Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT yadai uchunguzi huru wa kimataifa ghasia za Oktoba 29, yamtaja Lissu

Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Tanzania Bara, Isihaka Mchinjita, akizungumza wakati akisoma maazimio ya kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichofanyika jana.

Muktasari:

  • Hatua hiyo imekuja baada ya kikao cha dharura cha Kamati Kuu Maalumu ya chama hicho kilichofanyika jana, Mei 3, 2026, kikiongozwa na Mwenyekiti wake, Othman Masoud Othman, kwa lengo la kufanya tathmini ya hali ya siasa nchini kwa kuichambua ripoti ya Jaji Chande.

Dar es Salaam. Baada ya kuichambua ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, Chama cha ACT-Wazalendo kimeazimia na kupendekeza hatua kadhaa, ikiwemo kuanzishwa kwa uchunguzi huru wa kimataifa chini ya Jumuiya ya Kimataifa au Umoja wa Afrika.

Mbali na hilo, kimependekeza kuachiwa huru watu wote wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi au wanaokabiliwa na kesi kwa sababu za kisiasa, akiwemo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.

Pia, kimependekeza kuanzishwa kwa mpango wa kitaifa wa kuwasaidia waathirika wote kwa misaada ya kifedha, kitabibu, kisaikolojia na kisheria.

Vilevile, chama hicho kimependekeza kuchukuliwa kwa hatua za kisheria dhidi ya wote waliohusika na matukio ya Oktoba 29, wakiwemo wakuu wa mikoa 11 wa maeneo kulikotokea vurugu, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, kuanza mchakato wa Katiba mpya, kuondoa vyombo vya usalama katika shughuli za kisiasa, kuvunjwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), pamoja na kutungwa kwa sheria mpya ya uchaguzi.

Hatua hizo zimekuja baada ya kikao cha dharura cha Kamati Kuu Maalumu ya chama hicho kilichofanyika jana Jumapili, Mei 3, 2026, kikiongozwa na mwenyekiti wake, Othman Masoud Othman, kwa lengo la kufanya tathmini ya hali ya siasa nchini kwa kuichambua ripoti ya tume hiyo.

Aprili 23, 2026, wakati akiwasilisha matokeo ya ripoti hiyo, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu mstaafu Othman Chande, alitaja vyanzo vitano pamoja na vichocheo vinne vya matukio hayo yaliyosababisha vifo vya watu 518, majeruhi na uharibifu wa mali za umma na watu binafsi.

Akisoma maazimio ya kikao hicho, Dar es Salaam, leo Mei 4, 2026, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita, amesema Taifa limefikia hatua inayohitaji nia ya dhati katika utekelezaji wake badala ya hadaa za kisiasa za kujenga taswira nzuri ya nchi kwenye jumuiya ya kimataifa.

“Taifa limefikia mahali ambapo kinachohitajika sasa ni nia ya dhati ya utekelezaji, si hadaa za kisiasa za kujenga taswira nje ya nchi,” amesema.

Amesema hatua za dharura zinazohitajika kufanyika kwanza ni kuanzishwa kwa uchunguzi huru wa kimataifa chini ya jumuiya za kimataifa au Umoja wa Afrika, ukiwa na ulinzi kamili wa mashahidi.

“Hatua za dharura tunazohitaji zianze mara moja ni kuanzishwa kwa uchunguzi huru wa kimataifa chini ya jumuiya za kimataifa au Umoja wa Afrika, huku mashahidi wakipewa ulinzi kamili,” amesema.

Akifafanua hoja hiyo, Mchinjita amesema kumekuwapo na dhana kwamba kualika vyombo vya kimataifa ni kupoka uhuru wa nchi, akisisitiza kuwa jambo hilo halina ukweli.

“Kuna dhana kwamba kualika vyombo vya kimataifa ni kupoka uhuru wa nchi, lakini hilo si kweli,” amesema.

Ameeleza jumuiya zinazotakiwa kushiriki ni zile ambazo Tanzania ni mwanachama wake na kwamba moja ya wajibu wa jumuiya hizo ni kulinda haki za binadamu na kuheshimu sheria pamoja na utawala bora.

“Tunasema wazi tunahitaji jumuiya ambazo Tanzania ni mwanachama wake, na moja ya wajibu wao ni kulinda haki za binadamu, kuheshimu sheria na kuimarisha utawala bora,” amesema.

Mchinjita amesema Tanzania imewahi kushiriki katika misheni za kimataifa kutatua matatizo kama yaliyotokea Oktoba 29 katika nchi nyingine, akitoa mfano wa machafuko ya mwaka 2007 nchini Kenya, ambapo Tanzania ilishiriki katika juhudi za upatanishi zilizoisaidia Kenya kutoka kwenye hali ya vurugu za uchaguzi hadi kufikia uchaguzi unaoheshimu haki za raia.

Vilevile, amesema Tanzania imewahi kushiriki katika juhudi za kimataifa kuisaidia Sudan, na hivyo ni jambo la kushangaza kuona leo nchi inapata kigugumizi kuzialika jumuiya za kimataifa kusaidia kuliponya Taifa.

“Inashangaza kuona leo Tanzania inapata kigugumizi kuzialika jumuiya za kimataifa, ilhali yenyewe imewahi kushiriki kusaidia mataifa mengine kama Sudan,” amesema.

Kuhusu suala la watu kushikiliwa kwa sababu za kisiasa, akiwemo Lissu, Mchinjita amesema matukio ya kisiasa hujenga chuki na hasira miongoni mwa jamii na kuendeleza mpasuko katika Taifa.

“Matukio ya kisiasa yanapokuwa ya aina hii hujenga chuki, hasira na kuongeza mpasuko katika jamii,” amesema.

Amesema inashangaza kuona watu bado wanashikiliwa, wakiwemo viongozi wa kisiasa, kwa tuhuma zisizo na ushahidi wa wazi.

“Inashangaza kuona bado kuna watu wanashikiliwa, wakiwemo viongozi wa kisiasa, kwa tuhuma ambazo hazina ushahidi wa wazi,” amesema.

Amesema masuala hayo yanapaswa kushughulikiwa iwapo viongozi wana nia ya dhati ya kuliponya Taifa baada ya matukio yaliyotokea.

“Waathirika lazima wasaidiwe kwa njia zote kifedha, kisaikolojia, kisheria na kitabibu, hasa waliopata ulemavu au waliopoteza wapendwa wao.

“Viongozi waliokuwa na dhamana ya ulinzi wa raia wanapaswa kuwajibika kwa kujiuzulu kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao,” amesema na kuongeza kuwa haiwezekani kudai matukio kama hayo hayatajirudia ilhali waliokuwa na dhamana ya ulinzi wa raia walishindwa kutekeleza wajibu wao.

Pia ametaka Msajili wa Vyama vya Siasa na wakuu wa mikoa ambayo matukio hayo ya mauaji  yametokea kuwajibishwa, ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Dodoma, Shinyanga, Mara, Geita, Ruvuma, Iringa, Mbeya na Songwe.

Jaji Chande alipowasilisha ripoti yake, pamoja na mambo mengine, alipendekeza kuundwa kwa Tume ya Jinai kuchunguza kwa kina matukio hayo na kutoa nafasi ya wanaotuhumiwa kujieleza kabla ya kuchukuliwa hatua zaidi.