Buriani Edward Ngoyai Lowassa

Dunia imetingishika kwa kuondokewa na mwanasiasa mahiri, Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa wiki hii. Mama nakupa pole kutoka mtimani mwangu kwa jinsi ulivyopokea taarifa za umauti wake kwa mshituko mkubwa. Nazidi kumwomba Mwenyezi Mungu ailaze mahali pema peponi roho yake, aipe nguvu familia yake na kuwafariji viongozi wote mlioguswa na msiba huu.
Ukiachilia mbali umahiri wake kwenye siasa, Lowassa alikuwa kiongozi wa kipekee sana Tanzania, Afrika na duniani kiujumla. Uchapakazi wake ulikuwa mfano wa kuigwa na wengi, ufuatiliaji makini wa miradi, uzalendo pamoja na kuepuka tabia ya kuwalea watumishi wabovu, pamoja na uwajibishaji wa watendaji wazembe vilimjengea sifa machoni mwa umma. Unyoofu wake katika siasa za Tanzania ulifananishwa na waziri mkuu wa zamani wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine.
Alikuwa miongoni mwa mawaziri waliopachikwa jina la "Askari wa Mwavuli” na Rais Benjamin Mkapa. Hata hivyo alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza kujiuzulu kwa kashfa nchini Tanzania. Kwa miaka mingi baadaye aliandamwa na tuhuma za rushwa na ufisadi alizozikanusha, lakini hakuchoka kuonesha ukomavu wake kisiasa kwa kutoropoka wala kubishana. Hii ilimzidishia heshima kisiasa.
Kikubwa tunachojifunza na tutakachokikumbuka zaidi kutoka kwa nguli huyu ni uzalendo na msimamo usiopinda. Hakuwa mwoga kuachia nafasi kubwa kama aliyokuwa nayo kwa maslahi ya Taifa. Lakini pia tunakumbuka utendaji wake ulionyooka katika ngazi zote alizowahi kupitia.
Katika safari yake ya siasa aliwahi kuteuliwa mara mbili kuwa waziri kwenye Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi. Nyota yake iling’aa zaidi alipoteuliwa kuwa Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000. Hapa Lowassa aliingia kwenye fani yake, maana baba yake alikuwa mfugaji, naye alimrithi kwenye kazi hiyo.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 ulifungua pazia lingine kwa Lowassa wakati Jakaya Mrisho Kikwete, mwanasiasa aliyetajwa kuwa karibu na Lowasa alipochaguliwa kuwa rais wa Tanzania. Ikaibuka imani kwamba Lowassa angekuwa waziri mkuu wa nane, na jina lake lilipotajwa bungeni mnamo Desemba 29, 2005, lilipokewa kwa shangwe na kuidhinishwa kwa wingi mkubwa wa kura.
Chini ya kaulimbiu ya uchaguzi ya "ari mpya, nguvu mpya, kasi mpya”, Lowassa aliingia madarakani akibeba matumaini ya Watanzania wengi. Kauli na hatua zake zilizonyooka zilidhihirisha kuwa taifa limepata kiongozi aliye tayari kulifanyia mageuzi. Lakini yote hayo hayakudumu zaidi ya miaka miwili, kwani Watanzania walipokea kwa mshtuko tuhuma za kiongozi wao aliyekuwa taswira ya matumaini na utumishi bora.
Kashfa ya Richmond ilibomoa sifa za Lowassa. Alituhumiwa kutumia nafasi yake kurefusha mkataba wa kampuni hewa ya Richmond iliyopewa kandarasi ya kufua umeme. Kamati ya bunge iliyofanya uchunguzi wa kashfa hiyo, ilisema Lowassa alipuuza ushauri wa Shirika la Umeme la Taifa, Tanesco na kushinikiza kurefushwa mkataba wa Richmond. Uamuzi huo ulilisababishia taifa hasara ya mabilioni ya shilingi.
Ilikuwa ni kashfa ya kipekee iliyolitikisa taifa na kuhatarisha utawala wa Rais Jakaya Kikwete. Wabunge wa chama tawala na upinzani kwa pamoja walitoa maneno yaliyokuwa mwiba kwa Serikali kwenye ukumbi wa bunge. Ilikuwa dhahiri kuwa waziri mkuu aliyeingia madarakani kwa ahadi ya mageuzi asingeweza kusalimika.
Hatimaye Februari 7, 2008 Edward Lowassa aliachia ngazi.
Mpaka leo wapo wanaoamini kashfa ya Richmond ilikuwa mkakati wa kumwondoa Lowassa madarakani kutokana na makundi ndani ya chama tawala. Imani hiyo inatokana na kukubalika kisiasa kwa Lowassa, hivyo inatajwa lengo la kumng’atua lilikuwa ni kumzuia kuwania urais mwaka 2015 baada ya Kikwete kumaliza muhula wake. Ukweli au uongo wa dhana hiyo haujawahi kufuta kukubalika kwa kiongozi huyo mstaafu.
Katika hotuba yake ya kujiuzulu uwaziri mkuu, mwanasiasa huyo alilalamika sana kwa kutosikilizwa na tume iliyochunguza sakata la Richmond. Hakuwahi kufikishwa mahakamani wala kupata nafasi rasmi ya kujitetea kuhusu uhusika wake kwenye kashfa hiyo. Mwenyewe tangu wakati huo hadi kifo chake aliendelea kukanusha kuhusika na kashfa hiyo, ingawaje kufanya hivyo hakukumwondolea zigo la lawama.
Uchaguzi wa mwaka 2015 ulikuwa na tofauti kubwa zaidi. Wakati Mheshimiwa JK anamaliza muhula wake wa miaka kumi, kinyang´anyiro cha kumpata mrithi wake kilikuwa kikali ndani ya chama tawala. Wengi walitarajia Lowassa kupita kwa kishindo, lakini baada ya jina lake kukatwa CCM, Lowassa alifanya uamuzi mgumu sana. Aliamua kuachana na CCM na kujiunga na chama cha upinzani, Chadema.
Baada ya kukaa upinzani kwa miaka michache, Lowassa aliamua kurudi nyumbani CCM mwaka 2019, ambapo alisalia kuwa mwanachama hadi mauti yalipomfika. Tangazo la kifo chake mnamo Februari 10 mwaka 2024 lilizusha simanzi kubwa chini Tanzania. Bila ya shaka kifo cha Lowasa kinahitimisha enzi ya mwanasiasa aliyetumainiwa na wengi katika aina yake ya uongozi.
Mwenyezi Mungu ampe pumziko la amani, amuondolee adhabu za kuzimu, aipe nguvu familia na kuwapa ustahimilivu viongozi na wananchi walioguswa na msiba wake, Amen.