Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Ilichobaini tume matukio ya Oktoba 29 hiki hapa

Muktasari:

  • Baada ya kusubiriwa kwa takriban miezi mitano, hatimaye ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 imewekwa hadharani leo.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Jaji mstaafu Mohammed Chande, amesema tume imebaini kuwa kilichotokea kabla na baada ya uchaguzi ni ghasia, siyo maandamano ya amani kama inavyodaiwa nje.

LIVE: Rais Samia akipokea ripoti ya tume ya Oktoba 29


“Tume imepata ushahidi usio na shaka kwamba matukio ya ghasia za Oktoba 29 yalipangwa, yaliratibiwa, yalifadhiliwa na kutekelezwa na watu waliopata mafunzo, waratibu walitumia mbinu mbalimbali, ikiwemo kuwatumia watu wasio na ufahamu wa kina na vijana waliokata tamaa,” amesema.
Jaji Chande amebainisha hayo leo, Alhamisi, Aprili 23, 2026, Ikulu, jijini Dar es Salaam, alipozungumza kabla ya kukabidhi ripoti kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Akiwasilisha ripoti ya tume hiyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan, wenyekiti wa Tume hiyo Jaji mstaafu Mohamed Chande, amesema baadhi ya picha na video hizo zilikuwa za kweli na zingine zilikuwa zimetengenezwa.

“Uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya picha zilizosambaa zilikuwa za kweli na zingine hazikuwa za kweli,” amesema Jaji Chande.

Katika maelezo yake, Jaji Chande amesema baadhi ya video zilizosambazwa zaidi katika mitandao ya kijamii ni zile zilizotengenezwa akitolea mfano picha iliyosambazwa zaidi ikionesha miili ya watu kwenye mifuko ya bluu.


Athari

Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, imebainisha kuwa ilifanya uchunguzi katika maeneo 202 yaliyoathirika zaidi, yakihusisha wilaya 21 kutoka mikoa 11 ya Tanzania Bara.

Ametaja maeneo yaliyoathirika zaidi ikiwemo Dar es Salaam, Mbeya, Songwe, Mwanza, Geita, Arusha, Iringa, Dodoma, Shinyanga, Ruvuma na Kimara.

“Uchunguzi ulihusisha maeneo 202 yaliyoathirika zaidi katika wilaya 21 na mikoa 11. Lengo lilikuwa kupata taswira halisi ya matukio na sababu zilizochangia uvunjifu wa amani,” amesema Jaji Chande.

Aidha, amesema tume hiyo ilitembelea pia Zanzibar na mkoa wa Kilimanjaro kama sampuli ya maeneo ambayo hayakukumbwa na ghasia, ili kujifunza mazingira yaliyosaidia kudumisha utulivu.


Matumaini

Mwenyekiti wa Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Jaji Mohamed Chande Othman amesema ripoti ya tume hiyo inalenga kusaidia Taifa kutibu majeraha, kuwajibika na kujifunza ili kusonga mbele.

“Tunaamini ripoti hii na mapendekezo yake yatabeba dhamira ya taifa ya kutibu majeraha, kuwajibika pale panapostahili na muhimu zaidi kujifunza na kusonga mbele,” amesema.


Mbinu

Jaji Chande, amesema uchunguzi umebaini kuwepo kwa mbinu 16 zilizotumiwa na wahusika wakuu na waratibu wa ghasia zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi huo.

Amesema baadhi ya mbinu hizo ni pamoja na kuweka vizuizi barabarani, kuchoma moto, matumizi ya pikipiki, pamoja na alama za kutambuana kati ya wahusika.

“Matukio haya yalikuwa na malengo ya kuzuia na kuvuruga uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025. Hii inadhihirishwa na uharibifu wa vituo vya kupigia kura, kufikisha ujumbe kwa Serikali, na baadhi ya matukio ya uporaji na wizi; pili, vijana kufikisha ujumbe kwa Serikali ili iwasikilize changamoto zao,” amesema.


Katiba

Jaji Chande amesema maandamano ya vurugu zilizotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 wahusika walikuwa na malengo makuu matatu.

Amesema makundi hayo yalivamia na kuharibu vifaa vya kupigia kura, kushambulia askari polisi waliokuwa wakilinda kwenye maeneo hayo.

Kwa mujibu wa Jaji Chande lengo lingine lilikuwa ni kufikisha ujumbe kwa Serikali kutokana na changamoto ya gharama za maisha, uwepo wa demokrasia na haki sawa kwa vyama vya siasa pamoja na madai ya Katiba mpya.

Amesema kwa muda mrefu kumekuwepo kilio cha madai ya Katiba mpya hivyo, vurugu hizo zililenga kufikisha kilio hicho kwa Serikali na mamlaka husika.

Kwa mujibu wa Jaji Chande amesema baadhi ya makundi yalikuwa na lengo la kuvamia huku akieleza kuwa, wafanyabiashara waliofika mbele ya Tume walilalamika kuibiwa mali kwenye maeneo yao.

