Devotha Minja atangaza kujiondoa Chadema akisema, ‘hakuna kushusha silaha chini’

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kati, Devotha Minja ametangaza kujiondoa ndani ya chama hicho akisema: “Aluta kontinua, hakuna kushusha silaha chini, mapambano yaendelee.”
Minja ambaye amewahi kuwa mbunge wa viti maalumu kupitia chama hicho (2015-2020) ametangaza uamuzi huo leo Alhamisi, Mei 15, 2025 katika mkutano wake na waandishi wa habari mkoani Morogoro akiwa ameambatana na baadhi ya wanachama.
Kanda ya kati yenye mikoa ya Singida, Morogoro na Dodoma ni miongoni mwa kanda 10 za Chadema nchini huku Minja akiwa ndiye mwenyekiti pekee mwanamke anayeongoza kanda nyingine zikiongozwa na wanaume.
Mbali na Minja viongozi wengine mkoani humo waliotangaza kujivua uanachama ni pamoja na Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) Jimbo la Morogoro, Katibu wa Baraza la Vijana (Bavicha) Jimbo la Morogoro, Katibu Baraza la Wazee (Bazecha) Jimbo la Morogoro, mjumbe wa mkutano mkuu, wajumbe wa kamati tendaji jimbo la Morogoro Mjini pamoja na viongozi mbalimbali wa kata.
“Hii ni siku maalumu sana kwangu...dakika 20 zilizopita nilikuwa mwana Chadema kwa miaka kama 10, nimeshika nafasi mbalimbali ikiwa ni nafasi ya mjumbe wa kamati kuu, mwenyekiti wa kanda yenye mikoa ya Singida, Morogoro na Dodoma na nimekuwa mwanamke pekee ambaye nilishinda nafasi ya mwenyekiti wa kada, nikiwashinda wanaume wanne,” amesema Minja.
Minja ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Morogoro amesema akiwa mjumbe wa kamati kuu suala la No reforms, no election ‘bila mabadiliko hakuna uchaguzi: “Hakuna popote tulisema tunakwenda kuzuia uchaguzi, hakuna popote tulisema tunakwenda kuzuia uchaguzi, nasema haya kwa sababu nilikuwa mjumbe wa kamati kuu.”
Minja amesema tangu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akamatwe na kufunguliwa kesi ya uhaini viongozi waliobaki: “Wameshindwa kuitisha Kikao cha kamati kuu ili kujadili suala hili muhimu na nyeti na kujua tunakwendaje. Wanachama wameumizwa kwenye kesi, madhila yanakipata chama hakuna Kikao chochote.”
Endelea kufuatilia Mwananchi