Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hivi hapa vyanzo, vichocheo vurugu za Oktoba 29

Muktasari:

  • Miongoni mwa vyanzo hivyo, amesema ni masuala ya kisiasa yanayojumuisha madai ya Katiba mpya, demokrasia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, malalamiko ndani ya vyama vya siasa, madai ya maboresho ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na mfumo mzima wa uchaguzi.

Dar es Salaam. Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025, imetaja vyanzo vitano na vichocheo vinane vya matukio hayo, zikiwamo kauli za wanasiasa, matukio ya utekaji na ushawishi wa wagombea waliokatwa kwenye vyama vyao.

Tume hiyo iliundwa na Rais, Samia Suluhu Hassan Novemba 18, 2025, baada ya kutokea vurugu siku ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29 na kusababisha vifo, majeruh na uharibifu wa mali.

Taarifa ya vyanzo na vichocheo vya ghasia hizo, imetolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mohamed Chande Othman, alipokuwa akiwasilisha ripoti hiyo kwa Rais, Samia.

Chande amesema tume ilibaini kuwa vurugu hizo ziliratibiwa, kupangwa na kuwatumia watu wasio na uelewa wa kutosha kufika maeneo mbalimbali kuzunguka vyuoni, sokoni na maeneo mengine kuandikisha watu na kuwashawishi kushiriki maandamano hayo.

“kijana mmoja wa Usa River Arusha, alisema ameshawishiwa kwa kupewa Sh50, 000 ili ashiriki maandamano, akiahidiwa angepewa Sh5 miliano akishiriki maandamano,” amesema Jaji Chande huku akiainisha mbinu mbalimbali zilizotumiwa na waandamanaji hao.


Vyanzo vikuu

Akibainisha vyanzo vya matukio hayo wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu huo, Jaji Chande amesema uchunguzi umebaini ghasia hizo zilitokana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwepo katika jamii kwa muda mrefu bila kutatuliwa.

Miongoni mwa vyanzo hivyo, amesema ni masuala ya kisiasa yanayojumuisha madai ya Katiba mpya, demokrasia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, malalamiko ndani ya vyama vya siasa, madai ya maboresho ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na mfumo mzima wa uchaguzi.

Chanzo kingine, amesema ni masuala ya kiuchumi yanayojumuisha ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira na kukosekana kwa usawa katika fursa za ajira na za kiuchumi, mazingira ya biashara na uwekezaji yasiyo rafiki, utitiri wa kodi na tozo na mfumo usio rafiki wa utozaji na ukusanyaji.

“Masuala ya kijamii yanayojumuisha mmomonyoko wa maadili na kushuka kwa uzalendo, kutopatiwa ufumbuzi na majibu stahiki kwa kero katika jamii kama vile rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na madai ya utekaji na kupotea kwa watu,” amesema.

Katika taarifa yake hiyo, Jaji Chande amerejea takwimu za Jeshi la Polisi za kati ya mwaka 2023 hadi 2025 zinazoeleza watu 758 walipotea, kutekwa au kujiteka.

Amesema kati ya hao, watu 513 walipatikana na mashauri manane yalifunguliwa na upelelezi unaendelea.

“Hivyo, katika jumla ya watu 758 waliopotea, kutekwa au kujiteka kwa sababu mbalimbali, 245 hawajapatikana. Takwimu hizo zinaakisi malalamiko ya wananchi kuhusu masuala ya utekaji na kupotea kwa watu,” amesema.

Katika matukio hayo, amesema polisi ilieleza sababu za kupotea au kutekwa kuwa ni masuala ya kimapenzi (113), imani za kishirikina (87), waliotekwa na wahalifu kwa lengo la kujipatia kipato au mali (97) na waliojihusisha na vitendo vya kihalifu kwa chuki na kulipiza visasi (47).

Wengine, amesema ni waliojiteka wao wenyewe kutokana na sababu mbalimbali za kudaiwa na kukwepa mkono wa sheria (56), walioondoka bila taarifa (74) na usafirishaji haramu wa binadamu (39).

Chanzo kingine, amesema ni utendaji usioridhisha wa baadhi ya watendaji na watumishi wa umma, hususan ngazi za chini, ikiwa ni pamoja na kutosikiliza au kutatua kero za wananchi kwa wakati na utekelezaji hafifu wa mapendekezo ya Tume zinazoundwa.

“Masuala yanayohusu uhusiano wa kimataifa katika dunia ya leo na ijayo, ambapo mataifa mengi yanatanguliza mbele masilahi yao kama msingi wa mahusiano na kujaribu mbinu na mikakati mbalimbali ya kujiweka katika nafasi nzuri kuendeleza masilahi yao katika nchi nyingine, hasa zinazoendelea na zenye raslimali nyingi,” amesema.


Vichocheo

Kwa upande wa vichocheo, Jaji Chande amesema ushahidi na taarifa umeonyesha baadhi ya wanasiasa na wanaharakati walitumia changamoto za wananchi zinazotokana na vyanzo mbalimbali vilivyobainishwa kama fursa ya kuwashawishi kushiriki katika ghasia kwa kutumia kaulimbiu na matamko mbalimbali.

