Prime
Chadema yaruhusiwa kuandamana kwa masharti magumu

Viongozi wa Chadema wakiwa kwenye moja ya mikutano waliyoifanya. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi nchini limeyaruhusu maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), lakini kwa masharti ya kwamba wahakikishe maandamano yao yanakuwa ya amani, hayasababishi kutendeka kwa vitendo vya kihalifu na kuzuia lugha za uchochezi.
Ruhusa hiyo imetolewa ikiwa imepita siku moja baada ya Chadema kueleza kwamba viongozi wake walizungumza na jeshi hilo na kukubaliana kwamba maandamano hayo yafanyike bila kuzuiwa.
Juzi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliandika kwenye ukurasa wake wa X akisema timu ya Chadema ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu-Bara, Benson Kigaila ilikuwa na kikao na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro na timu yake kuhusiana na maandamano ya amani waliyoyapanga.
Mbowe alisisitiza makubaliano yalifikiwa maandamano yaendelee kama yalivyopangwa, “nalipongeza Jeshi la Polisi kwa busara hii. Karibuni Watanzania wote, tuandamane kwa Amani.”
Hata hivyo juzi, Jeshi la Polisi halikuwa tayari kuhusu kuthibitisha taarifa ya Chadema juu ya kuruhusiswa kuandamana.
Kigaila alijitokeza na kusisitiza maandamano hayo yatafanyika kama yalivyopangwa hata kama polisi hawatatoa kibali.
Kamanda Muliro, alipozungumza na gazeti hili alisema, “lengo la kuwaita ilikuwa kuwahoji juu ya viashiria vya uvunjifu wa amani na matamko ya kuchochea hisia za uvunjifu wa amani na tuliwahoji kuhusu matamko yao.”
Jana, Wakuu wa Polisi Wilaya (OCD) za Kariakoo, Buguruni na Magomeni walijibu barua za Chadema kwenda kwao (polisi) za kutoa taarifa juu ya maandamano hayo yenye vituo viwili vya Buguruni na Mbezi Mwisho.
Barua hizo ambazo zote zilikuwa na maudhui yanayofanana na kutofautiana saini za Ma- OCD walieleza kuruhusiwa kwa maandamano hayo iwapo yatakuwa ya amani.
Maandamano hayo yatakayoongozwa na viongozi waandamizi wa Chadema kuanzia asubuhi, yatahitimishiwa Ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) katika jengo la PSSSF, barabara ya Sum Nujoma, Ubungo.
Msingi wa maandamano hayo yaliyotangazwa Januari 13, mwaka huu ni kupinga miswada mitatu ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa bungeni Novemba 10, mwaka jana huku Chadema ikitaka iondolewe kwa kile wanachodai maoni ya wadau wengi hayakuzingatiwa.
Hoja nyingine ni ugumu wa maisha yanayowakabili wananchi.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dk Joseph Mhagama juzi alisema maoni ya wadau mbalimbali yalipokelewa. Hatua za kutungwa sheria zinaendelea ikiwemo Bunge zima, wakati ukifika miswada hiyo itajadiliwa.
Walichosema Ma-OCD
Katika barua za Ma-OCD hao wameandika, “kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zinazohusu ‘taarifa za maandamano’, hayatazuiwa na Jeshi la Polisi iwapo maandamano hayo hayataleta uvunjifu wa amani au kusababisha kutendeka kwa vitendo vya kihalifu.”
Jeshi la Polisi linatoa maelekezo kwa wanachama wa Chadema kuzuia lugha za kichochezi kwenye maandamano hayo pamoja na kuhakikisha kwamba maandamano hayo hayasababishi uvunjifu wa amani.
“Kwa barua hii viongozi wa Chadema na wanachama mnalo jukumu la kuzuia lugha za uchochezi, kejeli zinazoweza kupelekea kutendeka kwa vitendo vya uvunjaji wa sheria.
Mtalazimika kufuata utaratibu wa kisheria katika maeneo yote kwa kadiri mtakavyoelekezwa na wasimamizi wa sheria, polisi wakiwa ni kiongozi katika eneo hilo mlilolitolea taarifa.
