Prime
Hekaheka miaka mitano ya ubunge wa Mdee wenzake 18

Muktasari:
- Kilichotokea bungeni kwa kina Mdee na wenzake 18 kinafungua fursa ya kutafakari kuhusu umuhimu wa uwajibikaji wa wawakilishi kwa wananchi zaidi ya utii kwa vyama.
Dodoma. Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaelekea ukingoni, likitarajiwa kuvunjwa Juni, 2025. Kila mbunge ana yake aliyoyapitia bungeni.
Kwa wabunge wa viti maalumu 19 waliokuwa wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanahitimisha uhai wa Bunge wakiacha historia ya aina yake.
Mwaka 2020, baada ya uchaguzi mkuu, Chadema kilipinga matokeo ya uchaguzi na kutangaza kutoshiriki katika mchakato wowote wa kisiasa ndani ya mfumo wa Bunge.
Hata hivyo, wanachama wake walioteuliwa kupitia orodha ya viti maalumu, ikielezwa ni pasipo kuwa na ridhaa ya uongozi wa juu wa chama hicho walikwenda bungeni ambako waliapishwa.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, vyama viwili kati ya 20 vilivyoshiriki ndivyo vilipata sifa ya kupata wabunge wa viti maalumu ambavyo ni CCM na Chadema. CCM ilipata viti 94 na Chadema viti 19 kati ya 113.
Ilikuwa Novemba 24, 2020 Spika wa wakati huo, Job Ndugai aliwaapisha hadharani, nje ya ukumbi wa Bunge wabunge hao 19 wa viti maalumu, licha ya kuwapo mzozo kati yao na chama chao.

