Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pasua kichwa sura mbili za mwelekeo wa maridhiano

Muktasari:

  • Awali, akipokea ripoti ya Tume ya Jaji Chande, Rais Samia Suluhu Hassan alisema siku zote yeye ni muumini wa mariadhiano.

Dar es Salaam. Pendekezo la Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kuanzishwa kwa Tume ya Kitaifa ya Maridhiano na Mwafaka, limeonekana kama suluhisho la kuliunganisha tena Taifa.

Kwa sasa kumekuwa na mitazamo tofauti kutokana na kilichotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, ambayo imeliweka Taifa kwenye mtanziko.

Hata hivyo, swali linalogonga vichwa vya wengi ni maridhiano ya aina gani yatakayoivusha Tanzania kutoka mahali ilipo na kurejea kwenye asili yake ya maelewano, uhusiano mzuri na kusikilizana huku upendo, umoja na amani vikitawala kama ilivyozoeleka tangu kupata Uhuru.

Kutokana na hoja hiyo, baadhi wamekuwa wakiunga mkono kuhusu kuanzishwa Tume ya Mariadhiano kama ilivyopendekezwa na Tume ya Jaji Chande kuwa tiba ya kwenda kuliponya Taifa huku wengine wakionesha hofu wakitaka kwanza kufanyike mabadiliko mbalimbali kwenye mifumo kabla ya kuanzishwa kwa chombo hicho.

Wanaounga mkono kuanzishwa kwa mariadhiano wanaeleza kwamba, kwa sasa ndio suala muhimu zaidi ili kurudisha mshikamano, wakirejea mifano ya migogoro mbalimbali ya muda mrefu iliyotatuliwa kwa njia ya mazungumzo.

Kwa upande wa wanaopinga, wanasema licha ya kutamani kuiona tena Tanzania yenye mshikamano na inayozungumza lugha moja ya amani, lakini wanataka kwanza kuona viashiria ama mambo yaliyoligawa Taifa yanapatiwa ufumbuzi ndipo milango ya maridhiano ifunguke.

Hata hivyo, lipo kundi linaloona ni sawa kwenda kwenye maridhiano, lakini yazingatie mahitaji ya kila upande; na watakaoridhiana wakubali kuacha baadhi ya vitu na kuweka msimamo na makubaliano ya pamoja.

Akipokea ripoti ya Tume ya Jaji Chande, Rais Samia Suluhu Hassan alisema siku zote yeye ni muumini wa mariadhiano na kwamba, falsafa yake ya 4R inajieleza na amekuwa akiitumia siku zote kwenye uongozi wake.

Falsafa hiyo inayoakisi Maridhiano, Ustahamilivu, Mageuzi na Kujenga upya Taifa, imekuwa maarufu kutokana na kufanya mageuzi kwenye mifumo ya utoaji haki pamoja na kuruhusu shughuli za kisiasa kurejea upya baada ya kusitishwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Tano.


Wadau na mitazamo tofauti

Akizungumza leo Jumapili, Aprili 26, 2026, Mchambuzi wa masuala ya siasa, Maggid Mjengwa amesema yaliyotokea Oktoba 29, 2025 yameshatokea, yamewagusa na kuwaumiza Watanzania wengi.

Katika mazingira kama hayo, ameeleza watu wanasikitika lakini kila janga linapaswa kutoa somo na funzo. Tume ya uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29, jukumu lake lilikuwa ni kuonesha cha kujifunza.

Hata hivyo, amesema hadi yanatokea ya Oktoba 29, ni kwa sababu hakukuwa na mazungumzo ya kuaminiana, kiasi cha kusababisha kilichotokea.

“Pamoja na yote hayo, mwisho wa siku maisha lazima yasonge mbele. Siasa ni mazungumzo na majadiliano yasiyokoma, hii ndiyo tafsiri ya siasa,” amesema Mjengwa.

Amesisitiza maridhiano hayo yanalenga kutoa nafasi ya kujadiliana sio kusaka tiba tu. Ndani yake kunakuwa na diplomasia inayosababisha kupatikana mwafaka.

“Huwezi kukimbia maridhiano kwa sababu usipotaka maridhiano unataka nini na hicho unachotaka kitafanyikaje bila kuhusisha mazungumzo. Migogoro mingi duniani iliyodumu kwa muda mrefu ilipata mwafaka kwa njia ya mazungumzo, hivyo kuzungumza ndiyo njia sahihi.

“Katika yote yanayoendelea lazima kuzungumza na kama itashindikana kuzungumza wenyewe, lazima awepo mtu wa kutuzungumzisha,” amesema Mjengwa.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Nuhu Mruma amesema Tanzania imepita katika kipindi kigumu ambacho haikuwahi na uzoefu nacho,hivyo suala la kuridhiana ndio muhimu zaidi kwa sasa.

Amesema yote yaliyotokea kwa kiasi kikubwa yalichochewa na masuala ya kisiasa na sio mambo ya kijamii, maridhiano yajikite zaidi kwenye siasa ikiwa ni pamoja na kuwa na demokrasia ya kweli kwani, ndiko kwenye shida zaidi.

“Kuridhiana ni katika yale ambayo hakukuwa na mwafaka, katika maridhiano unakutanisha mawazo mawili kinzani na mwisho wa siku mnakubaliana jambo moja,” amesema.

