti huyo mstaafu kiendelee kuwepo hata baada ya kung’atuka kwake.
Moja ya hotuba za mwisho za Mbowe ni ile ya Januari 22, 2025, wakati akiwaaga wajumbe wa mkutano mkuu baada ya kushindwa uchaguzi. Mwanasiasa huyo mkongwe alitoa wito kwa viongozi wapya kuhakikisha wanaona haja na nia ya kuwaunganisha.
Alisema hatua hiyo inatokana na “kukanyagana” kulikotokana na kampeni za uchaguzi huo, akishauri kuundwa kwa kamati ya ukweli na upatanishi.
Ni kwa ushauri huo, katika mijadala mbalimbali, wamekuwa wakitaka hilo lifanyike, lasivyo chama kitaendelea kutetereka. Hata wale wanaotangaza kuhama wakidaiwa kwenda Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), wanamtaja Mbowe.
Mwananchi kwa nyakati tofauti limemtafuta Mbowe ili kupata mtazamo wake wa kinachoendelea bila mafanikio, kwani simu zake zinaita bila kupokelewa, na hata akitumiwa ujumbe mfupi wa maandishi haupati majibu.
Mmoja wa viongozi waandamizi wa chama hicho, aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake, amesema:“Kilichotokea kwenye uchaguzi wetu kilimuumiza sana Mbowe, aliumia kwa kusingiziwa mambo mengi. Na waliopo madarakani... sijui kala asali, sijui fedha za nani. Sasa ameamua kukaa kimya.”
“Licha ya yeye (Mbowe) kuwa mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu, hajawahi kushiriki kikao chochote. Unajua Mbowe ni kama taasisi. Kumtusi, kumbagaza hakusaidii, zaidi kinatuteteresha sana. Yaani jamaa kukaa kimya anakitesa chama,” anasema.
Kiongozi huyo ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu amesema: “Tunawajibu mkubwa wa kupambana kwa kweli. Unajua hata kura za Lissu na Mbowe walipishana kura 31 tu, kwa hiyo Mbowe bado ana nguvu. Uongozi wa sasa unapaswa kulijua hilo.”
Katika uchaguzi huo, Lissu alipata kura 513, Mbowe akipata 481, huku Charles Odero akipata kura moja. Jumla ya kura zilikuwa 999 na kura tatu ziliharibika.
Alichokisema Mnyika
Baada ya mjadala mkali mtandaoni, hasa kutokana na waliokuwa wajumbe wa Sekretarieti ya chama hicho kutangaza kukihama, wakisema chama kimepoteza mwelekeo kwa kuingia uongozi wa Lissu, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akaandika kile alichozungumza na Mbowe.
Mnyika, akitumia ukurasa wake wa X, aliandika maelezo marefu Mei 8, 2025, akisema: “Nimewasiliana na mwenyekiti mstaafu, Freeman Mbowe. Amenieleza hana dhamira ya kugombea urais, ubunge au uongozi wa chama chochote cha siasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.”
“Natambua kuwa wachache waliojiondoa Chadema, baadhi yao wamekuwa wakitumia jina lake kushawishi baadhi ya viongozi wa chama na wenye nia ya kugombea kujiondoa kwenye chama kwa madai anawaunga mkono na anajiandaa kugombea urais kupitia chama kingine.”
Katika maelezo yake, Mnyika amesema: “Kwa uzoefu wangu wa kuwa kwenye Sekretarieti ya chama kwa takribani miaka 21, tumepitia mapito mengi ya Chadema ambayo tulifanikiwa kuyashinda. Hii vita dhidi ya Chadema naamini pia tutaishinda. Tuelekeze nguvu kwenye mapambano ya No Reforms No Election.”
Ukimya wake una pande mbili
Inawezekana Mbowe akawa sehemu ya yanayoendelea ndani ya Chadema, au asihusike kabisa kwa kuwa yuko kimya, hivyo hakuna mwenye ithibati ya lolote kati ya hayo, kwa mujibu wa mtazamo wa mchambuzi wa masuala ya siasa, Kiama Mwaimu.
Kwa mujibu wa Mwaimu, ukimya wa Mbowe unatosha kuwa ushahidi kuwa anahusika, kwa kuwa kama kiongozi mwandamizi alipaswa kukemea, lakini bado huwezi kuthibitisha kuwa anahusika.
“Ni vigumu kuthibitisha kwamba Mbowe anahusika, lakini ushahidi wa kimazingira unaonyesha ukimya wake si wa kupumzika bali ndani yake una kitu.”
“Tangu mambo haya yaanze, Mbowe hajakemea wala kukana hadharani. Sasa kwamba mambo haya mawili, ushahidi wa mazingira unaonyesha huenda akawa anahusika na mpango huu kutokana na ukimya wake,” amesema Mwaimu.
Katika mazingira ya sasa ya chama hicho, mchambuzi huyo wa siasa ameusihi uongozi wa chama hicho kujikita katika kujenga chama badala ya kumpopoa Mbowe aliyekaa kimya, akisisitiza kufanya hivyo ni kupoteza muda.
