Prime
Chadema kuamua kusuka au kunyoa

Muktasari:
- Chama hicho kimekuwa kikipita kwenye misukosuko tangu uchaguzi wake wa ndani Januari 21, 2025 na kupata uongozi mpya wa Tundu Lissu kuchaguliwa kuwa mwenyekiti mpya akichukua nafasi ya Freeman Mbowe.
Dar es Salaam. Wakati Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ikitarajia kukutana kesho Jumanne, Juni 3, 2025, huenda ikatoka na uamuzi wa kusuka au kunyoa dhidi ya maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Chama hicho kimekuwa kikipita kwenye misukosuko tangu uchaguzi wake wa ndani Januari 21, 2025 na kupata uongozi mpya wa Tundu Lissu kuchaguliwa kuwa mwenyekiti mpya akichukua nafasi ya Freeman Mbowe.
Tangu wakati huo, chama hicho hakijatulia kutokana na kukabiliwa na mashambulizi ya ndani na nje huku viongozi wake wakiendelea na operesheni ya ‘No reforms, no election,’ wakikabiliana na changamoto hizo.
Mei 13, 2025, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilitengua uteuzi wa wajumbe wanane wa sekretarieti na Kamati Kuu ya Chadema, waliothibitishwa na Baraza Kuu la chama hicho Januari 22, 2025.
Wajumbe hao ambao Msajili hawatambui ni John Mnyika (Katibu Mkuu), Amani Golugwa (Naibu Katibu Mkuu-Bara), Dk Rugemeleza Nshala (Mwanasheria Mkuu), Ali Ibrahimu Juma, Godbless Lema, Rose Mayemba, Salima Kasanzu na Hafidhi Ali Saleh.
Mbali na kutengua nyadhifa zao, ofisi hiyo ilitoa maelekezo kwa chama hicho yanayopaswa kufanyiwa kazi ili kukidhi matakwa ya Sheria ya Vyama vya Siasa, kanuni na katiba ya Chadema.
Uamuzi huo ulifanyika kujibu malalamiko yaliyowasilishwa kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Lembrus Mchome aliyepinga uhalali wa viongozi waliothibitishwa na Baraza Kuu kwa sababu akidi haikutimia.
Mei 23, 2025, kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kilifanyika, makamu mwenyekiti wa chama hicho, Bara, John Heche alisema Kamati Kuu iliridhia kwa kauli moja kutokuijibu barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Barua hiyo ya Msajili aliituma kwa Chadema akielezea uamuzi wake wa kukitaka chama hicho kuitisha upya Baraza Kuu ili kuwaidhinisha viongozi wanane waliokuwa wameteuliwa na mwenyekiti wake, Tundu Lissu, Januari 22, 2025 kwani akidi haikuwa imetimia.
Katika kujibu uamuzi huo wa Kamati Kuu ya Chadema, Mei 27, 2025, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliwaandika barua Chadema kuwajulisha kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa, kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 18(6) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, ameamua kusitisha kuwapa ruzuku hadi watakapotekeleza maelekezo yake.
Barua hiyo ilieleza sababu kuwa ni chama hicho kukosa viongozi wanaoweza kusimamia mapato, matumizi na marejesho ya fedha hizo za umma.
Pia, barua hiyo kutoka Ofisi ya Msajili ilionya kwamba, endapo Chadema wataendelea kukaidi kutekeleza uamuzi na maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa, anaweza kuchukua hatua ikiwamo kusimamisha usajili wa chama hicho, kama kitaendelea kuwatambua viongozi ambao hawatambui.
Siku moja baada ya Msajili kueleza hatua atakazozichukua kutokana na Chadema kukaidi maelekezo yake, chama hicho kimeitisha kikao cha Kamati Kuu kesho Juni 3, 2025 kujadili barua ya Msajili.
Chama hicho kimebainisha kwamba baada ya kukutana kitatoa mwelekeo, huku kikidai Msajili anatishia kukifuta kinyume na utaratibu wa sheria.
Wakati sarakasi hizo zikiendelea, kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Lissu, inaendelea leo na amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kusikilizwa kwa shauri linalomkabili la uhaini na kuchapisha taarifa za uchochezi.
Huko nje, wakili wake wa kimataifa, Robert Amsterdam amewasilisha malalamiko Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu kuwekwa kwa Lissu kizuizini kinyume cha sheria.
Wakili huyo amewasilisha malalamiko hayo UN Ijumaa iliyopita kuhusu kuwekwa kizuizini kwa mwanasiasa huyo kinyume cha sheria, hatua inayolenga kuongeza shinikizo la kimataifa ili aachiliwe huru.
Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025 na kushtakiwa kwa uhaini, kosa ambalo adhabu yake ni kifo, kufuatia madai kuwa alitoa matamshi ya kuwataka wafuasi wake kuzuia uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 2025.
Kwa mujibu wa ripoti ya Reuters, wakili wa kimataifa wa Lissu, Amsterdam malalamiko hayo kwa UN ni sehemu ya kampeni ya kuishinikiza Serikali kumwachia huru kiongozi huyo wa Chadema.
