Prime
Jaji Warioba ataja ‘dawa’ ya kuliponya Taifa
Muktasari:
- Mapendekezo ya Jaji Warioba yanakuja kipindi ambacho Tume ya uchunguzi wa matukio wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29 mwaka jana imetoa mapendekezo yake ya kulikwamua Taifa, ikiwemo kuanza mchakato wa maridhiano.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema kuziondoa dosari zilizosababisha migawanyiko ya wananchi na kutokea vurugu za Oktoba 29, 2025 ndiyo mbinu itakayoliwezesha Taifa kutoka katika changamoto iliyotokea.
Amezitaja dosari tatu zinazopaswa kufanyiwa kazi ili kuliondoa Taifa katika hali ya migawanyiko kuwa ni kuirudisha amani ya nchi, kufanya mageuzi ya mifumo ya uchaguzi na kupatikana kwa Katiba mpya.
Mapendekezo hayo ya Jaji Warioba yanakuja kipindi ambacho tume ya uchunguzi wa matukio wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka jana imetoa mapendekezo yake ya kulikwamua Taifa, ikiwemo kuanza mchakato wa maridhiano.
Hata hivyo, mambo matatu yaliyotajwa na Jaji Warioba ni miongoni mwa yaliyopendekezwa na tume hiyo, ikitaka yafanyiwe kazi, hasa Katiba mpya, ambayo imetakiwa kupatikana kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka 2029.
Pamoja na hayo, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) chenyewe kinaona mapendekezo ya tume hiyo hayawezi kuwa suluhu ya changamoto zilizopo, kikipendekeza kuundwe chombo huru kufanya uchunguzi wa kina.
Tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman ilifanya uchunguzi kwa siku 153 na kuwasilisha ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Aprili 23 mwaka huu.
Hata hivyo, Jaji Warioba ameonesha kushangazwa na uamuzi wa ripoti hiyo kutowekwa hadharani.
Jaji Warioba, aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo katika muhimili wa Mahakama, amesema hayo leo Jumatatu, Mei 11, 2026 katika mahojiano maalumu aliyoyafanya na kituo cha televisheni ya mtandaoni ya The Chanzo.
Tunatokaje
Nguli huyo wa sheria anaona kufikiwa kwa maridhiano kunahitaji kuanza na kulirudisha Taifa kwenye misingi yake ya watu kuamini katika usawa, haki, umoja, mshikamano na uzalendo ili kuipata amani.
“Kwa hiyo mambo yote yanayoingilia misingi hii ndiyo tuyaondoe,” amesema Jaji Warioba.
Lingine linalopaswa kufanywa kwa mujibu wa kiongozi huyo ni kuwarudishia wananchi mamlaka ya kuamua kiongozi wanayemtaka kupitia uchaguzi, akisisitiza mifumo ya uchaguzi irekebishwe.
“Kwa sasa hakuna muunganiko kati ya uongozi na wananchi, wananchi wanaona hawana haki ya kuchagua viongozi wanaowataka. Lazima madaraka ya mwananchi yalindwe ili viongozi wawe na uhalali,” amesema.
Amesisitiza lazima mabadiliko yaje, na muhimu yafanywe katika utaratibu wa kawaida, kinyume na hivyo wasioridhika wanaweza kutumia njia nyingine zitakazoleta matatizo.
Hoja hizo za Jaji Warioba zinaungwa mkono na mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Elias Mwakalinga, anayesema amani haiwezi kulindwa kwa nguvu bali kwa wananchi kujihisi wanatendewa haki.
“Ukiona wananchi wanapoteza imani kwa mifumo ya uchaguzi na taasisi za dola, kuna ufa unaotakiwa kuzibwa haraka. Amani ya kweli haiwezi kulindwa kwa nguvu pekee, inalindwa kwa wananchi kujisikia wanatendewa haki,” amesema.
Amesema ni muhimu kila linalofanyika lisitazamwe katika mawanda ya kisiasa pekee, bali lishirikishe wananchi wa kawaida ili kuondoa hisia za upande mmoja kunufaika.
Mtaalamu wa sheria, Rehema Mbise, anaona Katiba mpya sio turufu ya kuondokana na changamoto zilizopo, bali kunahitajika utekelezwaji wa dhati wa sheria zilizopo.
“Unaweza kuwa na Katiba bora, lakini kama taasisi hazina uwajibikaji na uamuzi hauzingatii haki, bado migogoro itaendelea. Suluhu ya kwanza ni kujenga utamaduni wa kuheshimu sheria,” amesema.
Ripoti kubaki kwa Rais
Akirejea kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan, Aprili 23 mwaka huu kwamba ripoti ya tume hiyo ni mali ya Mkuu wa Nchi na hakuna mwenye mamlaka ya kujimilikisha, Jaji Warioba amesema imemchanganya.
“Ilinichanganya kwa sababu nilitarajia tutapata tume imefanyaje kazi, imepata nini na inapendekeza nini,” amesema.
Amesema ni kweli kisheria Rais ana mamlaka ya kuunda tume na inapokamilisha kazi yake hukabidhi ripoti kwake, lakini kumekuwa na utamaduni kwamba kwa masuala muhimu ya kitaifa tume ikitoa taarifa huwekwa hadharani.
Ametoa mfano wa tume iliyowahi kuundwa na Rais Julius Nyerere kuhusu kurudisha mfumo wa siasa za vyama vingi, ripoti yake haikuishia kwa Mkuu wa Nchi, bali iliwekwa hadharani.
