Prime
Chadema yapigilia msumari msimamo uchaguzi 2025

Muktasari:
- Lissu asema bila mabadiliko ya kisheria na Katiba, uchaguzi hauwezi kufanyika. Vyama vingine vyaendelea na maandalizi, huku Serikali ikisisitiza uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa Oktoba 2025.
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepigilia msumari msimamo wake wa kuhakikisha uchaguzi haufanyiki nchini kama mabadiliko ya msingi katika mfumo wa uchaguzi hayatafanyika.
Chama hicho kimebainisha kwamba hata mabadiliko wanayoyataka yakifanyika mwaka huu, bado uchaguzi hauwezi kufanyika kwa sababu utahitajika muda wa utekelezaji wa mabadiliko hayo, kama vile mabadiliko ya sheria, Katiba na uandikishaji wa wapigakura.
Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, amesisitiza msimamo huo leo Jumapili, Machi 2, 2025, kwenye majadiliano na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), akisema chama hicho kinakwenda kupigania mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi ambao umekuwa na matatizo kwa miaka mingi.

Chadema kupitia kaulimbiu yake ya "No Reforms, No Election" (Bila Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi), kinakutana na wadau mbalimbali nchini ili kuwashawishi kuunganisha nguvu katika vuguvugu walilolianzisha.
Hadi sasa, Lissu amesema amekutana na baadhi ya wazee, akiwemo Jaji Joseph Warioba. Pia, amekutana na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Itakumbukwa siku chache zilizopita wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi, Lissu alieleza namna kaulimbiu hiyo haijaeleweka vizuri kwa wanachama na wapenzi wengine wa chama hicho.
Wakati chama hicho kikiendelea na vuguvugu hilo, vyama vingine vya siasa vinaendelea na maandalizi ya uchaguzi mkuu Oktoba 2025, vikiwa na msimamo tofauti na wenzao wa Chadema.
Tayari Chama cha Mapinduzi (CCM), kupitia mkutano mkuu wa Januari 18-19, 2025, kimewapitisha wagombea wake wa urais ambao ni Rais Samia Suluhu Hassan kwa upande wa Tanzania na Dk Hussein Mwinyi kwa upande wa Zanzibar, na Dk Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza wa Samia.
ACT Wazalendo nacho kimetangaza kukaribisha watia nia ya kuwania nafasi za uongozi kupitia chama hicho, na hadi sasa Kiongozi wa chama, Dorothy Semu, ndiye ametangaza nia ya kugombea urais wa Tanzania, wakati Othman Masoud Othman naye akitangaza nia upande wa Zanzibar.
Chama cha ADC, pia, kimesisitiza kushiriki uchaguzi mkuu ujao na kupitia kaulimbiu ya "Kama mbwai na iwe mbwai" kinakwenda kupigania mabadiliko ya muhimu baada ya kuchaguliwa na wananchi kwenye uchaguzi huo.
NCCR-Mageuzi, kimeishaeleza kitashiriki uchaguzi na mgombea wao wa urais atafahamika mwezi ujao. Vyama vingine navyo vinaendelea na maandalizi.
Akizungumza kwenye majadiliano na wahariri, Lissu amesema mambo muhimu yaliyokifanya chama chake kuja na kaulimbiu hiyo kuelekea uchaguzi wa Oktoba 2025 ni pamoja na kupinga mfumo kandamizi wa uchaguzi.
Amesema tume mbalimbali zilizoundwa na marais miaka ya nyuma, zimebainisha mfumo wa uchaguzi wa Tanzania hautengenezi mazingira sawa ya uchaguzi kwa vyama vyote vya siasa.
"Tume ya Jaji (Francis) Nyalali ilisema katika ripoti yake ya mwaka 1991, kwamba mfumo wa uchaguzi ni wa chama kimoja, ulitengenezwa kukiimarisha chama kimoja.
“Tume hiyo ikapendekeza mfumo wa uchaguzi na taasisi zake ubadilishwe ili pendant na mazingira ya vyama vingi. Ilipendekeza mabadiliko hayo yafanyike kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995," amesema.
Lissu amesema lugha inayotumia ya ‘No reform no election’ imekuwa kali kwa sababu wanataka mfumo wa sasa wa uchaguzi ufanyiwe mabadiliko kwa madai sio rafiki kwa upinzani.

