Aliyepinga Rais Samia kupitishwa mgombea pekee urais afukuzwa CCM

Muktasari:
- Dk Malisa amesema anaendelea na mchakato wa kupinga uamuzi wa mkutano mkuu wa CCM wa kumpitisha Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea pekee wa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu akidai Katiba ya CCM imekiukwa.
Moshi. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro kimemfukuza uanachama, Mchungaji Godfrey Malisa, kwa tuhuma za kukiuka katiba na maadili ya chama hicho.
Hatua ya kufukuzwa kwa Malisa inatokana na kauli zake za kupinga uamuzi wa Mkutano Mkuu wa chama hicho Taifa uliofanyika Januari 19, 2025, akidai uamuzi wa kupitisha mgombea urais ulikiuka katiba ya chama hicho tawala.
Mchungaji Malisa, aliyewahi kuwa mgombea urais, uspika na hata ubunge, alijiunga na CCM mwaka 2020 na alikuwa miongoni mwa makada tisa waliochukua fomu kugombea uenyekiti wa chama hicho mwaka 2022.
Akitangaza uamuzi wa kikao cha Halmashauri Kuu ya chama mkoa, Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Merce Mollel, amesema Mchungaji Malisa amefukuzwa uanachama kuanzia leo, Jumatatu, Februari 10, 2025.
"Leo tulikuwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro ambacho, pamoja na mambo mengine, kimemfukuza Dk Godfrey Malisa aliyekuwa mwanachama wa CCM," amesema Mollel na kuongeza kuwa:

Mchungaji Godfrey Malisa aliyefukuzwa CCM.
"Malisa amefukuzwa kutokana na kukosa sifa za kuendelea kuwa mwanachama wa CCM kwa sababu mara kwa mara sasa amekuwa akibeza maamuzi halali yaliyofanywa na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa uliofanyika Januari 19, jijini Dodoma."
Amesema baada ya Mkutano Mkuu, Malisa amekuwa akitoa matamko ambayo hayaleti umoja na mshikamano ndani ya chama na nchi.
Mollel amesema Malisa ameenda mbali na kudai kuwa mkutano huo mkuu umevunja Katiba ya CCM, jambo ambalo si la kweli.
"Kwa mujibu wa kanuni za maadili ya chama chetu, kifungu cha 6, kifungu kidogo cha tatu, kinaeleza waziwazi. Hivyo, amekosa sifa za uanachama," amesema katibu huyo.
Hata hivyo, Mwananchi imezungumza na Dk Malisa kuhusiana na hatua hiyo, ambaye amesema taarifa ya kufukuzwa kwake ameisikia kupitia vyombo vya habari na kwamba bado hana taarifa rasmi kutoka CCM.
"Nimesikia nimefukuzwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro bila kusikilizwa wala kupewa taarifa. Hii ni taarifa tu niliyoisikia," amesema Dk Malisa.
Lakini Katibu Mollel amesema kikao cha Halmashauri Kuu kimetimiza matakwa ya katiba ya kumfukuza kwa kigezo cha usaliti kwa sababu amekuwa akipingana na uamuzi halali wa kikao kikubwa cha chama.
"Malisa anajiita mwanachama mwandamizi wa CCM, hiyo siyo kweli kwa sababu alijiunga na CCM mwaka 2020, na muda wote tulikuwa tunamlea," amesema Mollel.
Mapema leo asubuhi, Dk Malisa amezungumza na Mwananchi kuhusu kauli yake ya kutaka kwenda mahakamani kupinga uamuzi wa Mkutano Mkuu wa CCM wa kumpitisha Rais Samia Suluhu Hassan kugombea nafasi ya urais, ambapo amesema amepewa wito wa kufika polisi kwa ajili ya mahojiano.
Amesema tayari ameanza utaratibu wa kuiburuza mahakamani Bodi ya Wadhamini wa CCM kwa kitendo cha kumtangaza Rais Samia kuwa mgombea pekee wa urais.
Amesema chama hicho kinazingatia demokrasia na katiba ya nchi na haijawahi kuwa na utaratibu wa kumpitisha mgombea mmoja kwenye kinyang’anyiro cha urais, huku akisisitiza kuwa kilichofanyika kinawanyima wanachama fursa ya kuchagua na kuchaguliwa.
Dk Malisa amesema tayari mamia ya wanachama wa CCM wamejitokeza kumuunga mkono kuifungua kesi hiyo.
"Tayari tunakamilisha mchakato wa kisheria wa kuipeleka Bodi ya Wadhamini mahakamani kwa kitendo cha CCM kumpitisha mgombea mmoja wa nafasi ya urais bila kutoa fursa kwa wanachama wengine," amesema.
Amesema kuna utaratibu wa wazi wa wagombea wa nafasi ya urais namna wanavyotakiwa kupatikana, lakini kwa CCM umekiukwa.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Mkutano Mkuu wake ndiyo chombo cha mwisho cha uamuzi wa uteuzi wa mgombea wa kiti cha urais kupitia chama hicho.
Siku ya uamuzi wa kumpitisha Samia kugombea nafasi hiyo, lilitolewa azimio kuwa agombee nafasi hiyo na likaridhiwa na wajumbe wote wa Mkutano Mkuu.
Mbali na Rais Samia kupitishwa kuwa mgombea pekee wa CCM upande wa Tanzania Bara, pia mkutano huo uliridhia na kupitisha jina la Dk Hussein Mwinyi kuwa mgombea urais kwa upande wa Zanzibar.