Prime
Chadema yabadili msimamo, kumpeleka Msajili mahakamani

Muktasari:
- Kamati Kuu ya Chama cha Demokarasia na Maendeleo (Chadema) iliyokutana Jumanne ya Juni 3, 2025 imetoka na maazimio mbalimbali ikiwamo kwenda mahakamani kumpinga Msajili
Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokarasia na Maendeleo (Chadema), John Heche amesema chama hicho kinatarajia kwenda mahakamani kumshitaki Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kupinga uamuzi wake dhidi yao.
Uamuzi wa Msajili unaotarajiwa kupingwa na Chadema ni kubatilisha uamuzi wa Kikao cha Baraza Kuu la chama hicho wa kuwateua viongozi na kukisitishia ruzuku.
Hatua hiyo inakuja, wiki moja tangu ofisi ya msajili iandike barua kwenda Chadema, ikiitaka iwaondoe viongozi wote waliothibitishwa na kikao cha baraza kuu la chama hicho la Januari 22, mwaka huu, lililodaiwa kuwa batili.
Mbali na viongozi hao, pia msajili alitaka wakurugenzi walioteuliwa na kamati kuu iliyokuwa na wajumbe waliothibitishwa na Baraza Kuu ambalo halikuwa na akidi kuangaliwa upya ili kutimiza matakwa ya sheria na kanuni za vyama vya siasa.
Pamoja na kuuondoa uongozi huo, Msajili pia alitangaza kusitisha utoaji wa ruzuku kwa chama hicho hadi hapo kitakapotekeleza maelekezo hayo.
Mzizi wa yote hayo, ni malalamiko ya mmoja wa makada wa Chadema, Lembrone Mchome aliyedai kikao hicho cha Baraza Kuu chini ya uenyekiti wa Tundu Lissu kilikuwa batili kwa kuwa, akidi haikuwa imetimia.
Mvutano baina ya Msajili na Chadema umedumu takribani wiki mbili, Chadema kupitia kwa Heche walikuwa wakisisitiza hawabatilishi uamuzi wa Baraza Kuu na wajumbe wanane akiwamo Katibu Mkuu, John Mnyika wataendelea na nafasi zao kama kawaida.
“Namwambia Msajili hahitaji kumtambua katibu mkuu wa chama chetu, sisi Chadema tunamtambua katibu mkuu wetu, huna uwezo wa kututeulia nani awe katibu mkuu wa chama chetu.
“Msimamo wa chama chetu, katibu mkuu wetu atateuliwa na mwenyekiti kama katiba inavyosema na mwenye malalamiko akate rufaa katika mkutano mkuu,” alisema Heche, Mei 13, 2025, akihutubia mkutano wa hadhara wa No reforms no election, huko Mgumu, wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara.
Hata hivyo, kikao cha kamati kuu kilichokutana jana Jumanne, Juni 3, 2025 makao makuu ya Chadema, Mikocheni jijini Dar es Salaam chini ya Heche kimetoka na uamuzi tofauti na wa awali.
Leo Jumatato, Juni 4, 2025, Heche katika mkutano wake na waandishi wa habari, ametoa maazimio ya kikao hicho alichokiongoza baada ya mwenyekiti, Tundu Lissu kuwa gerezani kutokana na kesi zinazomkabili ikiwamo ya uhaini.
Heche amesema chama hicho kimejiridhisha kuwa Msajili hana mamlaka ya kutafsiri katiba ya chama hicho kwa namna anavyoona yeye.
"Tunaenda mahakamani kwa sababu Msajili amejipa jukumu kama mtafsiri wa katiba yetu kwa maana yeye ndio anaijua katiba yetu kuliko sisi," amesema.
Sababu nyingine inayowapeleka mahakamani, amesema ni kitendo cha msajili kuzuia ruzuku ya chama, jambo alilosema ni kinyume na matakwa ya Sheria ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Heche amesema uamuzi wa Msajili kuzuia ruzuku kwa chama, kwa mujibu wa kifungu cha 18(6) cha Sheria ya Msajili wa Vyama vya Siasa, unapaswa kuchukuliwa baada ya kuwepo hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
"Tungestahili adhabu hiyo kwa mujibu wa kifungu hicho, iwapo kungekuwa na hoja ya CAG ya ama matumizi mabaya ya fedha na vinginevyo, lakini sio anakaa nyumbani anajiamria," amesema.
Hata uzuiwaji wa ruzuku wenyewe, amesema ulipaswa kufanywa kwa ofisi hiyo ya Msajili kuiandikia barua bodi ya wadhamini ya chama.