Hata hivyo, Aprili mwaka jana, Serikali iliwasilisha bungeni miswada ya sheria ya mabadiliko ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024, Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 2024, Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa ya mwaka 2024.
Pamoja na mambo mengine mabadiliko hayo ya sheria yalibadili jina la tume na kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), utaratibu wa kupata maofisa wa tume hiyo na kuweka takwa la mgombea kutopita bila kupingwa.
Msingi wa mabadiliko hayo ni kutokana na malalamiko ya vyama vya upinzani kuhusu sheria hizo zinazosimamia uchaguzi.
Akizungumzia kampeni hiyo, Lissu amesema ilipitishwa na Kikao cha Kamati Kuu cha Desemba 2-3, 2024, chini ya uenyekiti wa Freeman Mbowe, na kuungwa mkono na mkutano mkuu wa Januari 21, 2025, ambao nao uliongozwa na Mbowe.
Amesema shida kubwa zinazowasukuma kutaka uchaguzi wa mwaka huu usifanyike kama hakuna mabadiliko ni pamoja na mfumo wa uchaguzi kudhibitiwa na Rais.
Amesisitiza Chadema haijasema itasusa uchaguzi, bali itazuia uchaguzi, "hatujarembaremba hapo, tutawaalika Watanzania kuunga nasi kupinga mabadiliko hayo."
Hivi karibuni, viongozi waandamizi wa CCM, akiwamo Makamu Mwenyekiti Bara, Stephen Wasira, alisema uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 utafanyika kama ulivyopangwa na hakuna chombo chochote cha Serikali kinachoweza kuukwamisha.
Alisema wanaosema pasipo mabadiliko haufanyika wanaota ndoto ya mchana, huku akiwaomba Watanzania kuendelea kujiandaa na uchaguzi huo.
Wasira alieleza hayo Februari 11, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, akisema licha ya msimamo wao huo wa Chadema, uchaguzi utafanyika baada ya Tume Huru ya Uchaguzi kutangaza tarehe kama ilivyopewa mamlaka na Katiba ya nchi.
“Sisi ni wadau wa uchaguzi, kazi yetu ni kuitumia dola kuleta mabadiliko ya watu, kwa hiyo hatuwezi kuambiwa hakuna uchaguzi. Wao kama wanataka kuingia kwenye uchaguzi, bahati mbaya sisi tunawakaribisha maana uwezo wa kuwashinda tunao. Wanatusingizia CCM wanaiba, tunaiba nini?"
"Sasa mimi nataka kuwaambia hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuhairisha uchaguzi. Hakuna! Hakuna chombo chochote kiwe cha kiserikali au cha nani kinachoruhusiwa kuhairisha uchaguzi. Ibara ya 41, sehemu ya nne ya Katiba inaipa tume mamlaka ya kutangaza tarehe ya uchaguzi, na wakati utakapofika tume itatangaza tarehe ya uchaguzi,” amesema.

Mbali na Wasira, Rais Samia, akiwa ziarani Mkoa wa Tanga, aliwahamasisha wananchi kuendelea kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura na wakati ukifika wa kupiga kura, wajitokeze kwa wingi.
Nguvu ya Rais, majimbo
Katika maelezo yake, Lissu amesema Rais ana nguvu ya kuteua mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, makamu wake, wajumbe wa tume na wasimamizi wa uchaguzi ambao sheria inaeleza kuwa wawe watumishi wa umma waandamizi.
“Kwa Katiba ya Tanzania, watumishi wa umma ni wateule wa Rais na wanafanya kazi kwa niaba ya Rais. Kilichobadilika kwenye sheria ni maneno tu, badala ya kusema wakurugenzi, sasa wanasema watumishi waandamizi,” amesema Lissu.
Jambo lingine, Lissu amesema mgawanyo wa majimbo umekuwa hauna uwakilishi sawa na kwamba majimbo yamekuwa yakigawanywa kwa kuangalia jiografia badala ya idadi ya watu.
Ametolea mfano Zanzibar kuwa na majimbo 50, ikiwa na idadi ndogo ya watu, wakati mkoa wa Dar es Salaam, wenye idadi kubwa ya watu (wakati huo watu 3,427,000).
“Mfumo wetu wa mgawanyo wa majimbo umevurugwa, hauna uwakilishi wowote. Majimbo yanaanzishwa kwa kuwatengenezea urahisi baadhi ya watu ili warudi bungeni,” amesema.
