Prime
CCM: Uteuzi wa Dk Nchimbi haulengi urais 2030

Muktasari:
- Hatua ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumpitisha Dk Emmanue Nchimbi kuwa mgombea mwenza wa urais, imetajwa kuwa si mbinu ya kumuandaa kwa mbio za urais mwaka 2030.
Dar es Salaam. Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla amesema uamuzi wa chama hicho kumpitisha Katibu Mkuu wake, Dk Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza wa urais, haulengi kumtengenezea nafasi ya kugombea urais katika uchaguzi wa 2030.
Msingi wa ufafanuzi wa Makalla ni mitazamo iliyoibuka baada ya Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho, kumpitisha Dk Nchimbi kuwa mgombea mwenza wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Dk Nchimbi alipitishwa Januari 18, katika mkutano mkuu maalumu wa CCM, ambao pia ulimpitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano, huku Dk Hussein Mwinyi kugombea nafasi hiyo visiwani Zanzibar.
Uamuzi huo kwanza, umetafsiriwa kuwa wa haraka zaidi kuwahi kufanywa na chama hicho tawala, lakini umeshtua wengi kwa kuwa Dk Nchimbi hakuwa miongoni mwa wanaotarajiwa kuteuliwa katika mbio hizo.
Mazingira hayo ndiyo yaliyoibua mitazamo kuwa, pengine anaandaliwa kwa mbio za urais wa mwaka 2030, huku mmoja wa makada wa chama hicho, Dk Godfrey Malisa akiibuka hadharani kupinga kupitishwa kwa wagombea hao na hatimaye akafukuzwa uanachama.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla (katikati) akifanya mahojiano maalumu na wahariri wa Gazeti la Mwananchi, alipotembelea Mwananchi Communications Ltd (MCL), leo. Picha na Sunday George
Makalla ametoa ufafanuzi huo leo, Ijumaa Februari 21, 2025 alipofanya mahojiano maalumu na wahariri na waandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL), Tabata Relini jijini Dar es Salam.
Kwa wanaohisi Dk Nchimbi amepitishwa kwa sababu anaandaliwa kugombea urais mwaka 2030, Makalla amesema wanapaswa kufahamu kilichofanyika kimezingatia Katiba ya CCM inayosema iwapo mgombea urais atatoka Zanzibar, mgombea mwenza lazima atokee Bara.
“Kuna shida gani ya mgombea mwenza aliyeteuwa, moja anatoka bara, Mjumbe wa Kamati Kuu, amekuwa Mwenyekiti wa vijana kwa awamu mbili na sasa ni Katibu Mkuu wa CCM, amekuwa Waziri, Mbunge. Kwa sifa za kuwa Makamu wa Rais au mgombea mwenza, hakuna mtu anayepinga,” amesema Makalla.
Amesema hisia kuhusu kuandaliwa urais, angalau zingekuwa na mashiko, iwapo Dk Nchimbi angelikuwa na historia ya kuwahi kutia nia au kuomba ridhaa ya nafasi ya urais.
“Nchimbi aliwahi kuchukua fomu ya urais? Maana angemteuwa Mwigulu (Dk Nchemba-Waziri wa Fedha) kwa mfano, si aliwahi kuchukua fomu ya urais au Januari (Makamba-Mbunge wa Mombuli) si aliwahi kuchukua fomu ya urais?
“Je, Nchimbi aliwahi kuchukua fomu ya urais? Aliwahi kutangaza popote? kwa hiyo hisia. Hajawahi Nchimbi kuomba, kutangaza wala kudiriki kuchukua fomu,” amesema.
Ameeleza wapo makada waliowahi kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya urais na iwapo mmoja wapo angeteuliwa, angalau kungekuwa na sababu ya kuhisi kuwa anaandaliwa kwa mbio za urais wa mwaka 2030.
Ameambatanisha ufafanuzi huo na pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan, akisema amemteuwa mtu ambaye hakuwahi kugombea nafasi ya urais.
“Hayo mengine yanayoendelea ni hisia ambazo unajijengea mwenyewe, unatengeneza hofu mwenyewe. Unamtengenezea mtu kwamba huyu ndio anakwenda kugombea urais wakati hajawahi kusema mahali popote, hayo ya 2030 yanatoka wapi,” amehoji Makalla.
Kuhusu Malisa
Katika maelezo yake, amemtaja Dk Malisa kuwa mwanachama mchanga ndani ya chama hicho na hivyo pengine hajafahamu vema taratibu za CCM.

