Itutu amdondosha Doyo uenyekiti ADC

Mwenyekiti mpya wa chama cha ADC, Shabani Itutu akizungumza baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi hiyo katika mkutano mkuu wa nne uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Juni 29, 2024.

Muktasari:

  • Kati ya jumla ya kura zilizopigwa 192 Itutu amepata kura 121 dhidi ya Doyo aliyepata 70, huku moja ikiharibika.

Dar es Salaam. Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), kimepata viongozi wapya wa kitaifa, huku aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Shabani Itutu akiibuka na ushindi  kwa nafasi ya Mwenyekiti Taifa.

Itutu amemshinda Doyo Hassan aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.

Uchaguzi huo wa nne wa ADC umefanyika leo Jumamosi Juni 29, 2024 katika ukumbi wa Lamada jijini Dar es Salaam.

Umefanyika baada ya viongozi wa awali kumaliza muda wao wa kipindi cha miaka 10 kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti Hamad Rashid Mohamed.

Akitangaza matokeo, msimamizi wa uchaguzi huo, Mwalimu Azizi amesema jumla ya kura zilizopigwa ni 192 na kati ya hizo, Itutu amepata kura 121 dhidi ya Doyo aliyepata 70, huku moja ikiharibika.

Kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti –Zanzibar,  Azizi amesema kati ya wagombea wa nafasi hiyo, Fatuma Salehe amepata kura 120 dhidi ya mpinzani wake Shara Amran aliyepata kura 49, huku nne zikiharibika.

Nafasi ya Makamu Mwenyekiti -Bara, Hassan Mvungi amepata kura 135 dhidi ya Scola Kahana aliyepata kura 35. Kura tatu zimeharibika.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Itutu ameahidi kutoa ushirikiano kwa mgombea aliyekuwa akishindana naye, akiwashukuru wapigakura kwa ushirikiano waliouonyesha.

Amesema Doyo ni mwanachama wa siku nyingi waliyeanza naye ndani ya chama hicho, hivyo wataenda pamoja na kufanya naye kazi bila kujali chochote.

“Chama hiki sasa ni kikubwa kama mnavyoona mkutano huu ni wa kipekee, hata msajili amekiona,” amesema Itutu.

Awali, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohamed Ali Ahmed amekipongeza chama hicho kwa kuweka utaratibu wa ukomo wa uongozi.

Amesema chama hicho ni kichanga lakini kimezidi kukua kikiwa na wanasiasa wakongwe na wabobezi.

 "Niwapongeze ADC ni kimojawapo kati ya vyama vichanga lakini kimeweka utaratibu mzuri wa kupokezana vijiti," amesema.

Amebainisha kuwa vipo baadhi ya vyama vya siasa (bila kuvitaja) ukiviangalia, unaona viongozi wake hawataki kutoka na wengine wakijaribu kuingia.

Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Hamad Rashid awali aliwataka watakaochanguliwa kutokubali kuuza utu wao, kwa kuwa watakibomoa chama endapo wataingia kwenye rushwa.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa kwanza wa ADC, Said Miraj Abdallah amesema sifa ya kiongozi mzuri ni yule anayefikiri kwa ajili ya anaowaongoza kwa kutumia akili kwa masilahi ya taasisi.