Heche amesema Msajili hana mamlaka ya kubatilisha uamuzi halali wa chama hicho, pia sio mamlaka ya rufaa na sio chombo cha kupokea malalamiko yoyote ya mwanachama.
"Kama kuna mwanachama wetu, amefanyiwa jambo baya, katiba yetu inakutaka ukate rufaa kwa ngazi husika na mamlaka ya rufaa ya eneo husika itasikiliza rufaa yako," amesema.
Amesema chama hicho kimegawanya vema mamlaka kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa hadi Taifa na kama mtu ana malalamiko kwa ngazi fulani afuate ngazi husika.
Heche amesema Chadema inakwenda mahakamani kwa lengo la kuweka kumbukumbu sawa kuwa, Msajili hana mamlaka ya kusikiliza wala kupokea uamuzi wowote wa chama.
Hata hivyo, amesema tayari wanasheria wa chama hicho wameshaelezwa kuhakikisha kabla ya Juni 13, mwaka huu wahakikishe kesi hiyo imefunguliwa.
Sambamba na hilo, Heche amesema kikao cha kamati kuu kwa mamlaka kiliyonayo, kimeazimia kuwakaimisha viongozi wake Mnyika kuwa kaimu katibu mkuu na wengine wote walioondolewa na Msajili wamekuwa kaimu manaibu, isipokuwa wajumbe wa kamati kuu.
Mbali na Mnyika, wengine ni Aman Golugwa kuwa kaimu naibu katibu mkuu Bara na Ali Ibrahim Juma kuwa kaimu naibu katibu mkuu Zanzibar.
Heche amesema tayari wamemwandikia barua Msajili wa vyama vya siasa juu ya mabadiliko ya uongozi huo.
Kuhusu wengine walioteuliwa na Lissu kuwa wajumbe wa kamati kuu na kuthibitishwa na Baraza Kuu ambao ni Godbless Lema, Dk Rugemeleza Nshalla, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh amesema wataendelea kuwa wajumbe wateule wa kamati kuu hadi Baraza Kuu litakapokutana.
Mbali na hao, Heche amesema kikao hicho kwa kutumia kifungu cha 7 (16)b cha katiba, kimemteua Tito Kitalika kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi, John Kitoka (Kaimu Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Diaspora, Brenda Rupia (Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi),” amesema Heche.
Wengine ni Gaston Garubindi (Kaimu Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu, Rems Kassanda (Kaimu Mkurugenzi wa Digital na Ubunifu).
Katika hatua nyingine, Heche amesema kamati kuu ya chama hicho, imeamua kuitisha Baraza Kuu ndani ya siku 60 kuanzia leo Jumatano, ili kujadili barua ya Ofisi Msajili wa Vyama vya Siasa.
Kabendera atimkia Chadema
Katika hatua nyingine, mmoja wa waanzilishi wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Engine Kabendera ametangaza kujiunga na Chadema, ikiwa ni wiki moja tangu alipotangaza kujiondoa katika chama chake cha awali.
Kabendera alitangaza kuihama Chaumma, wiki iliyopita akitaja sababu za uamuzi wake huo ni kutoridhishwa na mwenendo wa kilichokuwa chama chake, akisema kimekiuka misingi yake.
Kabendera kabla ya kujiunga na Chadema, alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma Bara na nafasi nyingine kadhaa za kitaifa.
Mwanasiasa huyo amepokewa na Kaimu Naibu Katibu Mkuu Bara, Amani Golugwa akisema Kabendera amekataa biashara yoyote inayoendelea nchini, kinyume na masilahi ya Taifa.
Akizungumza baada ya kupokewa, leo Jumatano, Juni 4, 2025 Kabendera amesema amegundua mwelekeo wa chama chake cha awali haukuwa unaendana na imani, maono na dhamira ya Taifa.
Amesema hakuingia kwenye siasa kwa ajili ya vyeo, badala yake aliingia kuhudumu na anapoona misingi hiyo inatikiswa na kutikisika huchukua hatua muafaka.
"Baada ya mashauriano ya kina na kutafakari nimeamua kujiunga na Chadema, huu sio uamuzi rahisi wala masilahi ya kisiasa. Ni uamuzi uliotokama na mshikamano wa kweli," amesema.
Amesema ni imani yake kuwa Chadema inatoa jukwaa la mabadiliko ya kweli hasa ndoto za jamii zilizotengwa, akisisitiza uamuzi wake umekuwa kwa ajili ya wananchi.