Dk Mutungi azikwa, Heche asisitiza kuendelezwa ndoto yake ya mageuzi
Ibada ya mazishi wa aliyekuwa mwasisi wa hama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Medard Mutungi
Muktasari:
- Dk Mutungi, aliyeshika wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu Bara, Chadema, kuanzia mwaka 1998 hadi 2004, alizaliwa mkoani Kagera. Alifariki dunia Aprili 26, 2026, baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa kiharusi alioupata tangu mwishoni mwa mwaka 2002, kwa mujibu wa wasifu uliosomwa na familia yake.
Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche ameongoza mazishi ya aliyekuwa mwasisi na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, Dk. Medard Mutungi, akimtaja kuwa miongoni mwa watu waliokuwa na ari kubwa ya kuona mageuzi ya kweli ya uchumi.
Dk Mutungi, aliyeshika wadhifa huo kuanzia mwaka 1998 hadi 2004, alifariki dunia Aprili 26, 2026, baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa kiharusi alioupata tangu mwishoni mwa mwaka 2002, kwa mujibu wa wasifu uliosomwa na familia yake.
Akizungumza Dar es Salaam leo, Aprili 28, 2026, baada ya kukamilika kwa ibada ya kuaga mwili wa kiongozi huyo iliyofanyika katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe, Mwenge, na kuhudhuriwa na makada mbalimbali wa chama hicho, Heche amesema mwaka huu umekuwa wa huzuni kubwa kwa chama hicho.
Viongozi na makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa cham hicho, Heche John na Katibu Mkuu wake, John Mnyika wameshiriki ibada ya mazishi wa aliyekuwa mwasisi wao Dk Medard Mutungi.
Amesema wamepoteza waasisi wawili, akiwemo Edwin Mtei aliyefariki dunia Januari 20 mwaka huu, ambaye pia alikuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
“Historia ya Dk Mutungi inaakisi kuanzishwa kwa Chadema. Hiki ni chama kilichoanzishwa na wasomi wa hali ya juu, wafanyabiashara na watu waliotamani mabadiliko ya kweli. Ndiyo maana wasifu wa waasisi wake ni mkubwa na unaonesha dhamira ya mageuzi ya kweli,” amesema Heche.
Ameongeza kuwa wao wamepokea kijiti kutoka kwa waasisi hao na kuahidi kuendeleza mazuri yote waliyoacha, ili kuhakikisha ndoto zao za kuona mageuzi zinatimia na Watanzania wanapata maendeleo bora ya kiuchumi.
“Kwanza ni kushinda mamlaka ya nchi kwa njia ya demokrasia na kubadilisha maisha ya wananchi. Hilo ndilo lengo na imani waliyojawa nayo, na sisi viongozi tulio hai tutailinda kwa wivu mkubwa,” amesema.
Heche amesema kutokana na uzito wa tukio hilo, waliacha vikao vya kamati na kuungana na wanachama pamoja na ndugu na familia ya marehemu ili kumsindikiza katika safari yake ya mwisho.
Viongozi na makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wameshiriki ibada ya mazishi wa aliyekuwa mwasisi wao Dk Medard Mutungi.
Kwa upande wake, msemaji wa familia ambaye pia ni mdogo wa marehemu, Jaji Francis Mutungi, ambaye ni Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, aliwashukuru wote walioshiriki kuifariji familia hiyo katika kipindi chote hadi siku ya mazishi.
“Marehemu alifanya kazi katika taasisi nyingi. Tunawashukuru wote mliohudhuria ibada hii. Nafahamu kuna watu wengi wamekuja kuwakilisha makundi mbalimbali, tunawashukuru kwa uwepo wenu,” amesema Jaji Mutungi.
Awali, katika wasifu wa Dk Medard Mutungi, imeelezwa kuwa alianza kazi yake ya utumishi wa umma katika ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza kama msajili wa silaha, kabla ya kujiunga na Benki ya Standard ya Afrika Kusini akiwa karani.
Viongozi na makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wameshiriki ibada ya mazishi wa aliyekuwa mwasisi wao Dk Medard Mutungi.
Pia alifanya kazi katika kampuni ya zao la tumbaku pamoja na taasisi nyingine mbalimbali. Ameacha watoto wanne, wajukuu watano na vitukuu watatu.