Sheikh Mruma amesema maridhiano hayo ni muhimu yazingatie mahitaji ya kila upande na watakaoridhiana wakubali kutoa na kupeana.

“Yasije yakawa maridhiano ya shinikizo la upande mmoja tu. Muhimu mmoja akubali kupoteza hili na mwingine akubali kupoteza hili, ili kujenga mustakabali wa pamoja,” amesema.

Kwa mtazamo wake, amesema haoni kama wananchi wana tatizo zaidi, yanayoonekana yanatoka kwa viongozi wa kisiasa. Hivyo, muhimu viongozi wawe mstari wa mbele kuwafanya wananchi wafurahie mazuri ya nchi yao.

Naye Mshauri wa Rais katika Masuala ya Diplomasia, Lazaro Nyalandu, amesema mwitikio wa Serikali wakati wa vurugu unapaswa kueleweka katika muktadha wa kurejesha utulivu na kulinda maisha ya Watanzania.

Balozi Nyalandu ameongeza kuwa ripoti hiyo inatoa ufafanuzi juu ya asili ya matukio hayo na umuhimu wa umoja wa kitaifa katika hatua zijazo kama ambavyo Rais Samia amekuwa akionesha dhamira hiyo siku zote.

“Kama umemsikiliza Rais Samia kwenye hotuba yake utagundua alivyo na utayari wa kuwaletea Watanzania pamoja baada ya matukio yale ambayo mwenyewe (Rais Samia) yamemhuzunisha kwa sababu yamelitia doa Taifa letu. Ameahidi mambo mengi ikiwamo uwajibikaji kwa watakaobainika kuhusika hivyo, kwangu ni muelekeo mzuri na sahihi jambo la msingi ni kupewa muda ili aendelee kutekeleza kile alichokianzisha,” amesema Balozi Nyalandu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Conrad Masabo amesema ufanisi wa ripoti hiyo utategemea jinsi matarajio ya makundi mbalimbali yatakavyosimamiwa.

Ameonya kuwa, kuangazia visababishi vya haraka pekee bila kushughulikia mizizi ya kimuundo kama kucheleweshwa kwa mageuzi kunaweza kupunguza athari yake.

Pia, amependekeza kuwa taasisi zinazopendekezwa, kama baraza la wazee, zinapaswa kujumuisha uwakilishi mkubwa zaidi wa vijana kutokana na muundo wa demografia ya nchi.

Profesa Benson Bana amesisitiza kuwa amani, haki na uhuru lazima vitafutwe kwa pamoja, akieleza kuwa hakuna kati ya hivyo vitatu vinavyoweza kudumu peke yake.

Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Wazee, David Sendo amewataka viongozi kuwa na tahadhari katika matamshi yao ya hadhara wakati wa utekelezaji wa mapendekezo, akisema mawasiliano yenye uwajibikaji yatakuwa muhimu katika kulinda utulivu wa Taifa.


Nani wahusika kwenye maridhiano?

Mwenyekiti wa Jukwaa la Vyama 12, Abdul Mluya amesema wadau wanaopaswa kuwepo katika maridhiano ni viongozi wa dini, asasi za kiraia, vyama vya siasa na uwakilishi wa kada nyingine zote katika Taifa.

"Kama ambavyo ilivyotengeneza wajumbe wa kikosi kazi. Katiba imefafanua wazi jambo lolote linalohusu masilahi ya watu, Watanzania wanapaswa kuwachagua wawakilishi wao wenyewe pasipo kuingiliwa," amesema.

Amesema haiwezekani kwenda kwa mtu mmoja mmoja, mkutano wa wadau ndio utakaotengeneza chombo kitakachosimamia maridhiano hayo na muhimu kila mtu awe na imani na chombo hicho.

Mluya amesema chombo kitakachosimamia maridhiano kisiwe na mrengo wa utegemezi wa upande wowote wa kisiasa, kidini, kikabila na kikanda bali kibebe taswira ya kulibeba Taifa.

“Hatufikirii wala kupendekeza tuwe na aina ya maridhiano yatakayosimamiwa na watu kutoka nje ya Tanzania, kwa sababu tuna historia ya kupita kwenye mikwamo ya kisiasa na tumetoka salama," amesema.


Chadema yashika ‘shilingi’

Akizungumzia kuhusu maridhiano, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila amesema kwa upande wake anaamini hoja ya maridhiano inalenga kuisafisha mamlaka kwa Watanzania na jumuiya ya kimataifa.

“Chadema msimamo ni uleule kuwa laiti kama tungeamua kujadili maridhiano, kuna mambo yangeshafanyika. Kama wana nia njema uchunguzi kutoka nje una shida gani, wangeuruhusu tu,” amesema.

Amesema inachokihitaji Chadema ni kufahamu waliohusika kwenye matukio ya mauaji ya Oktoba 29 na hatua za kuwajibika.

Pia, amesisitiza kuhusu msimamo wa chama hicho kwa sasa ni kutaka mwenyekiti wao, Tundu Lissu aachiwe huru, kinyume na hivyo, taarifa za maridhiano ni kile alichokiita ulaghai.

Hata hivyo, amesema uamuzi wa Chadema kuingia kwenye maridhiano ni matokeo ya majadiliano ya vikao vya chama hicho.