Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Katibu wa Bavicha akamatwa madai ya kuhamasisha maandamano

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi limethibitisha kumshikilia kiongozi huyo kwa mahojiano.

Shinyanga. Taharuki imeibuka katika eneo la Ndala, Manispaa ya Shinyanga, baada ya Katibu wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) Wilaya ya Shinyanga, Alfred Masanja, kuchukuliwa nyumbani kwake usiku wa kuamkia leo na watu waliofunika nyuso zao.

Taarifa za tukio hilo, zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii tangu alfajiri ya Julai 17, 2026, zikieleza kuwa kiongozi huyo wa vijana wa Chadema alichukuliwa na watu wasiojulikana waliotumia gari lisilo na namba za usajili.

Kutokana na taarifa hizo kuzua maswali mengi, Mwananchi ilifanya ufuatiliaji kwa viongozi wa chama hicho na Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ili kuthibitisha kilichotokea.

Akizungumza kwa simu leo, Julai 17, 2026 Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami amesema tukio hilo lilitokea saa 10 usiku, wakati watu waliokuwa wamefunika sura zao walipofika nyumbani kwa Masanja na kumtaka atoke nje.

Amesema watu hao walikuwa wakitoa vitisho na kudai kuwa iwapo mlango usingefunguliwa wangetumia nguvu kuingia ndani.

“Taarifa tulizozipata zinaonyesha kuwa watu hao walifika nyumbani kwake usiku. Walikuwa wamefunika sura zao na walimtaka atoke nje huku wakitoa vitisho. Mke wake alilazimika kufungua mlango ndipo wakaingia ndani na kuondoka naye,” amesema.

Mazingira ya tukio hilo, amesema yaliwaacha na hofu wanafamilia na baadhi ya majirani waliofahamu kilichokuwa kinaendelea, jambo lililosababisha taarifa za kutekwa kuanza kusambaa.

Mnyawami, amesema baada ya kufuatilia kwa kina walibaini kuwa Masanja alikuwa ameshikiliwa na Jeshi la Polisi, tofauti na hofu ya awali iliyokuwa imejitokeza miongoni mwa wanachama na wananchi.

“Baada ya kupata taarifa hizo na kuona taharuki imeongezeka, tulianza kufanya ufuatiliaji. Baadaye tukagundua kuwa yuko mikononi mwa Polisi. Hata hivyo, wakati huo hatukuwa tumepata sababu rasmi za kukamatwa kwake,” amesema.

Amesema namna ukamataji ulivyofanyika ndiyo iliyochangia wengi kuamini kuwa kiongozi huyo alikuwa ametekwa na watu wasiojulikana.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limethibitisha kumshikilia Masanja mwenye umri wa miaka 43, mkazi wa Kata ya Ndala katika Manispaa ya Shinyanga.

Katika taarifa yake, Polisi walisema Masanja anahojiwa kwa tuhuma za kuchochea maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Julai 7, 2026.

Taarifa hiyo ya leo, Julai 17, 2026 inasema Masanja alihamasisha makundi mbalimbali kushiriki maandamano hayo kutoka maeneo tofauti ya Mkoa wa Shinyanga.

“Tunaendelea na uchunguzi na mahojiano na mtuhumiwa huyo. Uchunguzi kamili utakapokamilika, taratibu stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Hadi wakati wa kuandikwa kwa habari hii, Masanja alikuwa bado anashikiliwa na Jeshi la Polisi huku uchunguzi ukiendelea.