“Maandamano hayo yasisababishe uvunjivu wa amani, watu kuibiwa au kuporwa na yawe kwenye njia zilizokubaliwa. Taarifa yenu pia izingatie muda wa kilichoelezwa kwenye barua yenu, ikiwa ni pamoja na kutoanzishwa mambo mengine ambayo hayamo kwenye taarifa iliyotolewa Polisi,” inasisitiza barua hiyo ya Jeshi la Polisi.
Vilevile, barua hiyo inaeleza kwamba ukiukwaji wowote wa masharti hayo utalilazimisha Jeshi la Polisi kuchukua hatua za kisheria bila kusita ili kuzuia madhara ya kuvunjika kwa amani. Barua hiyo inasisitiza kuhusu umuhimu wa kudumisha amani na utulivu.
Muda mfupi baada ya kupata barua hiyo, Mbowe aliandika kwenye ukurasa wake wa X: “Polisi kutoa barua saa chache kabla ya maandamano siyo sahihi na inatafsiriwa kama mkakati wa makusudi wa kupunguza vibe letu! Anyway, tukutane barabarani kesho asubuhi kuanzia saa moja…Buguruni na Mbezi Mwisho.”
Siyo mara ya kwanza kwa Jeshi la Polisi kuruhusu mikutano ya hadhara katika utawala wa awamu ya sita, maandamano mengine yaliyoruhusiswa na kufanyika ni yaliyoandaliwa na Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha).
Maandamano hayo yalifanyika Mei 11, mwaka jana kuelekea Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam ambapo yalifanyika kwa amani na utulivu huku yalisindikizwa na polisi.
Huko nyuma, maandamano yalikuwa yakizuiliwa ambapo Jeshi la Polisi lililazimika kutumia nguvu kuwatawanya waandamanaji, jambo ambalo limekuwa likihojiwa na wadau wa demokrasia, licha ya kuwa sheria zinaruhusu.
Akizungumzia maandamano hayo, Happy John, mkazi wa Ubungo jijini Dar es Salaam, alisema ni vema yakafanyika kwa amani ili yasije yakatokea mauaji kama ilivyokuwa mwaka 2018.
Februari 16, 2018, maandamano ya Chadema yaliyofanyika Kinondoni yalisababisha mauaji ya mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini ambaye alipigwa risasi wakati wafuasi wa chama hicho wakiandamana kwenda ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kinondoni.

Viongozi wa Chadema wakiongoza maandamano ya kupinga vitendo vya uonevu bungeni Februari 10, 2013. Picha na tovuti ya Chadema
‘Ni masharti magumu’
Akizungumzia maandamano hayo, mhadhiri wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Conrad Masabo alisema masharti yaliyotolewa na jeshi hilo ni magumu, hasa lile la kutotumika kwa lugha za uchochezi, kwa sababu mamlaka ndiyo inayotafsiri lugha hiyo.
“Kinadharia, watawala ndio wenye mamlaka ya kutafsiri lugha ya uchochezi ni ipi, sasa wakiamua kusema umetumia lugha mbaya au nzuri ni utashi wao. Lakini kiuhalisia uchochezi sio jambo baya kama tunavyolitafsiri, unaweza kuchochea maendeleo,” alisema.
Kwa upande mwingine, alieleza hatua ya kuruhusu maandamano hayo licha ya masharti yaliyotolewa, ni turufu kwa Serikali, kwani ingekosa cha kuieleza jumuiya ya kimataifa iwapo ingekataa.
“Kwanza, itapunguza tension (hofu) ya kisiasa, waliokuwa wanawaona Chadema ni waovu hawatawaona na sura hiyo tena, lakini Serikali inajijengea sura nzuri mbele ya jumuiya ya kimataifa,” alisema.
Hata hivyo, mhadhiri huyo alidokeza kile alichokiita ni hisia zake binafsi kwamba, uamuzi wa Serikali kuruhusu maandamano umelenga kumuokoa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
“Nadhani ni katika kumuokoa Mkuu wa Mkoa (Chalamila) na matamshi yake, kwa sababu alivyotamka ilieleweka kwamba anatumia jeshi kuzuia maandamano, kwa hiyo katika kuliondoa hilo, lazima maandamano yaendelee,” alisema.
Hisia nyingine, alisema pengine kauli ya Mkuu wa Majeshi, Jenerali Jacob Mkunda kuwa ndani ya Serikali wapo wakimbizi walioteuliwa kushika nafasi za maamuzi, imelegeza nguvu ya kuzuia maandamano hayo.
