Prime
‘Birthday’, vifo na ndoa vinavyotumika kusaka uteuzi wa udiwani, ubunge CCM

Muktasari:
- “Mtu anasema kumbukumbu ya marehemu bibi yake aliyefariki dunia mwaka 1970 anaalika wajumbe 3,000 na kwenye kumbukumbu ya mama yake anatoa na posho.”
Dodoma/Dar. Joto la uchaguzi mkuu linazidi kupanda na kuwafanya wanasiasa kuwa wabunifu katika kuhakikisha wanapata nafasi za uteuzi. Ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mambo yamezidi kupamba moto wakati ikiwa imesalia miezi takribani saba kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika baadaye mwaka huu. Kinachoendelea kwa sasa ndani ya chama hicho ni uwepo wa makada wakiwemo wabunge, madiwani na wale wanaosaka nafasi hizo, kutumia mbinu mbadala kusaka fursa za kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu.
Mbinu hizo zimemfanya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amewaonya makada wa chama hicho kuhusu mbinu hizo mpya zinazotumika kusaka nafasi hizo, akisema watakatwa tu.
Mbinu zilizotajwa kutumiwa na makada hao ni kufanya matukio ya sherehe za kumbukizi ya siku za kuzaliwa, vifo vya ndugu, jamaa na marafiki pamoja na kumbukumbu za ndoa, ambapo hutumia mwanya huo kugawa fedha na vifaa kwa waalikwa.
Pia, wapo wengine wameanzisha mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s), wakizitumika kama sehemu za mikakati ya kuwafikia wajumbe huku lengo likiwa ni kuutaka ubunge au udiwani.
Mbali na Dk Nchimbi, mwingine aliyewahi kuonya ni Rais Samia Suluhu Hassan, akisema kujipigia kampeni kabla ya wakati, ni kinyume na kanuni za chama hicho.
“Tunakemea kampeni zinazoanza mapema kabla ya wakati. Tumeshapokea malalamiko na ushahidi wa picha za watu wanaofanya misafara kwenda majimboni, wanaitisha mikutano ya jimbo kwa kigezo cha ufungaji ila malengo yao ni kujitambulisha kwa wanachana. Nawaonya wote wenye tabia hii kuacha mara moja,” amesema Rais Samia alipohutubia Mkutano Mkuu wa CCM, Dodoma uliofanyika Januari 18, 2025.
Hayo yanajitokeza kipindi ambacho zimebakia miezi michache kabla ya Bunge la 12 kuvunjwa kuruhusu mchakato za uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na urais.
Kwa mujibu ya ratiba iliyotolewa na Bunge, Juni 27, 2025, Rais Samia atalihutubia na kulivunja. Lakini, wakati hilo likisubiliwa fukuto la uchaguzi limetanda maeneo mbalimbali nchini kwa kila mmoja kujiunga kuwania nafasi hizo za ubunge na udiwani.
Katikati ya hayo, Dk Nchimbi leo Jumatano, Februari 19, 2025 alipohutubia mkutano wa makatibu wa kata na matawi wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini, ametumia fursa hiyo kutoa onyo.
“Mtu anasema kumbukumbu ya marehemu bibi yake aliyefariki dunia mwaka 1970 anaalika wajumbe 3,000 na kwenye kumbukumbu ya mama yake anatoa na posho,” amesema Dk Nchimbi na kuongeza: “Wapo wengine wanasema birthday (kumbukumbu ya kuzaliwa) anaalika watu 900 anatoa na posho na waalikwa wote wamevaa sare za CCM. Sasa hapa imezaliwa CCM umezaliwa wewe.”
Katika hotuba yake hiyo, ametolea mfano tukio alilodai limetoa hivi karibuni la kada aliyefanya tukio la kumbukumbu ya miaka tisa ya ndoa yake, ilhali ana miaka mitatu tu tangu afunge ndoa.
“Nataka wajue kuwa CCM ina mfumo wa kufuatilia kila kinachotokea. Nataka wajue kuwa tunachukua kumbukumbu ya matukio wanayoyafanya. Na kumbukumbu hizo ndizo zitakazowafanya waje washangae kitakachotokea. Kwa sababu kwa hakika tutaengua majina yao.
“Labda kama wana hamu ya kutumia fedha zao kama sadaka ya kugawa na hawahitaji chochote katika chama chetu waendelee tu, tunawatakia heri lakini kama wanataka tugombee na visingizio vya kuzaliwa na kumbukumbu marehemu bibi na ndoa waendelee tunawafuatilia,” amesema.
Dk Nchimbi ameonya pia na watu ambao waliotengeneza mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), wanaozunguka kwenye maeneo mbalimbali na kurubuni wajumbe kwa rushwa.
