VIDEO: Chadema, Polisi warushia mpira wa maandamano

Viongozi wa Chadema wakiwa kwenye moja ya mikutano waliyoifanya. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Hatima ya maandamano hayo itajulikana kesho, polisi watakapotoa taarifa
Dar es Salaam. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikisema maandamano yao yanayotarajiwa kufanyika keshokutwa yameruhusiwa na yatalindwa na polisi, jeshi hilo Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesema taarifa hiyo si ya kweli.
Akizungumza kwa simu leo, Jumatatu Januari 22, 2024, Kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro amesema hawajatoa taarifa yoyote ya kuruhusu au kukataza maandamano hayo.
Hata hivyo amekiri kukutana na wawakilishi wa Chadema wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu (Bara) wa chama hicho, Benson Kigaila leo saa tano asubuhi na kufanya mazungumzo mpaka saa tisa alasiri.
“Sipendi taarifa za uongo, ukiitwa sema ulichoitiwa na mlichozungumza,” amesema Kamanda Muliro na kuongeza:
“Lengo la kuwaita ilikuwa ni kuwahoji juu ya viashiria vya uvunjifu wa amani na matamko ya kuchochea hisia za uvunjifu wa amani na tuliwahoji kuhusu matamko yao.”
Kamanda huyo amesema kuhusu kukubali au kutokukubali Chadema kufanya maandamano, hilo litajulikana kesho saa saba mchana.
“Walitaka tuwajibu kuhusu barua walizoandika kuhusu maandamano, lakini tuliwajibu kuwa majibu watayapata kwa maandishi kwenye maeneo ambayo waliwasilisha kama walivyoleta barua zao,” amesema Muliro.
Mwananchi Digital, limemtafuta pia Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema azungumzie jambo hilo naye amesema:
“Makubaliano yetu ni kwamba maandamano yapo palepale, jambo moja ambalo polisi wamesema wanataka kujiridhisha kama Ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) yatakapoishia wako tayari kuyapokea maandamano yetu na sisi tukasema ndiyo.”
“Wakasema watafuatilia. Tulipowaeleza UN wenyewe wakasema watawasiliana na polisi. Kwa hiyo wanachokifanya polisi ni kutaka kuzuia maandalizi yasiwe kabambe,” amesema Mrema.
Mapema katika mkutano na waandishi wa habari leo, alasiri katika ofisi za chama hicho zilizoko Kinondoni jijini hapa, Naibu Katibu Mkuu Chadema – Bara, Benson Kigaila amesema Jeshi la Polisi limethibitisha kuyalinda maandamano yao na maandalizi ya yamekamilika kwa asilimia 100.
Amesema walipokea wito kutoka kwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro wakaonane naye wazungumze namna maandamano yatakavyokuwa.
"Tumekwenda kuonana na polisi na tukajadiliana kwa kirefu kuanzia saa tano mpaka saa tisa alasiri, tumekubaliana kwamba maandamano yetu yatafanyika kama ilivyopangwa na yatafanyika kwenye njia zilizopangwa.
“Mkiona polisi siku ya maandamano msiogope, mjue wamekuja kulinda maandamano,” amesema Kigaila.
“Na ninapenda kuwataarifu kuwa maandamano yetu ya Januari 24, yamekamilika kwa asilimia 100, tunachosubiri ni siku yenyewe, tufanye maandamano yetu ya amani," amesema Kigaila.
Amesema wamekubaliana chama kihakikishe maandamano hayo yanafanyika kwa usalama kama walivyosema ni maandamano ya amani.
Kigaila, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kile alichosema limeanza kupata weledi unaotakiwa katika majukumu yake.
"Tunaalika kila Mtanzania anayejua kuwa gharama za maisha ni shida kwake na hili halina vyama, tunaalika wapenda demokrasia na wapenda haki kuungana nasi kudai uchaguzi huru na haki na tume huru," amesema.
Amesema kila anayepinga miswada ya sheria za uchaguzi iliyopelekwa bungeni anapaswa kuungana nao katika maandamano hayo.
Amesema maandamano hayo yataanzia Buguruni na Stendi ya mabasi ya Mbezi kuelekea makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) na yatapokelewa na Mkuu wa UN nchini Tanzania.
“Tunakwenda UN na wenyewe wakiwa na taarifa kwamba tutaenda kwenye ofisi zao,” amesema Kigaila.
Ameongeza kuwa siku hiyo pia itakuwa ni ya uzinduzi wa maandamano nchi nzima na yataendelea kwenye mikoa mingine kutokana na ratiba ilivyopangwa.
Januari 17, 2024, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza maandamano hayo yakiwa na lengo la kupinga miswada ya sheria za uchaguzi iliyopelekwa bungeni Novemba, mwaka jana.