Doyo achukua fomu kurithi mikoba ya Hamad Rashid ADC

Muktasari:
- Aahidi kusukuma ajenda za kuleta mabadiliko kwenye sheria zenye matatizo, maisha bora kwa Watanzania
Dar es Salaam. Doyo Hassan Doyo amechukua fomu kuwania uenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) akitaja mambo matatu yaliyomsukuma kuwania nafasi hiyo.
Doyo ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa ADC ni miongoni mwa waanzilishi wa chama hicho.
ADC inaongozwa na Hamad Rashid anayemaliza muda wake kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.
Katiba ya ADC inasema, nafasi ya kiongozi ni vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja, baada ya hapo hataruhusiwa kugombea tena.
Doyo amechukua fomu leo Jumanne Juni 11, 2024 makao makuu ya chama hicho. Mgombea mwingine aliyechukua fomu kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti -Bara ni Scola Kahana.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu, Doyo amesema akipata ridhaa ya kuwa mwenyekiti wa ADC atasukuma ajenda za kuleta mabadiliko kwenye sheria alizosema zina matatizo.
"Hii ni ahadi nimeizungumza tangu nilipotangaza nia, nitaenda kwenye majukwaa ya kisiasa kusukuma ajenda za kuleta mabadiliko ya kisheria kwa zile zenye matatizo," amesema.
Jambo lingine ni kusukuma ajenda ya maisha bora kwa Watanzania.
"Hali ni ngumu ili kujikwamua kunahitajika msukumo wa viongozi kama mimi, Serikali iliyopo madarakani ione namna ya kufanya marejeo ya sera zake," amesema.
Pia, amesema atafanya siasa nzuri na za kistaarabu kwa mikakati ya kuijenga ADC iwe chama mbadala kitakachoshinda kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu.
Uchaguzi ndani ya chama hicho utafanyika Juni 29. Amesema atarejesha fomu Juni 20.
Awali, katibu wa kamati ya uchaguzi, Innocent Siriwa amesema mchakato wa kuchukua fomu na kurejesha unaendelea, hivyo wanachama wajitokeze kugombea.
Amewataka kufanya kampeni za kistaarabu, akionya kwamba kuna penalti kwa watakaoenda kinyume.
"Kuna kanuni ambazo zina penalti na ukienda kinyume unaenguliwa,” amesema Siriwa.