Chadema yaitisha Kamati Kuu kujadili barua ya Msajili

Muktasari:
- Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche amesema kuwa chama hicho kitaitisha kikao cha Kamati Kuu Juni 3, kwa lengo la kujadili na kujibu barua kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Arusha. Ikiwa imepita siku moja tangu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kueleza hatua atakazochukua baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kukaidi maelekezo yake, chama hicho kimesema kitaitisha kikao cha Kamati Kuu Juni 3, 2025 kujadili barua ya msajili.
Chama hicho kimesema baada ya kukutana kitatoa mwelekeo, huku kikidai Msajili anatishia kufuta chama hicho kinyume na utaratibu wa sheria.
Maelekezo aliyotoa msajili kwa Chadema ni kutaka liitishwe Baraza Kuu la chama hicho ili wapate wajumbe wa Kamati Kuu na Sekretarieti ambapo Chadema kupitia Kamati Kuu kiliazimia kutokujibu kwa kile walichodai ofisi ya msajili haina mamlaka ya kufanya hivyo.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Mei 28, 2025 na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa Operesheni ya 'No reforms, No election' uliofanyika katika viwanja vya Soko Kuu Arusha.
Amesema kumekuwa na mbinu mbalimbali za kujaribu kuua chama hicho.

Wananchi waliohudhuria mkutano wa Chadema mkoa wa Arusha
"Kuna mashambulizi mengi yamefanyika shambulio la kwanza kutumia watu tuliokuwa nao kuandika barua… wapinge uchaguzi, uchaguzi wa wazi uliorushwa na tv zote kila Mtanzania akashuhudia.
"Wakaandika hiyo barua mwezi Machi wakaipeleka kwa msajili, lakini vilevile wakatumia viongozi tuliokuwa nao kutoka Zanzibar aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa chama chetu kutoka Zanzibar akaandika kesi ambayo aliifungua…kwamba chama kinadhulumiwa kutoka bara,"
Makamu huyo amesema kumekuwa na mbinu mbalimbali za kuua chama hicho.
"Jana nimemsikia msajili anasema kwamba anaifutia Chadema ruzuku, anatishia kufuta chama hiki kinyume cha utaratibu wa sheria. "Sisi tukamjibu msajili kwamba wewe siyo mamlaka ya rufaa kwenye chama chetu, chama chetu kina vyombo vyake vya kufanya rufaa kama mtu ana malalamiko, kwa hiyo kama mtu amekuja kwako mwambie arudi ndani ya chama ashughulikiwe ndani ya chama,” amedai Heche.
Makamu huyo amesema maamuzi yaliyotolewa na chama hicho ni maamuzi ya Kamati Kuu hayakuwa maamuzi yake binafsi na kilisema barua ya msajili ni batili.
"Na tumeendelea kuwatambua viongozi wetu tuliowateua kwenye Baraza Kuu.Tumeitisha Kamati Kuu ya chama tarehe 3, kujadili barua ya msajili na tutatoa mwelekeo wa nchi ni wapi tunaelekea," amesema.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa nchini imeendelea na msisitizo wake wa kutoitambua Sekretarieti ya uongozi wa Chamdea inayomjumuisha Katibu Mkuu wake, John Mnyika.
Sekretarieti hiyo ya Chadema iliteuliwa Januari 22, mwaka huu kwenye Baraza Kuu la chama hicho baada ya kupatikana uongozi mpya unaoongozwa na Mwenyekiti wake Taifa, Tundu Lissu.
"Mimi nimeambiwa jana niangalie sana namba zangu zinahesabika, niwaambie sitakimbia nchi hii hata dakika moja kama damu yangu itamwagika katika kutetea haki katika nchi hii imwagike tusirudi nyuma,” amedai Heche.
Mnyika
Mnyika amesema kuwa Arusha ni miongoni mwa mikoa yenye kumbukumbu mbaya ya chaguzi za viongozi mbalimbali.
Akitolea mfano amesema kuwa uchaguzi wa mwaka 2010 baada ya kuisha Chadema iliitisha mkutano kujadili utaratibu huo na watu wengi kufa kwenye maandamano.
"Mbali na hilo, mwaka 2013 kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani, baadhi ya watu walifariki na wengine kujeruhiwa vibaya kutokana na bomu lililopigwa katika viwanja vya Soweto.
"Chadema tunasema imetosha damu kumwagika kwenye chaguzi zetu ndio maana tunataka mabadiliko kwenye tume ya uchaguzi na uzuri tumetengeneza ajenda ya madai yetu" amesema.
Mnyika amesema kuwa wao kama Chadema wako tayari uchaguzi usogezwe mbele kama muda wa kufanya mabadiliko utakuwa hautoshi.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, John Heche akihutubia wakazi wa Arusha eneo la Soko Kuu jiji la Arusha.
"Na kama wanasema muda hautoshi, tuko tayari uchaguzi uhairishwe hadi mabadiliko yafanyike kuliko kufanya uchaguzi huu kinyume na mabadiliko ya katiba na sheria za uchaguzi"
Aidha Katibu Mkuu huyo ameshukuru viongozi waasisi wa chama hicho ambao walikuwa ni Wenyeviti wa chama hicho kwa nyakati tofauti ambao ni Edwin Mtei, Bob Makani na Freeman Mbowe.
Lema
Mjumbe wa Kamati ya chadema Taifa, Godbless Lema amesema kuwa operesheni yao imekuwa ikipigwa vita hadi mikutano yake ya hadhara kitendo kinachokwenda kinyume na makubaliano ya mfumo wa vyama vingi.
"Na hii ni kutokana na viongozi wote waliopo madarakani hawako huru, Kila mmoja anapigania maslahi ya chama tawala kuanzia Mkuu wa Mkoa, mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Polisi Wilaya ambao wanapata madaraka yao kwa Rais.
"Tunaposema tunataka mabadiliko ndio mambo kama haya, hatutaki kuona eti kufanya mkutano ni dhambi, tangu juzi tunayumbishwa na kuzuiwa Kila eneo," amesema.
Amewataka wananchi wa Arusha kuhakikisha hawarudi nyuma katika kampeni hiyo ya kudai mabadiliko, lakini pia kuchangia chama hicho kiweze kutekeleza shughuli zake.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Boniface Jacob amesema wakati wa uchaguzi walikuwa kwenye makundi ila baada ya uchaguzi makundi yanakufa na wote wanahamia nyuma ya aliyeshinda.
"Nimekuja kusimama hapa kama ishara ya umoja na mshikamano ndani ya chama chetu na zile propaganda kuwa wamegawanyika si wamoja, si kweli," amesema.
Dk Slaa
Katibu Mkuu wa zamani wa chama hicho, Dk Wilbroad Slaa amemtaka Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Tundu Lissu na Heche, kutokuogopa na kuwa kupitia operesheni hiyo itaweka historia mpya.
"Kuna kitabu kiliandikwa cha Tanu na raia cha mwaka 1962, Heche na Lissu mmeanzisha kitu ambacho kilitabiriwa na Mwalimu Julius Nyerere alianza na ukombozi wa kwanza.
"Nyie mnaweka historia ya ukombozi mpya msiogope katika ukombozi huu, watu wanatekwa na kuuawa… huu sasa ni wakati wa operesheni hii kuiondoa CCM madarakani," ameongeza.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) Taifa, Deogratias Mahinyila amesema watatekeleza masuala yanayohusu chama hicho kwa muda watakaoamua wao na siyo kwa maelelekezo ya msajili.
(Imeandikwa na Janeth Mushi, Filbert Rweyemamu, Bertha Ismail )