Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasomi wachambua hatua ngumu zinazoinyemelea Chadema

Dar es Salaam. Mvutano unaoendelea kati ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Chadema unaelekea kwenye hatua ngumu ambazo wadau wa siasa wanasema zinaweza kuwa na athari hasi kwa chama hicho na siasa za Tanzania kwa ujumla.

Hali hiyo inatokana na msimamo usioyumba wa kila upande, kuhusu uhalali wa uteuzi wa viongozi wanane wa Chadema waliothibitishwa na Baraza Kuu, ambalo ofisi ya msajili inasema halikukidhi akidi inayotakiwa kulingana na katiba ya chama hicho.

Ingawa Chadema mara kadhaa imefafanua kuwa akidi ya kikao hicho ilitimia kwa kuwa hakikuwa cha uchaguzi wala kubadilisha sera, ofisi ya msajili imeweka ngumu, ikikataa kuwatambua, kusimamisha ruzuku yake na kuzitaka taasisi za serikali kutokutoa ushirikiano kwa viongozi husika.

Vilevile, Ofisi ya Msajili imetishia kuwa endapo Chadema kitaendelea kuwatambua wanachama hao kuwa ni viongozi wa chama hicho, kifungu cha 19 cha Sheria ya Vyama vya Siasa kinaipa mamlaka ya kusimamisha usajili wa chama hicho.

Hatua hiyo ndiyo inayowaibua wachambuzi hao wa siasa wakisema hali hiyo, endapo itaendelea bila muafaka wa pamoja, inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa mwelekeo wa demokrasia na taswira ya ushindani wa kisiasa nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa wachambuzi hao, msimamo mkali wa kila upande – Msajili akisisitiza kufuatwa maagizo yake na Chadema ikisisitiza uhuru wake wa ndani katika kuendesha shughuli za chama, unaweza kuchochea sintofahamu zaidi katika uhusiano kati ya vyombo vya dola na vyama vya upinzani nchini.

Ingawa Katiba ya nchi inatambua uhuru wa vyama vya siasa, kwa miaka kadhaa kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya vyama vya upinzani kuhusu kile kinachoelezwa kuwa ni kuingiliwa kwa shughuli zao za ndani na vyombo vya Serikali, hasa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Katika mazingira hayo, mivutano ya mara kwa mara kati ya Chadema au vyama vingine vikubwa vya upinzani na Ofisi ya Msajili si jambo jipya, lakini mwelekeo wa sasa unatajwa kuwa na uzito zaidi kutokana na mazingira ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Chadema inaendelea na kampeni yake ya ‘No reforms no election’ ikilenga kushinikiza mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi, ili kuweka uwanja sawa wa ushindani.

Kutokana na hali hiyo, wachambuzi wa siasa wanasisitiza umuhimu wa mazungumzo ya wazi na ya kisheria kati ya pande husika, ili kulinda misingi ya demokrasia na utawala wa sheria nchini.

Hata hivyo, licha ya hatua kali zilizofikiwa na zinazotarajiwa kufikiwa na ofisi ya Msajili, Makamu Mwenyekiti - Bara wa Chadema, John Heche ameedelea kusisitiza msimamo wa chama hicho, wa kutokubaliana na uamuzi wa Msajili.

“Msajili anatishia kufuta chama kinyume na utaratibu wa sheria anataka kuiua Chadema kinyume na sheria na kuwa maamuzi ya Kamati Kuu yalisema barua ya msajili ni batili. Na tumeendelea kuwatambua viongozi wetu tuliowateua kwenye Baraza Kuu,” amesema Heche kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja wa Soko Kuu la Arusha.

Hata hivyo, amesema wameitisha Kamati Kuu tena Juni 3, kujadili barua ya sasa ya msajili na watatoa mwelekeo wa nchi ni wapi wanaelekea.

Mara ya kwanza Heche kutoa kauli ya kumtalia Msajili ilikuwa Mei 25, 2025 alipokuwa akitoa maamuzi ya kikao cha Kamati Kuu, aliposema chama hicho hakitaipa uzito barua ya Msajili iliyowataka kuitisha upya Baraza Kuu kuwaidhinisha viongozi wanane walioteuliwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, Januari 22, 2025.

Heche alibainisha kuwa Kamati Kuu iliyokutana Jumamosi Mei 24, 2025, ilifikia uamuzi wa pamoja wa kutokujibu barua ya Msajili, ikisisitiza kuwa msimamo wa ofisi hiyo ni batili na haupaswi kufanyiwa kazi.


Viya ya wengi

Kufuatia msimamo huo, msomi wa sayansi ya siasa, Dk Faraja Kristomus amesema ikifika hatua hiyo anaona vita haitakuwa tena kati ya Chadema na msajili wa vyama pelee, bali kutakuwa na mgogoro kati ya ofisi hiyo na Watanzani, wafuasi wa Chadema na hali hiyo itavuruga hali ya kisiasa.

“Kwa jinsi hali ilivyo, hata kwa mtu wa kawaida ataona kuwa kuna nguvu fulani …ukizingatia mtiririko mzima wa matukio ndani ya Chadema.

“Jinsi mambo yalivyotokea kabla na baada ya uchaguzi na baadhi ya wanachama wa Chadema ambao hawakuridhika na kushindwa kwa Mbowe, walitishia na kutabiri kuwa Chadema itafutwa na Msajili.