Hata hivyo, Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) inatekeleza jukumu la mgawanyo wa majimbo kwa mujibu wa ibara ya 74 (6) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kifungu cha 10(1)(d) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024, ambavyo vimeipa tume jukumu la kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge.
Pia kwa mujibu wa ibara ya 75(4) ya Katiba, jukumu hilo linaweza kufanywa na Tume mara kwa mara na angalau kila baada ya miaka 10.
Akizungumzia ongezeko la gharama endapo tume itakuwa na watumishi wake hadi majimboni, Lissu amesema Serikali haiwezi kushindwa kulipa mishahara ya watu 5,000, ambao ni pamoja na wasimamizi wa uchaguzi 4,000 ngazi ya kata, wasimamizi 264 wa majimbo, na 31 kwenye mikoa yote nchini.
Lissu, aliyechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chadema Januari 22, 2025, akimshinda Freeman Mbowe, amebainisha pia ugonjwa wa kuengua wagombea wa upinzani kwenye chaguzi ni jambo wanalolipinga na wanakwenda kupigania lirekebishwe.
“Hakuna uchaguzi uliofanyika bila wagombea kuenguliwa. Mwaka 2020 ulitia fora kwa wagombea wengi kuenguliwa katika historia ya uchaguzi nchini.
“Wanaoenguliwa ni wagombea wanaoweza kushinda. Wasimamizi wa uchaguzi wanaengua wagombea kwa sababu wao ni watumishi wa umma, wanalinda maslahi ya Rais ambaye ni kiongozi wa watumishi wa umma," amesema.
Lissu amebainisha tatizo la kampeni kwenye uchaguzi zimekuwa hazitoi mazingira sawa kwa vyama vyote katika kupata haki ya kuweka mabango, kupata matangazo ya televisheni na haki ya kufanya mikutano ya hadhara.
Pia, Lissu amesema utatuzi wa migogoro ya uchaguzi ni suala lingine wanalolipigania katika kaulimbiu yao, kwa kuwa utaratibu wa kutatua migogoro hiyo haufai na hautoi haki kwa vyama vya upinzani.
Meza ya mazungumzo
Katika majadiliano hayo, wahariri walipata nafasi ya kuuliza maswali kwa Lissu na timu yake, akiwa na makamu mwenyekiti-Bara, John Heche, na Katibu Mkuu, John Mnyika, ambao nao walijibu maswali ya wahariri.
Mhariri mkongwe, Paschal Mayalla, alitaka kujua kwanini Chadema hawataki kutumia fursa ya kufanya mazungumzo ili kufikia mabadiliko wanayoyataka, badala ya kutoa masharti ya kukwamisha uchaguzi.
Akijibu swali hilo, Mnyika ameeleza Chadema wamekuwa kwenye mazungumzo kwa muda mrefu na wenzao wa CCM, na waliwasilisha hoja zao, ikiwemo kuukwamua mchakato wa Katiba mpya.
Hata hivyo, amesema CCM walikwamisha mazungumzo hayo kwa sababu hawakutaka kufanyia kazi madai yao ya kuukwamua mchakato
“Hakukuwa na utashi wa kisiasa wa kufanya mabadiliko ya aina yoyote. Baada ya mazungumzo marefu kwenye hoja hizo, tukawaambia tunataka mtujibu kwenye maeneo mawili; kuukwamua mchakato wa Katiba, na marekebisho ya kisheria ya kuwezesha uchaguzi huru na wa haki.
“Katika majibu yao ya maandishi, ilionekana wazi hawakutaka maridhiano yaendelee. Wakatujibu kwa maandishi namna ambavyo hawataki mchakato wa Katiba uendelee. Pili, wakatujibu kwa maandishi kukataa mapendekezo yetu yote ya kuwezesha uchaguzi huru na wa haki,” amesema.
Kwa upande wake, Heche amesisitiza chaguzi tatu zilizopita zinaonyesha dhahiri wana hoja ya msingi kupinga uchaguzi kuendelea kufanyika kwenye mazingira yaleyale ndiyo maana wanasisitiza kwamba "hakuna uchaguzi."
“Tunataka uchaguzi ambao mtu hata ukiwa nyumbani umeshinda uchaguzi utatangazwa, ndiyo tunachozungumza,” amesema Heche.