Makalla amesema Dk Malisa alipotamka kupinga uamuzi wa mkutano mkuu maalumu, aliitwa na uongozi wa chama hicho ngazi ya tawi lake kuelezwa kosa la kikatiba analolifanya.
“Kwanza kuna utamaduni uliojengeka kwamba Rais anayepatikana wa CCM atakwenda awamu ya pili, haijaandikwa kwenye katiba lakini ni utamaduni. Imeshafanyika hivyo na isipofanyika litakuwa jambo la ajabu.
“Ni wazi Rais Samia na Dk Mwinyi wanatakiwa kuendelea na kipindi cha pili kwa taratibu za CCM. Kwa hiyo Dk Malisa anaonekana alikuwa anajifunza kwa sababu alitokea kwenye chama kingine,” amesema.
Kwa mujibu wa Makalla, uamuzi wa Dk Malisa kufukuzwa uanachama ulianzia tawini, akapelekwa kwenye Kata, wilayani na hatimaye Kamati ya Siasa ya Mkoa na Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Kilimanjaro ikaamua kumfuta uanachama.
Hata hivyo, amesema ni muda wa Dk Malisa kuonyesha kujutia kosa na kuomba tena uanachama kwa kuwa CCM inatoa nafasi hiyo baada ya kumweka kwenye uangalizi.
“Unajua mkutano mkuu ni mkutano mkubwa mno, sasa Dk Malisa yuko Moshi kule mkutano mkuu unafanyika sisi wenyewe tunauogopa, yeye anatamka tu kule, ndio haki za mwanachama?” amehoji.
Mzizi wa yote ni hatua ya Dk Malisa kudai CCM imekiuka Katiba yake kwa hatua ya kumpitisha Rais Samia kuwa mgombea pekee wa urais bila kutoa nafasi kwa wanachama wengine kuomba nafasi hiyo.
Februari 10, mwaka huu Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Kilimanjaro ilimfuta uanachama kwa hatua hiyo, ikisema ametenda kosa la kukiuka katiba na maadili ya chama hicho.
Hakuishia hapo, Dk Malisa ameendelea na sasa amemwandikia barua Rais Samia kumweleza kusudio lake la kwenda mahakamani kupinga uamuzi wa mkutano huo mkuu.
Rushwa
Makalla pia ameeleza katika uchaguzi huu chama hicho imeendelea kuhakikisha suala la rushwa linadhibitiwa na imeanza kwa kuongeza idadi ya wajumbe wanaopitisha wagombea wa ubunge na udiwani.

“Kama ulikuwa umejipanga na watu 1,200 sasa utakutana na watu 25,000. Yote hiyo kudhibiti rushwa lakini kuongeza demokrasia ya watu kushiriki katika kuwapata wagombea,” amesema.
Pia, amesema kwa sasa chama hicho kimedhibiti mipango ya wagombea ubunge kujitengenezea nafasi za kupita bila kupingwa, sambamba na matukio mbalimbali ya kujinadi.
“Sisi tumetamka tunaamisha na Mwenyekiti (Rais Samia) amesisitiza tutakuwa makini. Sisi ndio watekelezaji, tuwahakikishie matamko haya ya Mwenyekiti na Katibu Mkuu hayawezi kupita hivi hivi tutayatekeleza,” amesema.