Mfano mwingine, amesema mwaka 1995, hayati Ali Hassan Mwinyi akiwa Rais aliunda tume kuchunguza kero, naye (Warioba) alikuwa mwenyekiti wake. Walifanya uchunguzi na kumkabidhi Rais ripoti ambayo akawaambia iwekwe hadharani.
“Nilitarajia taarifa ingetolewa hadharani pamoja na viambatanisho vyake. Sasa hii ya kusema kwamba haitoki hadharani, kuna masuala muhimu hayajafafanuliwa kwa kina,” amesema.
‘Tunachelewesha mambo’
Katika mahojiano hayo, Jaji Warioba ameonesha kutokubaliana na pendekezo la tume kuundwa kwa tume nyingine kufanya uchunguzi wa kijinai, akisema hilo linalenga kusahaulisha mambo.
“Kwa haya machache ninayofahamu kulikuwa na kuwajibika, na hiyo ingewaridhisha wananchi kwamba kuna hatua zimechukuliwa. Hii ya tume hizi ni kujaribu kufanya mambo yaje yasahaulike tuendelee hivi,” amesema.
Hata hivyo, kiongozi huyo amesema hana tatizo na uundwaji wala wajumbe wa tume hiyo, kwa kuwa anafahamu weledi wao na amewahi kufanya nao kazi.
“Niliwaona walivyokuwa wanafanya kazi na walitoa mambo ambayo pengine Serikali isingeyapenda, kwa hiyo hainipi matatizo. Tatizo langu ni kwamba waliyotoa tume hayakutoka hadharani,” amesema.
Kuhusu Katiba mpya
Jaji Warioba amesema kwa hali ilivyo, haoni kama pendekezo la tume kupata Katiba mpya mwaka 2028 litawezekana.
Hiyo inatokana na kile alichoeleza kwamba tatizo lililopo si kujua yanayohitajika ndani ya Katiba hiyo, bali kukosekana kwa utashi wa kisiasa.
Amesema Katiba mpya si kwamba unaandika kila kitu upya, bali inakuja pale kuna jambo la msingi linalohitaji mabadiliko ndani yake.
“Katika kipindi tulichopita, hivi hatujui matatizo yetu? Tulipokwenda kwa wananchi walikuwa na mambo yao, moja walitaka mgombea binafsi. Katika Katiba hii pendekezwa waliweka lakini kuna masharti,” amesema.
Amesema kukiwa na utashi wa kisiasa haitachukua muda Tanzania inaweza kuwa na Katiba mpya.
“Matatizo ninayoyaona ni kwamba vyama hivi vimekuwa hasimu kiasi kwamba hawazungumzi. Ukiona kiongozi wa CCM akizungumza na wa Chadema inaonekana kama usaliti,” amesema.
Warioba amesema kwa Taifa lilipofikia ni kama ubinadamu umekwisha, akidai baadhi ya watu wanaonekana kufurahia wanaposikia mwingine amefariki.
“Unaweza kuona kuna chuki na hasira katika hilo. Hii ni vyama vyote,” amesema.
Hofu ya maisha yake
Alipoulizwa iwapo anahofia maisha yake, Jaji Warioba amesema hajaona dalili kwamba maisha yake yako hatarini, ingawa kuna watu wengi wanaomshauri awe makini.
“Kuna wengine wanaoniambia kwamba, mzee labda ukae kimya tu, mambo unayosema yanaweza kukuletea matatizo kwa maisha yako,” amesema.
Amesisitiza hana wasiwasi kuhusu maisha yake wala hajihangaishi na jambo hilo.
Alipoulizwa kuhusu alivyoonekana kwenye picha na Rais Samia, amesema walikutana na akampa mawazo yake, naye akatoa yake, na hakikuwa kikao cha mazungumzo ya kufikia makubaliano.
“Ikitoka pale, yapo ambayo alinambia Rais niweze kuyachukulia, lakini nami ninatarajia baadhi ya mambo niliyomwambia labda atayazingatia au ataona yanafaa, na hiyo ni mambo ya kawaida,” amesema.
TLS
Katika hatua nyingine, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, amesema ripoti ya Tume ya Jaji Chande haiwezi kutumika kama suluhisho la mgogoro uliopo nchini, akisisitiza mchakato wa maridhiano lazima ujengwe katika ukweli, uwazi na uwajibikaji.
Amesema TLS imebaini upungufu mkubwa katika ripoti hiyo, ukiwamo wa kutokuwepo kwa uchunguzi wa kina kuhusu watu waliouawa, waliotekwa, waliopotea na kutotajwa kwa wahusika wa matukio hayo.
“Tunapozungumzia maridhiano lazima tuanze na ukweli, haki na uwajibikaji. Huwezi kusema tuanze upya wakati familia nyingi bado hazijui ndugu zao wako wapi,” amesema Mwabukusi.
Katika tathmini yake, Mwabukusi ametaja mambo saba waliyoyabaini katika taarifa ya tume, yakiwemo ukosefu wa uchunguzi wa kina kuhusu vifo na upotevu wa watu, kutotajwa kwa waliohusika na kukosekana kwa uwajibikaji.
Pia ametaja kuwepo kwa mkanganyiko wa takwimu za vifo na majeruhi, pamoja na kukosekana majibu kuhusu nani alitoa amri ya kutumia nguvu dhidi ya wananchi.
Katika maelezo yake, Mwabukusi ametaka kuundwa kwa chombo huru, shirikishi na kinachoaminika kitakachochunguza kwa upana ukweli matukio hayo na kutoa mapendekezo yatakayorejesha imani ya wananchi.
“Serikali inapaswa kukiri makosa na kuwawajibisha wote waliohusika na upotevu wa haki, kwa kuwa kukiri si udhaifu bali ni hatua ya uwajibikaji,” amesema..