Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia ateua wawili yumo Dk Jingu

Muktasari:

  • Mwaka 2018, kabla ya Dk Jingu kuteuliwa kwa mara ya kwanza na hayati Rais John Magufuli, alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi wawili wakuu serikalini, akimteua Dk John Jingu kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.

Hayo yamebainishwa leo Juni 12, 2026 kupitia taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, kupitia Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka.

Dk Jingu anachukua nafasi ya Profesa Elisante Gabriel ambaye amestaafu utumishi wa umma.

Awali, kabla ya uteuzi huo, Dk Jingu alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria alikohamishiwa akitokea Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, ambapo pia alikuwa Katibu Mkuu.

Pia, Dk Jingu amewahi kuhudumu chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kama Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, ambapo nafasi hiyo aliteuliwa na hayati Rais Dk John Magufuli kwa mara ya kwanza mwaka 2018.

Wakati huo, Rais Magufuli alimteua Dk Jingu kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto), ambapo sasa wizara hiyo imegawanywa.

Wizara ya kwanza iliyotokana na wizara hiyo ni Wizara ya Afya, na ya pili ni Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, na kote Dk Jingu amehudumu kwa nyakati tofauti kama Katibu Mkuu.

Kabla ya uteuzi wa kushika nafasi ya ukatibu mkuu katika wizara hizo zote, Dk Jingu alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo uteuzi wake wa mara ya kwanza alichukua nafasi ya Sihaba Nkinga ambaye alitenguliwa katika nafasi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya.

Katika uteuzi wa leo Juni 12, 2026, Rais Samia pia amemteua Francis Mossongo kuwa Karani wa Baraza la Mawaziri.