Chadema tukiingia Ikulu tutavunja ukuta wa Mirerani - Heche

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche (kulia) akipokea michango ya tone tone kwenye mkutano wa No Reform No Election uliofanyika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo
Muktasari:
- Ziara ya No reforms, no election ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imeingia mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara kwa chama hicho kuahidi kuvunja ukuta unaozunguka mgodi ya madini ya Tanzanite wakifanikiwa kuingia Ikulu.
Mirerani. Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche, amesema endapo chama hicho kitashinda na kuingia Ikulu, kitabomoa ukuta unaozunguka mgodi ya madini ya Tanzanite uliopo katika mji mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara.
Ukuta unaozunguka mgodi wa madini ya Tanzanite katika mji mdogo wa Mirerani, wenye urefu wa kilomita 24.5, ulijengwa katika utawala wa awamu ya tano chini ya uongozi wa hayati John Magufuli, kwa lengo la kudhibiti wizi na utoroshaji wa madini hayo. Ujenzi wa ukuta huo ulianza Novemba 1, 2017 na kukamilika Aprili 30, 2018.
Heche ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Mei 29, katika mji mdogo wa Mirerani, wakati wa ziara ya mkutano wa kampeni yao ya No reforms, no election, inayolenga kutoa elimu ya kutoshiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 pasipo kufanyika mabadiliko.
Heche amesema Chadema wakiingia Ikulu watavunja ukuta huo unaozunguka mgodi wa madini ya Tanzanite kwani hauna faida kwa watu wanaoishi eneo hilo zaidi ya kuwatesa.
"Mwaka 2018 wakati ukuta huu umemalizika kujengwa nilikuwa bungeni na rafiki yangu James Ole Milya na nikapinga ujenzi wake, kwani nilifahamu utawanyonya watu wa Mirerani," amesema Heche.
Ameeleza kwamba ukuta huo umesababisha umaskini kwa jamii inayozunguka eneo hilo hivyo hauna faida kwao, kwani huwezi kudhibiti wizi wa Tanzanite kwa kuweka ukuta.
"Hao wanaowapekua watu na kuwakagua nani anawakagua wao kama siyo ubabaishaji na wao ndiyo wanaamua nini kiingie na nini kitoke, ndiyo sababu tukiingia Ikulu tutavunja ukuta huu," amesema Heche.
Amewaomba wadau wa madini wa eneo hilo kuwaunga mkono kwenye nia yao ya bila marekebisho hakuna uchaguzi.
"Hatutaingia msituni ila tunataka saini zenu na majina yenu kwenye fomu zinazotolewa kwenye mikutano yetu kuwa mnapinga kufanyika uchaguzi ambao haufuati kanuni, taratibu wala sheria za uchaguzi," amesema Heche.
Mgombea ubunge wa Simanjiro mwaka 2020 kupitia Chadema, Emmanuel Landey amesikitishwa na kitendo cha wadau wanaoingia ndani ya ukuta huo kuambiwa wakate vitambulisho vingine na kulipia pindi wakihitaji kuingia.
"Mtu ana kitambulisho cha Taifa cha Nida, umeshamjengea ukuta, kisha unamwambia alipe fedha nyingine ili apate kitambulisho cha kuingia ndani ya ukuta huo," amesema Landey.
Amesema hatua hiyo ya kutaka watu walipie vitambulisho vipya ni kuendelea kufubaza uchumi wa wananchi wa mji mdogo wa Mirerani na kusababisha maisha kuwa magumu kwa wakazi hao.
"Hatushiriki wala kufanya uchaguzi mwaka huu na tunaposema No reforms, no election tunataka kanuni, taratibu na sheria mbovu za uchaguzi zifanyiwe marekebisho ili kuondoa makandokando ya uchaguzi," amesema Landey.
Mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, Patrick Ole Sosopi amesema mji mdogo wa Mirerani umebarikiwa utajiri mkubwa wa madini ya Tanzanite ila hauakisi maisha yao.
Ole Sosopi amesema hawashiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa sababu ya sheria kandamizi za uchaguzi ambazo zina ukakasi.
"Hatuendi kwenye uchaguzi na hatutafanya uchaguzi kwa sababu viongozi wanaopatikana wanashindwa kusimamia rasilimali zilizopo vyema," amedai Sosopi.
Mwenyeki wa Bavicha, Deogratius Mahinyila amedai hawashiriki uchaguzi kwa mwaka huu kutokana na taratibu na kanuni mbovu kutumika.
"Mimi ni wakili msomi wa mahakama kuu na mahakama nyingine za chini nchini ila niligombea nafasi ya mwenyekiti wa kijiji, wakakata jina langu wakampita mgombea wa CCM aliyeishia darasa la nne," amesema Mahinyila.