Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

FYATU MFYATUZI: Nimeamua kujipanga kuuza au kubinafsisha ubongo wangu!

Sihitaji ubongo tena. Kwanza, umenifyatua nikafyatua wengine hadi wanatishia kunifyatua kwa kuninyotoa roho. Ubongo umesababishe kero na hatari hadi nikageuka machukizo, ukiachia kujiudhi mwenyewe.

Ubongo umenibomoa badala ya kujijenga. Nilifyatua wengine ili wafyatuke na kuwafyatua wanaowafyatua nikaishia kujibomoa.

Mbali na ubongo kuniletea madhara kwa vile unachemka, zipo sababu zilizoko nje ya uwezo wangu zinazoniaminisha kuwa lazima niuuze lau nipate njuluku ya kupatia kanywaji.

Zifuatazo ndizo sababu zilizonisukuma kuuza hata kuubinafsisha ubongo wangu ili niwe huru:

Mosi, siku hizi sihitaji ubongo.

Wa nini wakati nina simu janja, kompyuta na gadgets nyingine ambavyo hufikiria kwa niaba yangu? Hapa sijaongeza akili mnemba (AI).

Pili, nina wanasiasa wanaoniwakilisha kwenye vyombo vya kufikiri kama vile kunitungia sheria hata kama zinanikandamiza au hazinifai. Hawa waungwana, kwa kutumia bongo zao, wanafanya ubongo wangu uende likizo.

Hebu fikiria. Kila ufikapo msimu wa kutengeneza kura za kula, wajanja hawa huja na kunihonga udohoudoho na udonodo mwingine tena kwa siku moja. Mie, huwapa kura ya kula kwa miaka mitano. Kwa ambao hawajajiandaa, msimu huu wa kulishwa ili kuliwa soon utaanza. Mafyatu kaeni chonjo saa mbaya.

Tatu, nina viongozi wanaotenda miujiza kiasi cha kufanya maisha yangu yawe poa. Juzi nilimsikia mmoja akisema kuwa ukiona wanakopa na kuomba, jua ni wakwasi.

Kwani, makapuku huwa hawakopi kwa vile hawaaminiki. Hakuna kilichonitisha kama upupu huu. Kama ni kweli kuwa kubomu na kukopakopa ni sifa ya utajiri na siyo sifa ya kipuuzi, inakuwaje kaya zinazokopa na kufadhiliwa zinaitwa kapuku? Kama fyatu kama huyu anapewa uongo, sorry uongozi, nini haja ya kuwa na ubongo unaoudhi kama wangu wa kifyatu? Lazima niupige seli kulalike.

Kwa vile ninao viongozi tena wenye bongo zinazochemka, shahada za juu na maono, kazi yangu ni kutafuna na kusifia miujiza hii badala ya kupoteza muda kufikiri kiasi cha kutaka zaidi ya kile nilichopewa.

Hivi kuku akianza kufikiri na kutamani kulala kitandani, amfugaye atamfanya nini? Je, kuku akiwa na ubongo kama wangu akaanza kuhoji ni kwa nini analishwa nafaka kavu na amlishaye anakula mayai yake yenye protini, ataishia wapi?

Mnajua mfugaji tamfanya nini? Na akimfanya nini, atamlaumu aliyemfanya nini au ubongo wake?

Nne, sihitaji ubongo kwa sababu baada ya viongozi wangu kutenda miujiza na kufanya maisha yangu kuwa swaaafi katika imani, siuhitaji. Kazi yangu ni kuimba mapambio na kusifia na hii haihitaji ubongo bali utumbo. Kusifia hakuhitaji ubongo, vinginevyo chawa wasingepata umaarufu kwa kufanya kazi hii isiyohitaji ubongo.

Tano, sihitaji ubongo kwa sababu wengine niliowahusudu kama maprofesa walionifundisha wameonyesha wazi kuwa dunia ya sasa inahitaji usiwe na ubongo, bali meno, maneno matamu na utumbo ndipo uuufyatue kabla haujakufyatua. Watoto wa kihuni huita kuukata. Ukiwa na ubongo, unakukata badala ya kuukata.

Sita, kama ni masuala ya imani, ninao viongozi wa kiroho hata wenye uroho na roho mtakakitu hata kama nyingine ni za ajabu wanaoniombea kiasi cha kutohitaji ubongo kwa kazi yoyote ya Mungu hata shetani.

Kwa vile dini yangu hainigeuzi kondoo ili wachunaji wanichune, sihitaji ubongo. Ubongo wa nini iwapo naweza kula na kunywa kwa miujiza na sala? Anayebishia hili, ajiulize ni kwa nini watu wanapanda neno badala ya mbegu na kuvuna utajiri tena chapchap na hakuna mwenye ubongo anayehoji.

Je, hii siyo miujiza? Palipo na miujiza hapahitaji kuwa na ubongo, bali imani. Na imani haitaki ubongo bali kukubali kila jambo hata kubadilishiwa jina na ubinadamu.

Saba, lijapo suala la kupata njuluku, sihitaji ubongo ndiyo nizipate. Wa nini wakati, siku hizi, hata chawa anapata njuluku nyingi kuliko mchumi. Katika usawa huu ambapo wachumi wamegeuka wachumia tumbo, na utumbo unauzidi ubongo, ubongo wa nini wakati ukifikiri kwa tumbo unapata njuluku?

Nane, nina uzoefu mkubwa wa kutumia ubongo kufikiri. Kwanza, kufikiri kunaumiza kichwa na hata kuuchosha mwili. Pili, kufikiri kunaamsha na kujenga tabia ya kuhoji na kupinga kiasi cha mwenye kuwa nao kuonekana mchokozi na mpingaji. Nani anataka ubongo ili autumie kujiumiza kwa kuhoji na kushuku hata kupinga wateule tena wa Sir God?

Tisa, sihitaji ubongo kwa sababu kuwa na ubongo ni dhambi kuu katika mazingira ya jinai. Ubongo ni kiungo kidogo, kama mdomo, madhara yake makubwa. Unadhani bila ubongo, waandishi wa umbea wangebanwa kama wanavyobanwa na wenye mamlaka?

Kumi, ukiwa na ubongo, unadai kila kitu na kukigeuza haki wakati wewe si mwenye haki. Kwa kutumia ubongo wangu, kuna kipindi nilijidanganya kuwa mimi ni mwenye kaya wakati wenyewe wapo.

Baada ya kugundua walivyoniangalia na kutaka kunifyatua, niligundua kuwa dawa ni kuuza au kubinafsisha ubongo.

Hivyo, usinishangae na kudhani nimefyatuliwa na mibangi hadi napanga kuuza ubongo. Je, wewe unao? Du! Kumbe naota!