“Tathimini ya tume imebaini kuwa, vilikuwepo vichocheo mahsusi vilivyoamsha ari ya kufanya ghasia wakati na baada ya uchaguzi mkuu. Vichocheo hivyo vinaweza kuwekwa katika makundi matatu,” amesema na kuyataja makundi hayo.

La kwanza, amesema linahusu mitandao ya kijamii ambayo kwa mujibu wa mashahidi, ilitumika kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu kwa kiwango kikubwa kuliko ilivyowahi kutokea nchini.

Aidha, amesema waliibuka watu waliokuwa wakibuni mada kwenye mitandao, zikiwamo za kuhamasisha wananchi kutoshiriki uchaguzi mkuu na kuhakikisha haufanyiki.

Amesema mitandao hiyo pia ilitumika kuandaa majukwaa ya majadiliano na kupanga mbinu na kuwaelekeza waliokubali kushiriki vurugu za kuzuia uchaguzi mkuu na namna ya kufanikisha lengo hilo.

Amesema kuanzia Aprili hadi Oktoba 2025, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilikuwa ikiwasilisha taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama, zikionzesha kuwepo kwa viashiria vya ghasia vinavyolenga kuzuia na kuvuruga uchaguzi.

Kwa mujibu wa Jaji Chande, Oktoba 17, 2025, TCRA iligundua kusambazwa kwa bango lenye maudhui ya kuchochea ghasia, likihamasisha maandamano yenye lengo la kuzuia na kuvunja uchaguzi mkuu.

Mbali na hilo, uchunguzi ulibaini mijadala mitandaoni iliyokuwa ikiendelea kuhusu mikakati ya kutekeleza ghasia siku ya uchaguzi.

“Majadiliano hayo yalionyesha kuwa siku ya uchaguzi baadhi ya watu walipanga kuharibu mifumo ya umeme ili kuiingiza nchi gizani, kuchoma moto vituo vya mafuta pamoja na vituo vya kupigia kura kwa lengo la kuvuruga uchaguzi mkuu,” amesema.

Tume hiyo imeeleza kuwa viashiria hivyo vya mtandaoni vilikwenda sambamba na ushahidi wa mashahidi mbele ya tume, ambao walieleza kuwepo kwa maandalizi ya vitendo vya ghasia nje ya mitandao.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, kulikuwa na vijana wasiopungua 500 waliokuwa wakihifadhiwa katika majengo, misitu na makambi mbalimbali nchini kwa takribani siku 28, wakipewa mafunzo maalumu kwa ajili ya kutekeleza ghasia siku ya uchaguzi.

Jaji Chande amesema tume ilifanikiwa kubaini moja ya nyumba iliyotumika kwa shughuli hizo jijini Dar es Salaam, ikiwa umbali wa takribani mita 10 kutoka kituo cha polisi, jambo linaloibua maswali kuhusu ufuatiliaji na udhibiti wa shughuli hizo.


Walipewa simu kupiga picha

Katika maelezo yake, Jaji Chande amesema wapo pia mashahidi walioshiriki kufanya ghasia waliokwenda mbele ya tume na kueleza kuwa baadhi yao walipewa simu maalumu za mkononi.

Amesema simu hizo walitakiwa kuzitumia kupiga picha na video za matukio ya majeruhi na vifo au kupiga picha jirani na magari ya JWTZ, na picha za maeneo ambayo wafanya ghasia walikuwa wamefanikiwa kufanya uharibifu.

“Picha na video zote hizo walizirusha moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii ili kuibua hasira za wananchi na kuwahamasisha nao wajitokeze kufanya ghasia kwa vile waliaminishwa kuwa JWTZ iko pamoja nao,” amesema.


No Reform no election, Oktoba tunatiki

Kundi la pili la vichocheo, amesema ni kauli za baadhi ya wanasiasa zilizogeuka kuwa kaulimbiu za waliokuwa wanafanya ghasia.

Amezitaja kauli hizo ni No Reforms No Election, Oktoba Tunatiki, Oktoba Tunatoka, Tumedhamiria uchaguzi hautafanyika, Samia Must Go, Tunataka kuikomboa nchi yetu na hakuna uchaguzi chini ya Serikali hii.

Jaji Chande, amezitaja kauli nyingine ni tutahakikisha nchi haisimami mpaka Serikali iondoke, hakutakuwa na uchaguzi bila mabadiliko ya mfumo na Serikali hii imepoteza uhalali wa kuongoza nchi.

Pia, ametaja ni lazima shinikizo la wananchi liongezeke hadi Serikali iondoke na mchakato wa kuwapata wagombea umekiuka taratibu, wagombea si halali, mchakato urudiwe.

Kundi la tatu lililotajwa kuwa kichocheo kwa mujibu wa ripoti hiyo ni baadhi ya waliokusudia kugombea viti vya udiwani na ubunge na majina yao kukatwa kwenye ngazi za juu za vyama vyao.

“Wakaona kuwa ghasia zilizokuwa zinafanywa zinawasaidia kudai mabadiliko ya mfumo wa kupata wagombea ndani ya vyama vyao na wakashiriki chinichini kuwahamasisha wafuasi wao kushiriki ghasia,” amesema.