Chadema yataja mkakati wake mpya

Naibu Katibu Mkuu Chadema, Amani Golugwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo mbalimbali ya chama hicho leo Aprili 11, 2025, Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Chadema imesema inapitia upya ratiba ya operesheni No reforms iliyovurugika ili kuendelea nayo.
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema operesheni ya kunadi ajenda ya No reforms, no election kwa wananchi itaendelea kama kawaida.
Chadema imesema lengo ni kufikisha ujumbe wa kuishinikiza Serikali kufanya mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.
Imesema kwa sasa inapitia upya ratiba ya mchakato kupitia kikao cha sekretarieti kinachoketi leo Ijumaa Aprili 11, 2025 katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Mikocheni, Dar es Salaam.
Operesheni kunadi ajenda ya No reforms ilianza Machi 23, 2025 katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Rukwa, kabla ya kuhamia Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Chama hicho kikiwa mkoani Ruvuma Aprili 10, ili kuhitimisha mikutano yake, Jeshi la Polisi lilisitisha kibali cha kuendelea kwa mikutano.
Jana Alhamisi Aprili 10, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya alisitisha kibali cha mikutano ya Chadema mkoani humo, akisema watakaokaidi watachukuliwa hatua.
Leo Ijumaa, Aprili 11, 2025 Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Aman Golugwa katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam amesema:
“Operesheni ya No reforms, no election itaendelea na leo sekretarieti ya chama Taifa itakutana kujadiliana na kupanga kuhusu mwendelezo wa operesheni.
“Mwenyekiti hayupo lakini viongozi waliopo, makamu wenyeviti Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na wajumbe wa kamati kuu operesheni itaendelea kwa kujiamini kabisa bila woga, kazi itaendelea.”
Golugwa amesema baada ya kikao cha sekretarieti, watatoa taarifa ya namna operesheni itakavyoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.
Pia amewashukuru Watanzania waliojitokeza kuunga mkono ajenda ya No reforms kila eneo viongozi wakuu wa Chadema walipopita kuinadi ajenda hiyo.
Kuhusu ‘Tone tone’
Wakati huohuo, Golugwa ametoa mrejesho wa kiwango cha fedha kilichopatikana kupitia uchangishaji fedha unaofanywa na Chadema kwa njia ya dijitali maarufu ‘Tone tone’.
Amesema tangu kuanza kampeni ya uchangiaji Februari 27, 2025 hadi Aprili 10 jumla ya Sh 105.6 milioni zimepatikana.
“Kwa niaba ya chama napenda kutoa shukrani zetu kwa Watanzania waliojitokeza katika kampeni ya ‘Tone tone’ ambayo wanachangia kidogo-kidogo kwa njia ya mitandao ya simu. Tumepata michango mingi, ikiwamo wengine kulipia malazi na kujaza mafuta kwenye magari ya viongozi,” amesema.