Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Askofu Shoo: Watawala heshimuni wito wa viongozi wa dini kuhusu haki, usalama wa raia

Muktasari:

  • Chuo Kikuu cha Midland kilichopo Nebraska nchini Marekani kimemtunuku Shahada ya Udaktari wa Heshima katika Thiolojia, Askofu Shoo.

Moshi. Mkuu wa Dayosisi ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo ametoa wito kwa watawala na vyombo vya usalama kuzingatia na kuheshimu wito wa viongozi wa dini kuhusu haki, amani na usalama wa raia.

Dk Shoo ambaye ni askofu, mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na mkuu wa KKKT mstaafu, amesema viongozi hao ni muhimu wakatoa hakikisho la haki, amani na usalama kutokana na mazingira ambayo nchi inayapitia.

Katika kipindi cha takribani miaka 10 kuanzia 2016, kumeibuka sintofahamu kuhusu matukio ya utekaji, kupotea na kuuawa kwa raia wasio na hatia kunakofanywa na genge la uhalifu lisilojulikana, lenye silaha na magari ya kisasa.

Ingawa takwimu za watu waliotekwa, kupotea au kuuawa bado zinabishaniwa, lakini hivi karibuni alitekwa Ally Kibao ndani ya basi na kwenda kuuawa kikatili, huku mwanaharakati, Mdude Nyagali akitekwa na watu wasiojulikana.

Wengine ni Deusdedith Soka na wenzake wote wakiwa viongozi na wafuasi wa Chadema, Abdul Nondo wa ACT-Wazalendo, mjumbe wa mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chonchorio na raia wengine.

Ukiacha hilo, kumekuwapo kilio cha rafu za uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na 2024 na uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani 2020, ambapo mambo hayo ni miongoni mwa yanayopigiwa kelele na viongozi wa dini.

Katika sikukuu ya Pasaka 2025, maaskofu wa KKKT, Anglikana, Katoliki na baadhi ya makanisa ya uamsho walipaza sauti juu ya matukio hayo na mengine, huku Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) likitaka haki katika uchaguzi.

Julai 2024, kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamadi Masauni, Serikali ilijibu kuwa nchi iko salama dhidi ya vitendo vya utekaji na inachukua hatua kuhakikisha wote walihusika wanachukulia hatua za kisheria.

Masauni alisema matukio ya utekaji yaliyotokea 2024 yalikuwa hayazidi manane na kuainisha yale ambayo wote waliohusika walikamatwa na kesi zao zilikuwa mahakamani, akisisitiza kuwa Serikali na vyombo vyake haina mkono na matukio hayo.


Alichosema Askofu Shoo

Akizungumza leo Juni 7, 2025 ikiwa ni siku chache baada ya Chuo Kikuu cha Midland kilichopo Nebraska nchini Marekani kumtunuku Shahada ya Udaktari wa Heshima katika Thiolojia, Askofu Shoo amesema tuzo hilo imempa chachu ya kupigania haki.

“Kwa neema ya Mungu Chuo Kikuu cha Midland, Nebraska, Marekani kimenipa udaktari wa heshima kwa kutambua mchango wangu kwa kanisa na jamii kipindi changu cha ukuu wa KKKT na uaskofu wa Dayosisi ya Kaskazini,” amesema na kuongeza:

“Udaktari huu wa heshima nimepewa pia kwa sababu ya masuala ya utetezi wa haki, amani, utunzaji mazingira, kusimamia ukweli wa injili na kuendeleza huduma za jamii kwa udiakonia, afya na elimu.”

Pia kutokana na kutunza uhusiano kati ya Dayosisi ya Kaskazini na makanisa mengine ndani na nje ya nchi.

“Nimeipokea kwa heshima kubwa. Mungu anatambua na kuheshimu pale tunapojitoa kwa dhati kuhudumia watu wake.

“Tusichoke kutenda mema na kuukataa uovu. Wito wangu kwa watawala na vyombo vya usalama, wazingatie na kuheshimu wito wa viongozi wa dini kuhusu haki, amani na usalama kwa wote. Wasingoje malaika washuke kusema nao,” amesema.

Hafla ya kumtunuku shahada ya udaktari wa heshima ilifanyika Mei 28, 2025 nchini Marekani kwa heshima ya Askofu Shoo aliyeongoza kwa miaka 10 KKKT kama mkuu wa kanisa na mkuu wa dayosisi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Masuala ya Elimu wa Chuo Kikuu cha Midland, Dk Jamie Simpson, alisema tukio hilo si tu la kumuenzi Askofu Shoo, bali ni kuendeleza urithi wa uhusiano wa kihistoria kati ya makanisa ya Kilutheri ya Nebraska na Tanzania.

“Leo tunashiriki hadithi ya ushirikiano iliyoanza zaidi ya miaka 100 iliyopita, hasa tangu mwaka 1922, ambapo Mchungaji Ralf Hult alitumwa katika maeneo ya Mlima Kilimanjaro kuanzisha huduma za kiroho,” alisema na kuongeza:

“Huo ulikuwa mwanzo wa urafiki mkubwa kati ya Tanzania na Nebraska ambao hadi leo unaendelezwa na viongozi kama Askofu Shoo.”

Kwa sasa chuo kina zaidi ya wanafunzi 1,600 na kinatoa elimu katika nyanja mbalimbali zikiwamo uongozi, biashara, afya, elimu na taaluma za kijamii.

Rais wa chuo hicho, Profesa Aly William alisema wameona ni vyema kumtunuku Askofu Shoo heshima hiyo kutokana na mchango wake wa kipekee.

“Askofu Shoo ameweka alama kubwa si tu katika Tanzania bali pia katika moyo wa ushirikiano wa kidini kati ya Marekani na Afrika. Ni fahari kubwa kwa taasisi yetu kumpa shahada hii ya heshima,” alisema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Askofu Shoo alisema: “Ninapokea heshima hii kwa unyenyekevu na moyo wa shukrani. Kwa zaidi ya karne moja, Midland imekuwa sehemu ya urithi wa kiroho na kijamii nchini Tanzania.”

“Elimu inayotolewa hapa si tu ya kitaaluma bali pia ya kujenga maadili ya kweli katika jamii. Tukio hilo limeashiria mwendelezo wa ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Marekani kupitia taasisi za kidini na elimu,” amesema.

Askofu Shoo alisema: “Kwa kunitunuku shahada ya udaktari wa heshima, Midland University imeonyesha namna taasisi za kielimu zinavyoweza kutambua na kuheshimu mchango wa viongozi wa kiroho katika maendeleo ya jamii.”