Angola yajitosa vita ya M23 dhidi ya FARDC, viongozi SADC nao kujifungia

Muktasari:
- Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN) mapigano kati ya wapiganaji wa M23 dhidi ya vikosi vya Jeshi la Ulinzi la DRC la FARDC yamesababisha watu zaidi ya 7,000 kuuawa huku mamia wakiwemo watoto wakitendewa ukatili ukiwamo wa kingono.
Luanda. Serikali nchini Angola imetangaza rasmi itawasiliana na waasi wa M23 ili kufanikisha mazungumzo ya moja kwa moja na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa lengo la kupata mwafaka wa kurejesha amani mashariki mwa taifa hilo.
Shirika la Habari la Associated Press lilitoa tangazo hilo jana Jumanne, Machi 12, 2025 muda mfupi baada ya mkutano wa Rais wa Angola, Joao Lourenço na Rais wa DRC, Félix Tshisekedi.
Rais Tshisekedi alifanya ziara Angola kwa mara ya pili tangu kuchaguliwa kuliongoza taifa hilo. Ziara hiyo ililenga kutafuta msaada wa kufanyika mazungumzo ya upatanishi yatakayorejesha amani nchini DRC angalau ndani ya mwezi mmoja.

Akizungumzia hatua ya Angola kupitia mitandao ya kijamii, Msemaji wa Ikulu ya DRC, Tina Salama amesema DRC inasubiri utekelezaji wa mpango huo wa upatanishi.
Zaidi ya hayo, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) imetangaza kuwa itafanya mkutano maalumu wa wakuu wa nchi na Serikali Alhamisi, ili kujadili hali ya usalama nchini DRC.
Mgogoro unaoendelea kati ya waasi wa M23 na Serikali ya DRC umesababisha idadi kubwa ya watu kuyakimbia makazi yao na kuzidisha hofu inayoambatana na janga la kibinadamu Mashariki mwa DRC. Hali bado ni tete licha ya juhudi za kidiplomasia na kijeshi kufanyika kwa lengo la kumaliza mapigano.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN) mapigano kati ya wapiganaji wa M23 dhidi ya vikosi vya Jeshi la Ulinzi la DRC la FARDC yamesababisha watu zaidi ya 7,000 kuuawa, huku mamia wakiwemo watoto wakitendewa vitendo vya ukatili ikiwamo wa kingono.
Maelfu wanadaiwa kujeruhiwa huku wengine wakilazwa hospitalini kutokana na majeraha waliyoyapata katika mapigano hayo.
UN pia imesema zaidi ya watu 300,000 wamekuwa wakimbizi katika mataifa jirani huku Shirika la Chakula Duniani (WFP) likidai watoto wako hatarini kukumbwa na janga la ukosefu wa chakula kutokana na mapigano hayo.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.