Heche: Kifo cha viwanda nchini ndiyo chanzo ukosefu wa ajira

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche akihutubia mkutano wa hadhara mjini Dodoma
Muktasari:
- Kiongozi huyo amekosoa mfumo wa ubinafsishaji kwa kila kitu hata na ambavyo haviwezekani akisema siyo sawa.
Dodoma. Makamu Mwenyekiti wa Chadema- Bara John Heche ametaja kufa kwa viwanda kuwa sababu kubwa vijana kukosa ajira.
Heche amesema viwanda ndiyo sehemu pekee ambayo watu waliosoma na ambao hawajasoma wanaweza kupata ajira bila kubaguana.
Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Juni 8,2025 wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa chama hicho katika Uwanja wa Mtekelezo jijini Dodoma.

Viongozi wa Chadema wapo Kanda ya kati katika kampeni yao ya No reforms, No election na leo walianzia katika wilaya za Kongwa, Mpwapwa, Kondoa na Chemba kabla ya kuungana uwanja wa Mtekelezo jijini humo.
"Watu wameua viwanda vyote halafu kesho wanasema eti tunataka ajira, haiwezekani hizo ajira zitatoka wapi,"amehoji Heche.
Amesema ajira za viwanda huwa chukua watu wenye elimu kwa ajili ya utaalamu lakini wengine wanachukuliwa hadi wabeba mizigo ambao hawahitaji kuwa na elimu.
Akizungumzia masuala ya uchaguzi, amesema tatizo linalowafanya watu wengi kushindwa kufanya mabadiliko ni uelewa mdogo kuhusu umuhimu wa uchaguzi wengi wakiamini hawahusiki.

Amesema lengo kuu la serikali ni ustawi wa wananchi na maendeleo hivyo hakuna sababu ya kuogopa kufanya mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi ili wapatikane wenye kukubalika.
"Mwalimu Nyerere alisema tunahitaji mambo manne, ambayo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora, tayari tuna watu na ardhi ipo lakini tunakosa nini..,"amehoji Heche na watu wakajibu uongozi bora.
Amewaambia wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo kuwa kitendo cha kuagiza kila kitu nje ya nchi hata vilivyopo kama viberiti na njiti za meno katika nchi yenye misitu ni jambo la aibu.
Katika hatua nyingine kiongozi huyo ametaka wananchi kujiandaa kwa mabadiliko na hata Chadema kikiingia madarakani kama hakitafanya vizuri pia kiondolewe.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama hicho John Mnyika amesema alichokiita mbinu za kilaghai za watawala ambao waliwaamini hadi vyama vingine kwenda kusaini kanuni za uchaguzi.

Mnyika amesema asingekuwa msaliti kwa namna yoyote kwa kuwa alijua kinachoendelea siyo mapenzi ya wananchi.
Kuhusu mikutano amesema wataendelea kufanya hata kama kiongozi wao (Tundu Lisu) ataendelea kuwa gerezani, kwani wana kikosi kipana ambacho hakiwezi kuyumbishwa kila akipumzishwa mtu ataingia mwingine.