Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCM, Chadema watakavyomkumbuka Mzee Msuya

Muktasari:

  • Jana Jumatano, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alitangaza kifo cha aliyewahi kuwa Makamu wa kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya (94) kilichotokea saa 3 asubuhi katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) vimeomboleza kifo cha aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa David Msuya (94).

CCM kimesema Mzee Msuya ni miongoni mwa makada wake waliolitumikia Taifa kwa moyo wa dhati, uadilifu na uzalendo usiotetereka.

Chadema chenyewe kimesema: “Tutamkumbuka Mzee Msuya kwa utumishi wake uliotukuka kwa Taifa letu. Tutaendelea kuenzi na kuthamini mchango wake mkubwa katika ujenzi wa Taifa.”

Mzee Msuya alifariki dunia saa 3 asubuhi ya jana Jumatano, Mei 7, 2025 katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya moyo aliyokuwa nayo kwa kipindi kirefu na kupata matibabu ndani na nje ya nchi.

Rais Samia Suluhu Hassan aliyetangaza kifo hicho, amesema Taifa litaomboleza kwa siku saba kuanzia jana Mei 7-13, 2025 ambapo bendera ya Taifa itapepea nusu mlingoti huku akisema taarifa zaidi za msiba zitatolewa.

Baada ya taarifa hiyo, CCM kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Dk Emmanuel Nchimbi na Chadema kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia walitoa taarifa kwa umma za kuomboleza kifo hicho.

“Mzee Msuya alikuwa miongoni mwa makada na viongozi waliotumikia chama, taifa letu na nchi yetu, kupitia nafasi alizoaminiwa kwa kuchaguliwa na kuteuliwa, kwa moyo wa dhati, uadilifu wa hali ya juu, na uzalendo usiotetereka,” amesema Balozi Nchimbi.

Amesema Msuya liaminiwa kushika dhamana mbalimbali za uongozi katika chama na Serikali, ikiwa ni pamoja na kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Katika nyadhifa hizo, alionesha uongozi uliotukuka, uliosheheni busara, hekima na kuzingatia maslahi ya wananchi,” amesema Balozi Nchimbi.

Kulingana na Dk Nchimbi amesema kwa niaba ya chama hicho: “Ninatoa pole nyingi kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na Watanzania wote walioguswa na msiba huu mkubwa kwa taifa letu.”

“Kwa namna ya kipekee, tunaungana na Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania, Samia, katika kipindi hiki cha maombolezo ya siku saba alizotangaza kwa heshima ya maisha na mchango mkubwa wa Mzee Msuya kwa taifa letu,” amesema Balozi Nchimbi.

Balozi Nchimbi amesema Msuya ataendelea kukumbukwa kuwa kama kiongozi aliyeacha alama ya kudumu katika historia ya Tanzania na CCM.

Taarifa ya Chadema ilitolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia alisema pamoja na mambo mengine: “Tutakumbuka pia kauli yake maarufu ndani ya chama chetu ‘Chadema ni wachambuzi wa mambo’ –kauli iliyobeba heshima na kutambua nafasi ya chama katika mjadala wa kitaifa.”