Mtihani kwa Chadema
Chadema, kupitia kikao cha Kamati Kuu, watakuwa na machaguo mawili katika uamuzi watakaoufanya, ama kutekeleza maelekezo ya Msajili ya kuitisha kikao cha Baraza Kuu ili kurudia mchakato wa kuwathibitisha upya waliokuwa wameteuliwa au kusimamia msimamo wao.
Endapo wataamua kutekeleza maelekezo ya Msajili, bado watakabiliwa na changamoto ya kutumia akidi kwa sababu baadhi ya waliokuwa wajumbe wa Baraza Kuu wamejiondoa kwenye chama hicho, hivyo inaweza kuwa vigumu kupata akidi kwa sababu mapengo hayo hayajazibwa.
Pia, jambo hilo linahusisha fedha kwa ajili ya posho za wajumbe watakaohudhuria kikao hicho.
Bado haijafahamika utayari na uwezo wa Chadema kuitisha kikao hicho ili kutekeleza matakwa ya Msajili na kujiweka salama dhidi ya hatua atakazozichukua dhidi yao.
Hata hivyo, baadhi ya wadau wamedai kuwa, uamuzi wa Msajili ni kinyume cha sheria, hivyo Chadema watakuwa na nafasi ya kwenda mahakamani kupinga uamuzi huo endapo Kamati Kuu itaazimia hivyo.
Akizungumza leo Jumatatu Juni 2, 2025, mchambuzi wa siasa, Buberwa Kaiza amedai kuwa, Msajili anaingilia mamlaka isiyokuwa yake kwa sababu vyama vina katiba zao, yeye wajibu wake ni kuhakikisha vinafuata Sheria ya Vyama vya Siasa.
“Kamati Kuu ikikaa itaangalia maelekezo ya Msajili kama yanaendana na sheria au yanakiuka sheria. Kama yanakiuka sheria hawatayafuata, watayaacha, kama yanafuata sheria wataenda nayo na huo ndiyo mustakabali wa chama chenyewe.
“Msajili anatakiwa aelekeze chama kwa mujibu wa sheria inavyomruhusu, siyo nje ya sheria inavyomruhusu. Hapa ni suala la uadilifu, sheria inaongoza utaratibu wa vyama utakavyokuwa, sheria haisemi Msajili atakuja na mambo yake anavyotaka,” amesema Kaiza.
Kwa maoni yake, amesema msajili angekuja na mapendekezo baada ya kushuhudia namna mkutano wa Chadema ulivyofanyika na kueleza aliona nini katika mchakato wote, badala ya kumsikiliza kada mmoja aliyeibuka na malalamiko yake.
“Baada ya mtu kulalamika, yeye angechukua jukumu la kufanya tathmini, siyo kuelekeza cha kufanya kabla ya kufanya tathmini. Hata mahakamani, ukipeleka mashtaka, mtuhumiwa anaitwa, wanatafuta ushahidi na kuangalia kama sheria imevunjwa,” amesema.
Mchambuzi huyo wa siasa ameongeza kuwa, katika kutafakari hilo, kuna Sheria ya Vyama vya Siasa, kanuni zinazosimamia sheria hiyo na katiba ya Chadema na kanuni zake, ambavyo ndiyo vinasimamia utaratibu wa namna uchaguzi wa viongozi unatakiwa kuchaguliwa.
“Hiki ni kikao cha dharura kujadili hii hoja maalumu, watafuata ushauri wa kisheria, watamwandikia Msajili. Kama wataona kuna haja ya kwenda mahakamani watakwenda mahakamani kama wanaona Msajili hajafuata sheria,” amesema.
Wakili Kiongozi wa Kampuni ya Haki Kwanza, Alloyce Komba amesema njia pekee kwa Chadema kupata haki yao ni kwenda mahakamani, kwa kuwa, tayari walishaweka msimamo wao wa kutojibu barua ya Msajili.
“Mimi naamini, hiki kikao ambacho Chadema watakaa, uamuzi watakaopitisha, ni kina Dk Nshala (mwanasheria mkuu wa chama) kwenda mahakamani kupinga uamuzi wa Msajili, kwa sababu wanasema amevunja hata katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa.
“Sehemu pekee ambayo wanayoweza kwenda ni mahakamani, wakapate haki zao kwa mujibu wa Ibara ya 107(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwamba mgogoro wowote ule, Mahakama ndiyo mahali pake,” amesema Komba.
Hata hivyo, amewataka kuwa makini kwa sababu kesi kwa wakati huu zinaweza kuwaharibia mambo mengine ya kisiasa.
“Mnaweza kuchelewa vitu vingine vya kufanya, ninyi mkawa mnahangaika mahakamani tu, matokeo yanakuwa tofauti. Kwa hiyo inabidi wawe makini kuangalia mamlaka ya Msajili, kama kweli anayo, wanaweza kurudi kwake ili auangalie upya uamuzi wake,” amesema Komba.