 “Hii itadhihirisha kuwa mvutano wao wa ndani ndio unaozaa haya matatizo, wanachoweza kukifanya Chadema ni kuamua kufunika kombe mwanaharamu apite, kwa kuitisha kikao cha Baraza Kuu la kukamilisha mchakato kwa mujibu wa taratibu zilizolamikiwa na Mchome (Lembrus), lakini bado swali la kujiuliza, haya yote yatatakiwa kufanyika kwa masilahi ya nani? amehoji Dk Kristomus.

Mwingine aliyezungumzia hali hiyo ni Dk George Kahangwa, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), aliyesema hali inayoikuta Chadema hivi sasa ni ngumu na inaonyesha wazi kuna shida kwenye uhai wa demokrasia Tanzania.

“Taasisi tulizonazo za vyama vya siasa na ofisi inayosimamia vyama vyenyewe zinafanya vitu vya kushangaza, ambavyo matokeo yake ni kuhujumu uhai wa demokrasia ya nchi, iliyoanza kustawi na kuanza kuleta manufaa,” amesema Dk Kahangwa.

Dk Kahangwa amesema yote yanayojitokeza anayepata hasara ni Mtanzania katika jambo jema linaloitwa demokrasia ya kweli, na ijulikane vyama vya siasa ni vitalu vya kuzalisha viongozi wa nchi.

 “Kitalu cha kuzalisha viongozi kinapohujumiwa au kukwamishwa, tafsiri yake Taifa linanyimwa fursa ya kupata viongozi wazuri, tutaishia kupata miche ya miti mibovu badala ya kuweka miche mizuri ili tupate miti mizuri ya kuliendesha taifa hili,” amesema.

Amefafanua kuwa wadau wanapotafakari uamuzi wa Msajili dhidi ya Chadema, kuna mambo mengi ya kujiuliza ni kwa nini sasa katika mazingira ya kuelekea uchaguzi mkuu.

 “Tukiwa ndani ya mwaka wa uchaguzi mkuu chama kikuu cha upinzani kwa muda mrefu kinapata mapigo mfululizo ndani ya majira haya, unaweza kusema si bure lazima kuna namna,” amesema.

Hata hivyo,  Dk Kahangwa, amesema kinachoikuta Chadema si jambo geni kwani kulikuwa na vyama viliwahi kukutana na dhoruba kama hiyo, vikiwemo vya CUF na NCCR- Mageuzi  na mwisho wa siku vilipasuliwa na kuzalisha vyama vingine.

Wakati Dk Kahangwa akieleza hayo, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu kupitia mtandao wa kijamii wa X ameandika:

 “Mwaka 2019, Maalim Seif (Sharif Hamad-marehemu) alipojiunga na ACT Wazalendo, Msajili wa Vyama vya Siasa alikataa uteuzi wake na viongozi wengine kushikilia nafasi mbalimbali ndani ya ACT Wazalendo kwa hoja kwamba hawakuteuliwa na halmashauri kuu.

 “Hatukukubaliana na hoja zake. Lakini, tuliamua kuimaliza mechi hiyo ‘kibingwa’. Tuliitisha kikao cha halmashauri kuu upesi na kuwateua watu walewale aliowakataa na mchezo uliishia hapo,”ameandika Ado.

Kwa upande wake Profesa Mohamed Bakari, mwanazuoni wa UDMS, amesema uamuzi wa Msajili si taarifa njema kwa Chadema, iwe Msajili amefanya uamuzi kwa mujibu wa sheria au kwa utashi wa kisiasa.

 “Chadema namna sahihi ya kupambana na hilo lazima wajue Msajili ameshika mpini na wap wamekamata kwenye makali,” amesema.

Profesa Bakari amesema kwa sababu Chadema ina migogoro mingi ya ndani, ilikuwa busara chama hicho kufuata utaratibu walioelekezwa wa kuitisha upya Baraza Kuu kuwathibitisha viongozi wanaolalamikiwa.

 “Hata Chadema wakiamua kwenda mahakamani kupinga uamuzi wa Msajili yatakuwa ni yaleyale, kesi itachukua muda mrefu na wataathirika zaidi kukosa hiyo ruzuku,” amesema.

Amesema kama Msajili anataka viongozi hao wasipewe ushirikiano, tafsiri yake hawatakuwa na uhalali hata kuitisha mikutano au kukusanya wanachama, na mambo mengi yanaweza kukwamishwa kisa uongozi wao kutotambuliwa na mlezi wa vyama vya siasa.

Kuhusu kusitisha ruzuku, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo amesema Msajili ana mamlaka hayo si tu kwa sababu wamekaidi kutekeleza maagizo yake, bali kwa sababu yeyote ile anayoiona yeye kwa mujibu wa sheria.

 “Kwa utaratibu wa fedha, kama hakuna katibu mkuu basi hupaswi kupeleka fedha za umma,” amesema Dk Masabo.

Hata hivyo, Dk Masabo amesema suala la ruzuku haina shida, lakini kusema taasisi za umma na binafsi zisiwapatie ushirikiano lina shida zaidi, swali linakuja je, Msajili hakitambui chama hicho?

 “Iwapo anakitambua kama chama halali kwa nini azuie taasisi zingine zisiitambue? ilitakiwa aulizwe, basi kama hakitambui basi ana uwezo wa kukifuta,” amesema.


Viongozi wanaolalamikiwa

Katibu Mkuu, John Mnyika, Amani Golugwa (Naibu Katibu Mkuu - Bara) na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu - Zanzibar).

Wengine ni wajumbe wa kamati huu, Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh pamoja na Dk Rugemeleza Nshala, ambaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi  wa Sheria wa chama hicho.