Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Askofu Mbilu: Tusiwachague wanaotoa rushwa kupata uongozi

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Msafiri Mbilu akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa tano baada ya Jubilee ya Miaka 125 ya Injili uliofanyika Magamba wilayani Lushoto mkoani Tanga kwa siku tatu na kuhitimishwa leo Aprili 5,2025. Picha na Rajabu Athumani

Muktasari:

  • Zaidi ya wajumbe 250 walikusanyika katika mkutano mkuu wa tano baada ya Jubilee ya Miaka 125 ya Injili, kujadili na kupokea taarifa za kiutendaji kutoka kwa Askofu. Pia, ulifanyika uchaguzi wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Dayosisi, wakuu wa majimbo na kuthibitisha jina la msaidizi wa Askofu. Uchaguzi huu hufanyika kila baada ya miaka minne.

Lushoto. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Msafiri Joseph Mbilu, amewataka waumini na Watanzania kwa ujumla kujiepusha na vitendo vya rushwa kutoka kwa wanasiasa wanaotarajia kuwania uongozi katika uchaguzi ujao.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa tano baada ya Jubilee ya Miaka 125 ya Injili, uliofanyika Magamba, wilayani Lushoto, mkoani Tanga, kwa siku tatu na kumalizika leo, Aprili 5, 2025, Askofu Mbilu amesema kuwa jambo moja muhimu ambalo wananchi wanatakiwa kuepuka ni kushawishika na kupokea rushwa ili kuwapigia kura wagombea, badala ya kufuata mifumo sahihi ya uchaguzi.

“Tutatoa elimu kwa wananchi kuwaonyesha umuhimu wa kuepuka rushwa kutoka kwa wagombea, hasa kwa wale wanaowania nafasi za udiwani na ubunge, ambazo ndizo zinazoonekana kuwa na wagombea wengi na pia huwavutia kupeleka rushwa,” amesema Askofu Mbilu, akisisitiza umuhimu wa uchaguzi wa haki na uwazi.

“Wananchi hawapaswi kushawishika kuwachagua wagombea wanaotoa rushwa ili wapate nafasi ya kuchaguliwa, kwani kufanya hivyo kutawafanya kuwa na shida baadaye.”

“Wananchi kama atashindwa kuuliza maswali muhimu, kwani tayari watakuwa na mkataba wa kumuweka mtu madarakani, jambo ambalo si sahihi. Kumpigia kura mtu ambaye si chaguo la wengi kunakosesha haki na kuleta madhara kwa jamii,” amesema.

Amesema wananchi wanatakiwa kuzingatia viongozi wanaoweza kuleta maendeleo katika maeneo yao, na si kuangalia kile watakachopata kutoka kwa mgombea husika.

“Rushwa inawapa nafasi watu ambao baada ya kushinda, watashindwa kutatua matatizo ya wananchi, kwa sababu walipita kwa njia zisizo halali.

"Sisi kama kanisa, mkazo wetu mkubwa ni kuwaelimisha watu waachane na rushwa, ili tuweze kuchagua viongozi wenye sifa na uwezo. Hatuchagui kiongozi kwa sababu amenipa rushwa, bali yule ambaye tunaona anafaa kuleta maendeleo kuanzia ngazi ya chini, kama vile madiwani na wabunge.

“Tunashirikisha makundi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, kuwawezesha kugombea nafasi za uongozi bila kushirikiana na rushwa," amesema Askofu Mbilu.

Askofu Mbilu amesisitiza kuwa uchaguzi ni jambo la amani na kila Mtanzania anapaswa kuhakikisha anailinda.

Amesema kuwa, ingawa ni rahisi kuvuruga amani, kurudisha amani ni mtihani mkubwa, na hivyo wananchi wanatakiwa kujifunza kutoka kwa nchi zilizokumbwa na machafuko.

Kwa upande mwingine, Askofu Dk Isaac Kisiri Laiser wa KKKT Dayosisi ya Magharibi Kati, aliwataka viongozi wa Dayosisi kutumia nyumba za ibada kusisitiza umuhimu wa haki katika masuala mbalimbali, ikiwemo uchaguzi ujao.

Amehimiza kwamba hakuna amani bila haki, na hivyo madhabahu za makanisa ziwe ni sehemu ya kutoa mwongozo kuhusu haki ili amani iwepo kwa jamii.

Askofu Laiser aliongeza kuwa viongozi wa dini wasiruhusu nyumba za ibada kutumika kwa ajili ya kunadi wanasiasa, bali wazingatie kutangaza maandiko ya Mungu, haki na maagizo ya dini.

Mchungaji Anna Msisiri Mdoe, ambaye ni mjumbe wa mkutano huo kutoka usharika wa Ubiri, amesisitiza kuwa viongozi wa dini wanatakiwa kunadi zaidi kuhusu amani na kufanya maombi maalumu kuliombea Taifa kuelekea uchaguzi mkuu, ili kupita salama.

Amesema pia kuwa wataendelea kutoa ushauri kwa wanasiasa pale inapohitajika.

Kadhalika, katika mkutano huo, Askofu  Mbilu ametangaza kuanzishwa kwa majimbo mapya, ikiwemo Jimbo la Diaspora Mission lililopo nchini Uingereza na Jimbo la Magharibi, hivyo kufanya Dayosisi hiyo kuwa na majimbo matano kutoka manne ya awali, pamoja na sharika 76.

Mchungaji Reuben Ismail Ngoda, mkuu wa Jimbo jipya la Magharibi, amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa jimbo hilo ni kusogeza huduma karibu zaidi kwa watu wa Handeni na Kilindi.

Awali, jimbo hilo lilikuwa chini ya Jimbo la Tambalale, ambalo linajumuisha wilaya za Muheza na Korogwe.

Amesema kuwa jimbo hilo lina sharika 13 ambazo awali zilikuwa zinazoongozwa na wainjilisti, lakini sasa zitakuwa zikiongozwa na wachungaji watakaotoa huduma za kiroho, kiuchumi na kijamii.

Pia, katika mkutano huo, wajumbe 217 kati ya 246, sawa na asilimia 88.5 walimuidhinisha Mchungaji Frank Richard Mntangi kuwa Msaidizi wa Askofu (Dean Mteule) wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

Mchungaji Mntangi, ambaye kwa sasa ni mkuu wa Jimbo la Pwani, ameteuliwa kuhudumu katika nafasi hiyo, akichukua nafasi ya Mchungaji Michael Mlondakweli Kanju, ambaye anastaafu kwa mujibu wa sheria za utumishi za KKKT.