Waliapishwa nje ya ukumbi wa Bunge kwa kuwa kipindi hicho kilikuwa cha ugonjwa wa Uviko 19.
Ndugai aliwaapisha ikiwa ni baada ya siku 14 kupita tangu wabunge wengine waapishwe ndani ya ukumbi wa Bunge.
“Nitawalinda kwa namna yoyote ile, fanyeni kazi zenu za kibunge na kuwatumikia Watanzania mimi nipo pamoja nanyi msijali, ninyi ni wabunge kama walivyo wengine,” ilikuwa kauli ya Ndugai alipowapisha.
Mzozo kuhusu nafasi za wabunge hao ulisababisha wavuliwe uanachama wa Chadema na kesi kufunguliwa mahakamani.
Wabunge hao 19 kabla ya kuenguliwa Chadema walikuwa na vyeo katika Baraza la Wanawake (Bawacha), Baraza la Vijana (Bavicha) na wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho.
Kwa wakati huo, Halima Mdee alikuwa Mwenyekiti wa Bawacha, Grace Tendega (Katibu Mkuu wa Bawacha), Nustrat Hanje (Katibu Mkuu wa Bavicha), Esther Matiko, Cecilia Pareso, Ester Bulaya na Agnesta Lambert.
Wengine ni Jesca Kishoa (Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha -Bara), Hawa Mwaifunga (Makamu Mwenyekiti wa Bawacha- Bara) na Tunza Malapo.
Pia Asia Mohammed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.
Mzozo watikisa
Baada ya kuapishwa, Chadema kilisema hakitambui uwakilishi wao kwa sababu hautokani na uamuzi wa ndani ya chama, jambo ambalo limevunja katiba.
Dk Wilson Mahera, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wakati huo, sasa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), alisema alipata orodha hiyo kutoka kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika.
Dk Mahera ambaye sasa ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, alisema Novemba 19, 2020, Mnyika alimuandikia orodha ya majina ya wanachama 19 waliopendekezwa kuwa wabunge wa viti maalumu na Tume ilitumia barua hiyo kuwateua.
Kutokana na mzozo huo, Chadema kiliandika barua kadhaa kwenda kwa Spika Ndugai kikieleza kutowatambua wabunge hao.
Novemba 27, 2020, Kamati Kuu ya Chadema chini ya uenyekiti wa Freeman Mbowe ilikutana jijini Dar es Salaam na kufikia uamuzi wa kuwavua uanachama wabunge hao kwa kosa la kwenda kuapishwa bila idhini ya chama hicho.
Mei 3, mwaka 2021, Ndugai aliwataka wabunge hao kuchapakazi kwa kuwa wako katika mikono salama, akionya vyama viache kuwanyanyasa wanawake.
“Makatibu wajifunze kuandika barua nzuri kwangu, huwezi kuniandikia kikaratasi hivi halafu unataka niwafukuze wabunge 19, hiyo siyo kazi yangu hata kidogo, ninyi wabunge chapeni kazi kwani mko katika mikono salama,” alisema Ndugai.
Alisema wabunge hao hawakuwa wamesikilizwa na Baraza Kuu la Chadema, hivyo hawezi kuwaondoa watu ambao hawajapata fursa ya kujitetea.
Harakati za kisheria
Mei 7, 2022, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema wabunge hao waliandikiwa barua za mwaliko wa kushiriki kikao cha Baraza Kuu baada ya kukata rufaa kwenye baraza hilo.
Baraza hilo liliitishwa Mei 11, 2022 kusikiliza rufaa za wabunge hao za kupinga kufukuzwa uanachama na Kamati Kuu. Baraza Kuu lilibariki uamuzi ya Kamati Kuu wa kuwafukuza uanachama.
Mnyika alisema baada ya uamuzi huo alimuandikia barua Spika wa Bunge kuhusu uamuzi huo.
Wabunge hao waliendelea kutekeleza wajibu wao bungeni, Mdee akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Kaboyoka akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Mei 16, 2022, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alilieleza Bunge anasubiri uamuzi wa mahakama kuhusu suala la kufukuzwa uanachama wabunge hao.
Dk Tulia alisema wabunge hao walifungua kesi Mahakama Kuu kupinga mwenendo wa kuvuliwa uanachama na Kamati Kuu na baadaye Baraza Kuu.
Alikiri kupokea barua kuhusu wabunge hao kufukuzwa uanachana na nyingine ya waliofukuzwa kwenda mahakamani.
Desemba 14, 2023 Mahakama Kuu ilitengua uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema lililoidhinisha uamuzi wa Kamati Kuu wa kuwavua uanachama wabunge hao.
Pia iliamuru Chadema kuzingatia haki za asili wakati ikishughulikia rufaa za kina Mdee.
Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Cyprian Mkeha aliyesikiliza kesi iliyofunguliwa Mahakama Kuu Masjala Kuu na kina Mdee wakipinga kufukuzwa uanachama kwa utaratibu wa mapitio ya Mahakama.
Ushawishi kisiasa
Licha ya kusimamia masuala muhimu ya kitaifa, wabunge hawa walikumbana na ukosoaji kutoka kwa uongozi wa chama chao wakichukuliwa kama vile waasi wa kisiasa.
Hata hivyo, walishiriki kikamilifu mijadala bungeni wakizungumzia masuala ya kijamii, hususan haki za wanawake, afya ya uzazi, elimu na uwajibikaji wa Serikali kwa wananchi.

Kwa mfano, Mdee, mbunge wa zamani wa Kawe katika mijadala aliibua hoja kuhusu masuala ya utawala bora na haki za wanawake. Kwa upande wake, Rwamlaza akizungumzia uwajibikaji wa watendaji wa Serikali hasa katika sekta za afya na maji.
Matiko alizungumzia masuala ya afya na ustawi wa jamii, huku Tendega akichangia hoja kuhusu elimu na uwezeshaji wa vijana.
Wabunge hawa waliendelea kuonyesha uwezo wa kujenga hoja bungeni kutetea masilahi ya wananchi.
Mdee na wenzake 18 katika Bunge la 12 wameacha alama katika historia ya siasa za Tanzania.
Harakati zao ndani ya Bunge zimeibua mjadala mpana kuhusu ushuru wa wabunge, mamlaka ya vyama vya siasa juu ya wawakilishi wao na nafasi ya wanawake katika uongozi.
Mbali ya mzozo wa wabunge hawa na chama chao kuonekana kuleta mgawanyiko, lakini ulifungua fursa ya kutafakari kuhusu umuhimu wa uwajibikaji wa wawakilishi kwa wananchi zaidi ya utii kwa vyama.