Chadema wadai kuhamishia kambi Jeshi la Polisi, latoa taarifa

Wafuasi na viongozi wa Chadema wakiwa katika makundi tofauti walipata chakula katika ofisi yao ya Chama hicho Kanda ya Nyasa walipoweka kambi kushinikiza kupatikana kwa kada na mwanaharakati wao, Mdude Nyagali
Muktasari:
- Wafuasi na viongozi wa Chadema wameendelea kuwasili zilipo Ofisi za Chama hicho Kanda ya Nyasa mtaa wa Kadege jijini Mbeya kuungana na wenzao kuweka kambi kushinikiza kupatikana kwa kada wa chama hicho, Mdude, huku wakitarajia kuhamishia zilipo Ofisi za Polisi mkoani humo.
Mbeya. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mbeya kimesema baada ya kambi ya siku tisa kwenye ofisi za chama hicho Kanda ya Nyasa kutozaa matunda, huenda wakahamia zilipo ofisi za Jeshi la Polisi wanapoamini alipo kada na mwanaharakati wa Chama hicho, Mdude Nyagali.
Mdude anadaiwa kuvamiwa na kujeruhiwa na watu wasiofahamika waliojitambulisha kuwa Askari Polisi tangu Mei 2, ambapo baada ya tukio hilo waliondoka naye ambapo hadi sasa hajulikani alipo.
Mei 3, viongozi na wafuasi wa chama hicho waliamua kuweka kambi zilipo ofisi za Kanda mtaa wa Kadege jijini Mbeya ikiwa ni njia ya kushinikiza mamlaka za serikali na vyombo vya dora kuweza kueleza alipo.

Kadri siku zinavyozidi kwenda, wafuasi na viongozi kutoka maeneo mbalimbali wameendelea kufika zilipo ofisi za Chama hicho Kanda huku Mwananchi ikishuhudia wengine wakiwasili na mizigo yenye vyakula kwa ajili ya kuungana na wenzao kambini hapo.
Hata hivyo, tayari Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limeshasema linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, huku likitoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa za mahali alipo Mdude kuwasilisha ili kufanikisha kumpata na waliohusika kwa hatua zaidi.
Taarifa nyingine iliyotolewa jana Mei 10 na Jeshi hilo, imesema halitasita kumchukulia hatua za kisheria na kumshughulikia mtu au kikundi chochote cha watu watakaojaribu kufanya uhalifu kutokana na matamko au kauli hizo zinazotolewa.
“Jeshi la Polisi likiwa linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, wamejitokeza baadhi ya watu na viongozi wa Chadema na kutoa matamko na kutaja baadhi ya majina ya Askari wakiwatuhumu kuhusika na tukio hilo bila ushahidi wowote.
“Kufuatia kauli na matamko hayo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa onyo kali kwa mtu au kikundi chochote cha watu wenye nia ovu kutojaribu wala kuthubutu kujihusisha na uhalifu wa aina yoyote ikiwemo kudhuru Askari” imesema taarifa hiyo.
Akizungumza leo Jumapili Mei 11, 2025, Katibu wa chama hicho mkoani Mbeya, Hamad Mbeyale amesema wamekaa kambi kwa siku tisa mpaka kufikia leo.
Amesema kwa sababu hawajui kinachoendelea, wafikiria kuihamisha kutoka ofisi za kanda kwenda eneo waloamini Mdude yupo.
“Leo tumefanya ibada maalumu kumkabidhi Mungu suala hili, lakini hatma yetu tunasubiri viongozi wetu wa kitaifa chini ya Naibu Katibu Mkuu Taifa, Aman Golugwa na Rais wa TLS Boniface Mwabukusi.”
“Hatuwezi kuendelea kuwaweka watu hapa kambini bila kuwa na muelekeo, kesho watakapofika viongozi wetu tutakuwa na tamko rasmi kwa kuwa na muda tulioweka wa saa 72 unaisha kesho, tutasogeza kambi huko Polisi tusaidiane kutafuta,” amesema Mbeyale.
Katibu huyo ameongeza kuwa hadi sasa hawaridhishwi na mwenendo wa uchunguzi wa suala hilo ikiwamo kutomshika mtu yeyote kwa mahojiano na kwamba hali hiyo inawapa sintofahamu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama hicho Jimbo la Mbozi mkoani Songwe, Mwarusanya Wilfred amesema kusanyiko waliloweka si sherehe bali kupigania binadamu mwenzao aweze kupatikana akiwa huru na kwamba kupitia tukio hilo, wanataka liwe la mwisho kwenye utekaji.

“Tunaamini Jeshi la Polisi ndilo linafahamu alipo Mdude, baada ya kubaini waliomshika kwa majina na makazi yao tukatangaza kufanya msako likaja tamko kututisha, hadi kufikia kufanya maombi hatujapoteza muda sisi ni binadamu” amedai Wilfred.