“NGOs inafanya hamasa na kutoa posho, tunawafuatilia waendelee tu. Tunafurahi sana mnatoa posho kwa viongozi wetu, lakini hiyo posho haitakuwa kisingizio cha kukuteua wewe kuwa kiongozi ama kupeperusha bendera,” amesema.
Amesema uzoefu unaonyesha wanaogawa fedha kirahisi, aghalabu zinatokana na kuwaibia wananchi hivyo, wakiwarudishia haitakuwa tatizo.
Aidha, Dk Nchimbi amesema yapo matukio ambayo yanaondoka katika dhamira nzuri ya mkutano mkuu wa CCM na vikao ambavyo vimefanya mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi.
“Nadhani kupitia vyombo vya habari mmeanza kuona baadhi ya wabunge wanapitisha fomu eti za wanachama kujiorodhesha kutaka apitishwe kuwa mgombea pekee. Hiyo kitu haipo, natuma salamu kwa wanaofanya hivyo kuwa wanapoteza muda wao bure.
“Wanachofanya ni kutulazimisha tufikirie kutengua majina yao. Kwa hiyo nasema watu wote walioanza kupitisha fomu kwa wanachama na viongozi kutaka wapitishwe kama wagombea pekee waache mara moja mchezo huo,” amesema.
Dk Nchimbi amesema vimeanza vikao vya matamko vya mikutano mikuu, halmashauri kuu, mikutano ya wanachama kuwa baada ya utekelezaji mzuri wa mbunge wao au diwani apite bila kupingwa.
“Nawatumia salamu kuwa hakuna hiyo kitu, wanachama wote watagombea na kadri utakavyohamasisha matamko katika maeneo hayo ndivyo ambavyo tutakuengua kirahisi zaidi,” amesema.
Mbali na hilo, Dk Nchimbi ambaye ni mgombea mwenza wa Urais, amesema wapo walioanza kampeni chafu za kuwatoa majimboni wabunge na madiwani waliopo kwa sasa.
“Kuna watu wanatengeneza fulana, mtu anapeleka fulana 3,000, zimeandikwa tokomeza (jina la mtu) Mpanda, sasa wewe ni mwana-CCM, unamchafua mwenzako, kwani yeye ni ukimwi,” amehoji.
Sababu za mabadiliko ya Katiba
Dk Nchimbi amesema ushindi wa chama hicho unategemea aina ya wagombea wanaopatikana katika uchaguzi husika.
“Lazima chama kifanye jitihada zote za kupata wagombea wenye sifa, watakaoweza kutimiza majukumu yao, lakini vile vile wanaochagulika, wanaokubalika na jamii. Wasiokuwa na kando katika jamii ambao jamii inawaamini wanaweza kuongoza katika nchi yetu,” amesema.
Amesema ndio maana katika mkutano mkuu walifanya mabadiliko makubwa ya kupata wagombea wao katika chaguzi mbalimbali.
Amesema katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2000 ni mikutano mikuu katika kata na ngazi ya wilaya ndiyo, iliyochagua wagombea ubunge na udiwani lakini mkutano mkuu wa Taifa, umefanya mabadiliko ya kuongeza idadi ya wapiga kura katika mikutano ya kata na wilaya.
“Wameongeza mabalozi, kamati za uongozi la ubalozi, kamati za siasa ngazi ya tawi na kata, kamati za utekelezaji za jumuiya zetu. Sasa idadi ya wapiga kura katika kila eneo la nchi yetu limeongezeka kwa asilimia 900,” amesema.
Dk Nchimbi amesema sababu za kuongeza idadi ya wapiga kura ni kutaka wanachama wa chama hicho kuwa wawakilishi wa wananchi lengo likiwa ni kupata mawazo ya wananchi kuhusu wagombea wanaowataka.
“Mkija kutuambia kuwa sisi huyu tumemkubali tunajua kuwa haya ni maoni ya wananchi wa kawaida kwamba huyu ndiye wanayemtaka, uwakilishi ni mkubwa zaidi. Unatoa nafasi ya watu wengi zaidi kusema kuwa huyu ndiye tunayemkubali,” amesema.
Pia, CCM imeongeza wapiga kura ili kupunguza mbembwe za rushwa na kuwa kwa bahati mbaya walikuwa na watu waliokuwa wakihesabu wajumbe wanaopiga kura.
“Wakimaliza kuchaguliwa anasema kuwa waliopiga kura 700, sifanyi kazi yoyote kwenye jimbo kwa miaka mitano, natunza hela ili utakapofika uchaguzi mwingine nitawapatia 50,000 watanichagua tena. Majambazi hayo yalikuwepo ndani ya chama chetu,” amesema na kuongeza: “Mkutano Mkuu wa CCM Taifa uliongozwa na Mwenyekiti wetu, Rais Samia Suluhu tabia hiyo haiwezi kuendelea kuendekezwa. Ukichaguliwa kafanye kazi ili upimwe kwa kazi ulioifanya, upimwe kwa maendeleo uliyoleta, hatuwezi kukupima kwa kiwango cha kutoa rushwa.