“Wasijaribu kufanya hivyo, watapoteza muda. Wajikite kuzungumzia hoja zao ili waendelee kuaminika mbele ya umma, kama wanavyofanya hivi sasa, ingawa mengine wanaongeza chumvi. Mbowe wasimzungumze kwa lolote maana mengine watakuwa wanamtuhumu bure,” amesema Mwaimu.
Wanaokerwa na anavyotukanwa
Mashambulizi ya kisiasa dhidi ya Mbowe kutoka kwa baadhi ya wanachama na viongozi wa Chadema yameonekana kuwakera baadhi, akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani, Boniface Jacob maarufu Boni Yai.
Hilo limethibitishwa kupitia chapisho lake katika ukurasa wake wa X (zamani Twitter), alilolipa kichwa cha habari cha “Ni nani katuroga...?”
Katika chapisho hilo aliloliambatanisha na picha ya Mbowe, Jacob amehoji inakuwaje watu wanahangaika na kiongozi huyo mstaafu ilhali amejikita katika biashara zake binafsi kwa asilimia 99.
“Kumzushia uongo, kumdhihaki, kumtukana na kumdhalilisha ndiyo imekuwa fasheni mpya ya baadhi ya watu wakitaka waonekane wajuaji na wenye mapenzi na Chadema kuliko wengine.”
“Huwezi kujifanya unaipenda Chadema kama unataka ikose internal stability (utulivu wa ndani) kwa kutengeneza vistori vya uongo.”
Amesema uzushi, kejeli, vijembe na dhihaka kwa viongozi ni mradi mpya wa kuwagawa wanachama, na kwamba watagawanyika kweli iwapo watayaendeleza.
Amesisitiza kuwa wanaofanya kazi ya kuwagawa wamewekeza ufundi kuhakikisha Chadema hairudi kuwa moja, licha ya juhudi za mwenyekiti wa sasa, Tundu Lissu, kutaka kuwaunganisha kabla hajakamatwa.
“Mwenyekiti Lissu akaunda kamati ya wazee kurudisha umoja wetu, kazi ambayo ilishaaanza vizuri. Wazee wale wanaendelea kuifanya kazi hiyo. Nasikitika baadhi yetu wanahujumu jitihada za mwenyekiti,” ameandika Jacob.
Ukiacha Jacob, matusi dhidi ya Mbowe yameonekana kumkera pia Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kichama wa Kinondoni, Henry Kilewo. Yeye ameandika: “Tuonyeshe ubora wa kujenga hoja na kuzitetea, tuonyeshe ubora wa uvumilivu na ustahimilivu wa kisiasa. Matusi, kejeli, vijembe siyo utamaduni kwa taasisi iliyopika maelfu kwa mamia ya vijana wenye uwezo na ushawishi.”
“Ni bahati mbaya sana kushuhudia hapa tulipo leo, hata watangulizi wetu tunawashambulia wenyewe kana kwamba ni maadui zetu. Pole sana Chairman wa awamu ya tatu, Freeman Mbowe, kwa hiki unachokiona.
“Najua unajiuliza nini kimekipata chama chako, lakini ukimya wako ni jibu tosha. Endelea na mapumziko yako na biashara zako. Ulitimiza wajibu wako kwa weledi wa hali ya juu.”
Kada mwingine wa chama hicho, Yericko Nyerere, ameandika katika moja ya kundi sogosi la WhatsApp kuwa Mbowe ndiye anayetukanwa huku wanachama wakipiga makofi.
“Mbowe aliwakosea nini enyi watu hadi leo mpo kwenye kampeni tu za kumtukana? Kampeni za uchaguzi bado ziko vinywani mwenu tu? Mmeshindwa kuunganisha wanachama, sasa wanaamua kuondoka, matusi mnayapeleka kwa Mbowe,” ameandika.
Yericko, katika andiko hilo, amemsihi Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche, kuunganisha chama na kuwaonya vijana wanaomtusi Mbowe.
Ujumbe wenye maudhui ya kupinga matusi dhidi ya Mbowe ulichapishwa pia na Katibu Mkuu mstaafu wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Catherine Ruge, na wengine kadhaa kupitia mitandao ya kijamii.
Wapo walioshindwa kuvumilia
Ukiacha wanaojibu hadharani, yapo makundi ya wanachama waliokuwa wafuasi wa Mbowe waliotangaza kukihama chama hicho, ambao hadi sasa ni zaidi ya 20. Miongoni mwao ni Ruge, John Mrema aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki na Mambo ya Ndani wa chama hicho.
Pia, wapo weka hazina, makatibu na maofisa wa chama hicho kutoka kanda nane za Chadema, na wanataja kutengwa na kuonekana wasaliti kwa kumuunga mkono Mbowe kuwa moja ya sababu za kuondoka kwao.
Ingawa sababu kuu ni nia ya kugombea nafasi mbalimbali katikati ya msimamo wa Chadema wa kuzuia uchaguzi kupitia ajenda ya No Reforms No Election, lakini jina la Mbowe linaendelea kutajwa.