Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kassim Majaliwa: Mwalimu aliyegeuka kiongozi wa Taifa

Muktasari:

  • Ni jina linalobeba simulizi ya maisha ya mtu aliyepanda ngazi ya uongozi si kwa kishindo cha maneno matupu, bali kwa bidii ya kazi na moyo wa huduma.

Dar es Salaam. Katika kurasa za historia ya siasa za Tanzania, jina la Kassim Majaliwa limejichora kwa wino wa uadilifu, utulivu, na uongozi unaotokana na vitendo si porojo.

Ni jina linalobeba simulizi ya maisha ya mtu aliyepanda ngazi ya uongozi si kwa kishindo cha maneno matupu, bali kwa bidii ya kazi na moyo wa huduma.

Safari yake ilianzia katika madarasa ya shule ya msingi, si kama mwanafunzi tu bali kama mwalimu, akitumia kalamu na ubao kuwasha taa ya maarifa kwa kizazi cha baadaye.

Kutoka darasani, akaanza kupanda ngazi moja baada ya nyingine kwa ustahimilivu na uaminifu, hadi hatimaye kufikia ngazi ya juu kabisa ya utumishi wa umma: Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Majaliwa alizaliwa Desemba 22,  1960 katika Kijiji cha Mnacho, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi. Alikulia katika familia ya maisha ya kawaida, iliyojengwa juu ya misingi ya maadili, nidhamu na ucha Mungu.

Maisha ya utotoni yaliyojaa changamoto za kijijini hayakumzuia kuwa na ndoto kubwa, ndoto ambazo baadaye zilimpeleka hadi kwenye nafasi ya juu kabisa ya uongozi serikalini.

Elimu yake ya msingi aliipata katika Shule ya Msingi Mnacho kati ya mwaka 1970 na 1976, kisha akaendelea na elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Kigonsera, mkoani Ruvuma, kuanzia 1977 hadi 1980.

Baada ya hapo, alijiunga na Chuo cha Ualimu Mtwara, ambako alipata stashahada ya ualimu. Kwa kuwa taaluma ya elimu ilimvutia kwa dhati, mwaka 1994 hadi 1998 alijiendeleza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kuhitimu shahada ya elimu.

Safari ya maarifa haikuishia hapo, kwani mwaka 1999 alikwenda nchini Sweden na kusomea shahada ya uzamili katika elimu.

Majaliwa alianza kazi rasmi ya utumishi wa umma mwaka 1984 kama mwalimu wa shule za msingi katika Wilaya ya Lindi, akihudumu kwa miaka miwili hadi mwaka 1986.

Bidii yake, uadilifu na uwezo wa kufundisha vilimfungulia milango zaidi, na akateuliwa kuwa mwalimu wa walimu katika Chuo cha Ualimu Mtwara, ambako alihudumu kwa muda wa miaka 12, akiwa kielelezo cha weledi na uvumilivu katika sekta ya elimu.

Lakini, Majaliwa hakujifungia tu darasani. Alijihusisha katika harakati za utetezi wa walimu kupitia Chama cha Walimu Tanzania (CWT). Mwaka 2001 alichaguliwa kuwa Kamishna wa Wilaya wa chama hicho, na baadaye kuwa Katibu wa Mkoa, nafasi ambazo zilimpa uzoefu mpana katika uongozi na kumuwezesha kuzielewa changamoto halisi zinazowakabili walimu na sekta ya elimu kwa ujumla.

Kutokana na utendaji wake mzuri, mwaka 2006 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, kabla ya kuhamishiwa Wilaya ya Urambo.

Kote huko, alijipambanua kwa nidhamu, bidii na uwajibikaji wa hali ya juu, huku akiendeleza rekodi ya uongozi ulioweka masilahi ya wananchi mbele.

Mwaka 2010 aliamua kuingia kwenye siasa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM). Aligombea ubunge wa Jimbo la Ruangwa na akashinda kwa kishindo.

Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, alimteua kuwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ambapo alihusika moja kwa moja na halmashauri za wilaya hasa katika sekta ya elimu, afya na maendeleo ya jamii.

Mwaka 2015, Tanzania iliingia katika sura mpya ya uongozi chini ya Rais John Magufuli ambapo  alimteua Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu.

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilimuidhinisha kwa kura nyingi, na hapo akawa Waziri Mkuu wa 12 katika historia ya nchi.

Amemuoa Mary Majaliwa, mwalimu kitaaluma mwenye shahada ya uzamili katika elimu na wamebarikiwa watoto wanne.