“Kwamba wewe ndiye, kiongozi bora kwa sababu unaweza kutuhesabu na kujua utatugawia shilingi ngapi ngapi? Tunaamini sana katika mabadiliko hayo yaliyofanyika rushwa katika mfumo wa kupata wagombea wa CCM, rushwa itapata jeraha la kudumu.”
Akimkaribisha Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Oganaizesheni, Issa Gavu amesema mafunzo hayo ni mwendelezo wa maelekezo Rais Samia chini ya usimamizi wa Dk Nchimbi.
“Makatibu na wenyeviti wa mikoa na makatibu na wenyeviti wa wilaya walishafanyiwa mafunzo haya.Kwa nini tunaanza mafunzo haya ni kwa sababu tunaamini chama chetu kimeanza katika shina hadi Taifani,” amesema.
Nje ya ukumbi huo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Dodoma, Halima Zuberi alipogeza chama chake kwa kurejesha dhamana kwa wanachama.
Mtazamo wa wadau
Akizungumzia hilo, Mwanazuoni kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (Tudarco), Dk Lazaro Swai amesema katika uwanja wa siasa kunahitaji jukwaa.
Amesema jukwaa hilo, aghalabu linatengenezwa kwa namna mbalimbali na nyakati tofauti na ndilo linalowezesha mwanasiasa kujulikana.
Dk Swai amesema ni kawaida mwanasiasa kutengeneza jukwaa la kujulikana, lakini anapaswa kuzingatia sheria na kanuni za chama chake wakati wa kufanya hivyo.
“Kama kuna katazo hupaswi kufanya kwa sababu unatakiwa uzingatie misingi ya katazo. Uking’ang’ania utakatwa kweli,” amesema.
Hata mbinu za kutafuta jukwaa la kujulikana, amesema hazipaswi kuhusisha vitendo vya rushwa kwa kuwa ni kosa kisheria.
Mchambuzi wa Sayansi ya Siasa, Majjid Said amesema hatari ya kujipitisha ni kutengeneza uadui ndani ya vyama, kadhalika mianya ya rushwa.
Amesema ikiruhusiwa kila mwanasiasa ajipitishe, kitakachotamba ni nguvu ya fedha na sio mapenzi ya wananchi.
Katika hatua hiyo, ameeleza ile hali ya wananchi kuchagua kiongozi kwa sifa haitakuwepo, badala yake watachagua kwa kuangalia nani amewapa fedha nyingi.
“Kwa sababu mwanasiasa ni vigumu kukwepa kuonyesha nia yako ya kugombea, ni vema ukatafuta njia sahihi za kuonyesha sio kutengeneza matukio yenye tafsiri mbaya kwako,” amesema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Dk Ponsian Ntui alisema wala CCM haipaswi kutumia nguvu kubwa kuliongelea hilo kwa kuwa wanazo taratibu, kanuni zinazowaongoza katika chaguzi zao ambazo wanatakiwa kuzitumia.
“Kama mnawajua na mnawaona wanafanya halafu mnakuja kutoka kwenye vyombo vya habari ama kwenye majukwaa unasema hiyo kwa tafsiri nyingine kwamba, hamna nia ya kutekeleza hilo au pengine hamna uwezo wa kulifanya hilo,” amesema.
Dk Ntui alisema miaka yote ya uchaguzi, wamewaona viongozi wakilikemea jambo hilo lakini huko mitaani wapo baadhi hutumwa na viongozi kuanza kampeni mapema.
“Mwaka 2020 katika uchaguzi mkuu wapo watu waliambiwa wakitoa rushwa watakatwa, lakini kwa maneno ya watu waliogombea wapo watu wanasemekana walihonga wajumbe na walipita na hawakufanyiwa lolote,” amehoji Dk Ntui.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie amesema uchaguzi una ushindani ni lazima atafute mbinu ya kujulikana na kujitangaza na ndio sababu ya matukio hayo.
“Siku hizi uchaguzi umekuwa kama biashara, yenye mauzo, bidhaa inayouzwa kwenye hii biashara ni kura, hivyo inanunuliwa na kuuzwa. Hii kura ni ya mtu na ili upate kura hiyo ni lazima umshawishi,” amesema.
Alisema jambo la muhimu ni kauli ya Dk Nchimbi kufanyiwa kazi na isiishie kwenye kutamka na kuwa ikiishia katika kutamka haitakuwa na maana yoyote.
Dk Loisulie amesema kauli zinapaswa kuendana na matendo na sio kusubiri hadi siku ya mchujo bali kuwepo kwa mkakati wa kuanzia sasa na kuendelea.