Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kunje wa AAFP mguu sawa kinyang’anyiro urais 2025

Dar es Salaam. Chama cha siasa cha Wakulima (AAFP) leo kimemteua rasmi kada wake, Kunje Ngombale-Mwiru kuwa mgombea wa urais atakayewakilisha chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Hata hivyo, chama hicho kimeshindwa kumpata mgombea urais upande wa Zanzibar baada ya aliyekuwa anawania nafasi hiyo, Said Soud kupigiwa kura nyingi za hapana.

Hivyo, uongozi utalazimika kuitisha mkutano mkuu maalumu utakaoketi kumchagua na kumpitisha mgombea mwingine atakayepeperusha bendera ya chama hicho upande wa Zanzibar.

Katika uchaguzi huo uliogubikwa na vimbwanga vya aina yake, Kinje alichaguliwa baada ya kupata kura70 kati ya 97 zilizopigwa huku washindani wake wawili ambao ni Kilasa Mohamed, akiambulia kura sita na Fatuma Geheka kura sita pia na tano zikiharibika.

Katika mkutano mkuu huo maalumu, uliokuwa unaangaliwa kwa karibu na Naibu Msajili wa Vyama Vya Siasa, Sisty Nyahoza, kada Kinje ataambatana na mgombea mwenza wake aliyepitishwa na mkutano huo, Chuma Mohamed.


Soud agomea uchaguzi huo

Katika kile ambacho hakikutarajiwa na wengi, aliyekuwa anagombea nafasi ya urais upande wa Zanzibar, Soud aligeuka mbogo baada ya kudai kuna mtu ndani ya chama hicho ameendesha siasa chafu dhidi yake kusudi asichaguliwe.

“Haiwezekani nipate kura sita halafu zote za kutoka upande wa Zanzibar, nimefanyiwa uhuni na mchakato huu wa uchaguzi sikubaliani nao, haiingii akilini na waliopiga kura nawajua kuna mchezo umechezwa ili mimi nisipate nafasi ya kugombea kwa sababu nimekuwa mwiba kule Zanzibar,” amedai Soud mkutanoni hapo.

Kinje Ngombale-Mwiru aliyesimama katikati  mgombea nafasi ya urais   uchaguzi mkuu 2025 kupitia chama cha Wakulima (AAFP)

Amesema hakubalini na mchakato huku akieleza yeye ni mzoefu ndani ya chama hicho na aliyefanya uhuni huo anamjua na asingependa kumwaga mchele kwenye kuku wengi.

“Namjua na nina akili si mtoto mdogo kwenye siasa, nataka kukijenga hiki chama ndiyo maana nimekuwa muwazi na siwezi kuficha uovu kazi yangu ni kuhakikisha chama kinakuwa na si mamruki,” amesema Soud.

Amesema  anaendelea kutafakari kabla ya kuchukua uamuzi mwingine huku akisisitiza hawezi kukubali kuchezewa mchezo wa kihuni.

Wakati mvutano huo ukiendelea, Naibu Msajili Nyahoza alijaribu kuingilia kati kutaka kupata usuluhishi ili wakamilishe mchakato huo, Soud aliwataka wajumbe wake aliosafiri nao kutoka Zanzibar, watoke ukumbini wakapande daladala aliyoikodi waondoke.

“Siwezi kuwaacha wajumbe wangu hapa, hawa ni wake za watu na tulishakata tiketi wanatakiwa kuondoka saa 10 jioni, wasipofika kule wanaume zao mimi watanielewaje au mnataka nisiwe na wajumbe, nasema wote chukueni mabegi yenu twendeni,” ameamuru Soud.

Akizungumza baada ya kuzuka kwa tafrani hiyo, Nyahoza  ameushauri uongozi uitishe mchakato mwingine ili kumpata mgombea nafasi ya urais upande wa Zanzibar.

“Pamoja na kwamba mambo yamekwama bado mnayo fursa ya kuitisha mkutano mwingine kwa mujibu wa katiba yenu ili mpate mgombea mwingine, lakini kwa mujibu wa sheria, mgombea wa urais upande wa Zanzibar anaweza hata kuchaguliwa na halmashauri kuu ya chama chenu,” amesema Nyahoza.

Amesema kwa kuwa katiba yao haitambui halmashauri kuu inawalazimu kuitisha mkutano mkuu mwingine kupata mgombea wa urais ingawa kwa sheria za nchi zetu hazilazimishi kufanya hivyo.

“Ndiyo maana kuna chama kimoja kimesema hakishiriki uchaguzi wanajiandaa na uchaguzi wa 2030, mwaka huu wamesema wao hawataki kushiriki uchaguzi na hiyo ni hiari  yao lakini kwa vyama 18 vinavyojiandaa na uchaguzi fursa wanayo kutafuta wagombea,”amesema.

Akizungumzia uchaguzi huo, Nyahoza amesema umeenda vizuri na kura zilikuwa zinapigwa na kuhesabiwa hadharani huku akieleza hakuna mtu aliyemuona analalamikia upigaji kura.

Kada wa Chama cha AAFP, Said Soud aliyekuwa mgombea nafasi ya Urais akizungumza na Msajili Msaidizi Sisty Nyahoza baada ya kususia mkutano huo kwakile alichodai amefanyiwa uhuni ili asishinde nafasi ya kupeperusha bendera ya chama hicho upande wa Zanzibar

“Isipokuwa wanalalamikiana wenyewe huyu hakunipigia kura na ni mambo ya kawaida kwenye ushindani, lakini hakuna anayelalamikia kwenye upigaji kura au jinsi zilivyokuwa zinahesabiwa,” amesema.