“Kauli hiyo maana yake kuna changamoto kwenye vyombo vya uchunguzi kabla ya uteuzi, sasa kama kuna shida hiyo inawezekanaje useme una intelijensia kiasi cha kuzuia maandamano kwa hofu ya amani,” alisema.
Hoja nyingine iliyoibuliwa na msomi huyo ni kila upande kati ya Jeshi la Polisi na Chadema, unaingia katika utekelezaji wa kazi yake bila uzoefu.
“Jeshi la Polisi halina uzoefu wa kuongoza maandamano ya upinzani kwa sababu hayakuwahi kuwepo, lakini Chadema nao wanaandamana wakiwa hawana uzoefu wa kuandamana kwa kuwa hawakuwahi kupata ruhusa, kwa hiyo kila mmoja anajifunza,” alisema.
Iwapo yatafanyika kwa mafanikio, alieleza yatafungua ukurasa mpya wa demokrasia nchini na utawala wa Rais Samia kuandika rekodi.
“Kama litafanikiwa lisilete rabsha, litafungua ukurasa mpya kwa Serikali kuona kwamba maandamano sio tatizo na upinzani.
“Kiuhalisia kabisa mimi nadhani sasa Samia atakuwa amevunja rekodi, ni yeye sasa huko mbele aamue atafanyaje. Nakumbuka aliahidi anaweza kufanya mabadiliko yoyote hata yanayoweza kugharimu nafasi yake,” alisema.
Ukurasa mwingine
Mwanazuoni wa sayansi ya siasa na sheria wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST), Profesa Ambrose Kessy alisema hatua ya kuruhusu maandamano hayo inafungua mawanda mapana ya demokrasia nchini.
“Kama mtu havunji sheria na anafuata miongozo ya Serikali kama alivyoelekezwa na anaona namna nzuri ya kufikisha ujumbe wake ni kutumia watu wengi, basi aruhusiwe na ndicho kilichofanyika,” alieleza.
Profesa Kessy ambaye pia ni Mkuu wa LST, Mipango, Fedha na Utawala, alisema kilichofanyika ni ukomavu wa hali ya juu ya demokrasia.
“Kwa sababu Katiba inaruhusu hilo kwamba mtu ana uhuru wa kueleza mawazo yake, kilichofanyika maana yake Serikali imetafsiri sheria vizuri,” alisema.
Aliwaasa wanaokwenda kuandamana kuhakikisha wanafuata taratibu za kisheria na kuzingatia kudumisha amani, wasikengeuke ili ruhusa hiyo iendelee kuwepo.
Ukuta, Akwilina

Aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini alipigwa risasi Februari 16, 2018 wakati wa maandamano ya wafuasi wa Chadema kudai barua za mawakala wao walioteuliwa kusimamia uchaguzi mdogo wa ubunge. Picha na Mtandao
Agosti 31, 2016 Chadema waliahirisha maandamano waliyoitisha ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).
Viongozi wa upinzani, akiwemo Edward Lowassa wa Chadema, wametangaza hatua hiyo kwenye kikao na wanahabari Dar es Salaam.
Walisema wameahirisha maandamano hayo kwa kipindi cha mwezi mmoja baada ya kusikia ombi la viongozi wa dini na wadau wengine waliowaomba kukumbatia na kuyapa muda mazungumzo.
Hata hivyo hawakuitisha tena maandamano hayo na mara kadhaa Rais John Magufuli aliyekuwa madarakani alionekana kutokuwa tayari kufanya mazungumzo na viongozi wa Chadema juu ya madai yao.
Februari 16, 2018 mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini alipigwa risasi wakati wafuasi wa Chadema wakiandamana kwenda ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kinondoni kudai barua za mawakala wao walioteuliwa kusimamia uchaguzi mdogo wa ubunge.
Hata hivyo, polisi waliwazuia waandamanaji hao, hali iliyosababisha vurugu kati ya pande hizo mbili.
Vurugu hizo ziliwafanya polisi watumie mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya waandamanaji na ndipo risasi moja inadaiwa kumpiga mwanafunzi huyo aliyekuwa ndani ya daladala.