Oktoba 29, 2025 Tanzania ilikumbwa na vurugu kwenye maeneo mbalimbali nchini na kusababisha vifo, uharibifu wa miundombinu na mali za umma na watu binafsi.


Vifo

Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, imesema kuwa vifo vilivyotokana na ghasia hizo ni 518 ambao wanaume 490 sawa na asilimia 94.6, wanawake 28 sawa na asilimia 5.4, ambapo katika vifo hivyo watoto walikuwa 21.

“Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na vifo vingi zaidi ikiwa na vifo 182 ikiuatiwa na Mwanza 90, Mbeya 80 na Arusha 53,” amesema Jaji Chande.


Majeruhi

Tume imesema watu 2,390 walijeruhiwa kwenye vurugu za Oktoba 29, 2025. Hadi kufikia mwezi Machi, 2026 uchunguzi wa Tume yake umebaini kuwepo majeruhi hao huku asilimia 95 wakiwa raia na asilimia tano ni maofisa wa Jeshi la Polisi.

"Inawezekana baadhi ya majeruhi hawamo katika idadi hiyo, kwa kupata huduma nje ya vituo (hospitali) na wengine kwenda nchi jirani hasa wale wa mikoa ya Mara na Songwe," amesema Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Chande.

Kwa mujibu wa Jaji Chande kati ya majeruhi hao, 219 walipata majeraha makubwa na 197 walipata majeraha yaliyotokana na risasi. Hata hivyo, amesema kuwa hakuna ushahidi wa mtu yoyote aliyefika mbele ya Tume kudai kuwa ameteswa.


Kauli za wanasiasa

Mwenyekiti wa Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Jaji Mohamed Chande, amesema baadhi ya kauli za No reforms, no election, Samia must go na Oktoba tunatiki ni baadhi ya vichocheo vya vurugu za Oktoba 29, 2025.

“Kauli za baadhi ya wanasiasa ambazo ziligeuka na kuwa kauli mbiu za baadhi ya waliokuwa wakifanya ghasia, No reforms, No election, Oktoba Tunatiki, Oktoba Tunatoka, Samia must go, wengine ni waliokatwa kwenye kugombea katika ngazi ya vyama, wakaona ghasia zilizokuwa zinafanywa zingewasaidia chini kwa chini,” amesema Jaji Chande.

Jaji Chande amesema baadhi ya kauli za No reforms, no election na Oktoba tunatiki ni baadhi ya vichocheo vya vurugu za Oktoba 29.

Oktoba 29, 2025 Tanzania ilikumbwa na vurugu kwenye maeneo mbalimbali nchini na kusababisha vifo, uharibifu wa miundombinu na mali za umma na watu binafsi.


Kaburi la halaiki

Jaji Chande amesema uchunguzi uliofanyika umebaini hakuna uthibitisho wa uwepo wa makaburi ya halaiki kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari vya kimataifa.

Akiwasilisha matokeo ya uchunguzi, Jaji Chande amesema uchunguzi wa kina umebaini madai hayo hayana ukweli.

Amesema tume ilitembelea na kukagua eneo la Makaburi ya Kondo, kufanya mahojiano na wasimamizi pamoja na kushirikisha wataalamu mbalimbali kufanya uchunguzi wa kisayansi, ikiwemo matumizi ya picha za satelaiti.

Amesema pamoja na hatua hizo, mazingira ya eneo hilo likiwa limezungukwa na makazi ya watu na kulindwa muda wote yalisaidia kufikia hitimisho kuwa hakuna ushahidi wa kuwepo makaburi ya halaiki.

“Hivyo kwa kuzingatia hali halisi ilivyo pamoja na taarifa za uchunguzi wa kisayansi, tume ilibaini madai hayo hayakuweza kuthibitika,” amesema.


Makambi

Uchunguzi wa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani umebaini kuwepo kwa dalili za kupanga na kuchochea ghasia za uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 zilianza kujitokeza miezi sita kabla ya siku ya kupiga kura hasa kupitia mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa Jaji Chande, Oktoba 17, 2025, TCRA iligundua kusambazwa kwa bango lenye maudhui ya kuchochea ghasia, likihamasisha maandamano yenye lengo la kuzuia na kuvunja uchaguzi mkuu.

Mbali na hilo, uchunguzi ulibaini mijadala mitandaoni iliyokuwa ikiendelea kuhusu mikakati ya kutekeleza ghasia siku ya uchaguzi.

“Majadiliano hayo yalionesha kuwa siku ya uchaguzi baadhi ya watu walipanga kuharibu mifumo ya umeme ili kuiingiza nchi gizani, kuchoma moto vituo vya mafuta pamoja na vituo vya kupigia kura kwa lengo la kuvuruga uchaguzi mkuu. Kwa mujibu wa uchunguzi huo, kulikuwa na vijana wasiopungua 500 waliokuwa wakihifadhiwa katika majengo, misitu na makambi mbalimbali nchini kwa takribani siku 28, wakipewa mafunzo maalumu kwa ajili ya kutekeleza ghasia siku ya uchaguzi,” amesema Jaji Chande.