Tume yagusa maridhiano, wachambuzi watia neno
Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman akisoma Muhtasari wa Ripoti ya Tume hiyo, Ikulu jijini Dar es Salaam, Aprili 23, 2026.
Dar es Salaam. Wakati Tume ya Kuchunguza Matukio ya Oktoba 29 ikipendekeza maridhiano na mwafaka wa kitaifa kuliponya Taifa, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamesema ni hatua muhimu, lakini imeacha maswali.
Wamesema maswali hayo yamejikita kwenye matukio ya utekaji wakihoji, upi mustakabali wake, kwa kuwa bado vitendo hivyo vinaendelea na je nani aliyefadhili vijana wanaodaiwa walifanya vurugu na kulilipwa fedha.
Pia, wamehoji ni upi umadhubuti wa vyombo vya ulinzi na usalama kushindwa kubaini mafunzo hayo yaliyotekelezwa kwa dhamira ya kufanya vurugu wakati wa uchaguzi.
Hata hivyo, katika eneo hilo Rais Samia Suluhu Hassan amesema: “Tumepokea mapendekezo yote yaliyowasilishwa na tutaanza kuyafanyia kazi mara moja, katika hatua hii, nitoe wito kwa Watanzania wenzangu tuungane kurejesha Taifa letu katika misingi yake na katika kuakisi mapendekezo ya tume, Serikali itachukua hatua za haraka.”
Rais Samia amesema suala la maridhiano ni moja ya ahadi zake alizotoa katika siku 100 atakapoingia madarakani na limechelewesha utekelezaji wake kutokana na ghasia za Oktoba 29.
Akiwasilisha ripoti hiyo leo Alhamisi Aprili 23, 2026 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa tume, Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman amesema maridhiano yanapaswa kuwa mtambuka kwenye maeneo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa kutathmini zaidi ukweli na kuponya majeraha,
Pia, kutafuta suluhisho na muafaka wa kisiasa na kukubaliana juu ya misingi, mambo yagusayo Katiba mpya na kurejesha umoja na mshikamano wa Taifa.
“Suala la maridhiano mheshimiwa Rais halikuanzishwa na ghasia, ilianzishwa kwa maoni ya wengi ulipoingia madarakani ukiwa na falsafa ya 4R (Ustahimilivu, Maridhiano, Mabadiliko na Kujenga upya) kwa hiyo sio ghasia zimeleta maridhiano ilikuwepo,” amesema.
Mbali na eneo hilo, Jaji Chande amesema kwa kuzingatia nafasi ya taasisi za dini kwa kujenga tunu na utangamano kwenye jamii, upo umuhimu wa kufanyika majadiliano kama sehemu ya maridhiano ya kijamii.
Jaji Chande amedokeza kuwa, majadiliano, maridhiano na mwafaka vitaimarisha uelewa miongoni mwao na mipaka kati ya dini na siasa wakati wa utekelezaji wa majukumu na kuepusha migongano.
Jambo lingine, Jaji Chande ametaja maridhiano yatakayofanyika ngazi ya kitaifa, yatashuka hadi Serikali za mitaa kwa kutumia mifumo ya utawala kwa wilaya, tarafa, kata hadi vijiji.
“Ili kuhakikisha mchakato wa maridhiano na mwafaka wa kitaifa unafanikiwa na kusaidia kukwamua mikwamo iliyojitokeza ni muhimu kuwa na Baraza la Ushauri la Wazee ili wazee wote washauri kutafuta changamoto na mivutano kwenye jamii na mambo mengine ya kitaifa,” amesema.
Akitolea maoni ripoti hiyo, mchambuzi wa masuala ya kijamii, Oscar Mkude amesema hakuna asiyetaka maridhiano, lakini tume hiyo haijatoa njia ya kuendelea.
Amesema pamoja na mapendekezo mazuri ya tume hiyo, bado kunaibuka maswali juu ya tume kueleza kuwa walikuwepo watu waliofadhiliwa kutekeleza vurugu wakati wa uchaguzi.
Swali alilosema Mkude tume ingejibu ni kina nani wamefadhili mafunzo hayo, ni wapi Jeshi la Polisi lilikuwepo na je, intelijensia ya polisi nayo haikuwa ikifanya kazi.
“Watanzania wanajua nini kilitokea; kwa nini yametokea, bado ni swali. Tume ingesema zaidi yaliyotokea kama kulikuwa na mafunzo wangesema nani alifadhili,”amesema.
Pia, amesema tume inataja matukio ya utekaji lakini hadi sasa bado kuna watu wamepoteza wapendwa wao, wanalia na maumivu ya muda mrefu, hivyo maridhiano yanafanyika wakati wa maumivu.
Hata hivyo, Jaji Chande katika hilo na mengine yanayohusu jinai, amesema kwa mujibu wa Katiba anayetuhumiwa lazima apewe fursa ya kujitetea, kwa mantiki hiyo wasingeweza kusema kuwa wanaotuhumiwa.
Mchambuzi wa Masuala ya kisiasa, Noel Shao amesema suala la maridhiano ni muhimu kushirikisha makundi yote kwenye jamii, lakini Serikali ni lazima iwajibike kwa yaliyotokea.
“Lazima Serikali iwajibike, mambo yaliyotokea yafanyiwe kazi ili yasijirudie, kwa kuwa yaliharibu sifa ya utawala uliopo na nchi kwa jumla,”amesema.