Mgomo wa Walimu Kenya, Tanzania ina mengi ya kujifunza

Suzan Mwillo
Muktasari:
Mara zote ambazo CWT ilipanga kuanza mgomo, azma yao ilikatishwa na amri ya Mahakama ama mazungumzo baina ya chama hicho na serikali.
Kwa muda mrefu sasa Serikali imekuwa kwenye mgogoro wa kimaslahi na walimu, jambo lililofanya Chama cha Walimu nchini (CWT) kuwahamasisha wanachama wake kuingia kwenye mgomo usio na kikomo.
Mara zote ambazo CWT ilipanga kuanza mgomo, azma yao ilikatishwa na amri ya Mahakama ama mazungumzo baina ya chama hicho na serikali.
Vitu ambavyo walimu wamekuwa wakidai ni pamoja na kulipwa malimbikizo ya fedha za likizo, kupandiswa madaraja na kutaka mishahara yao iongezwe.
Madai hayo hayatofautiani na yale ya walimu wa Kenya ambao wamekuwa kwenye mgomo kwa majuma mawili licha ya kuwapo kwa amri ya mahakama iliyowataka kurudi darasani.
Umoja wa Walimu nchini Kenya (KNUT), umekuwa ukisisitiza kuendelea na mgomo huo mpaka pale Serikali ya nchi hiyo itakapoyafanyia kazi madai yao.
Chama hicho kinasema kuwa, tangu mwaka 1997 wamekuwa wakitaka serikali kufanyia kazi madai yao kuboreshewa masilahi yao.
Wanasema kuwa, walikubaliana na serikali kuwa walipwe posho maalumu kwani mishahara yao ni midogo isiyotosheleza mahitaji yao.
Posho ambayo Serikali ya Kenya ilikubali kuwalipa walimu ni ile ya matibabu, usafiri na ile ya nyumba.
Miaka 16 ya uvumilivu kwa walimu hao, imefika kikomo na kuamua kuweka chaki chini kusubiri serikali itekeleze madai yao ndiyo warudi darasani.
Mwenyekiti wa Umoja wa Walimu, Wilson Sossion amekuwa mstari wa mbele kuhimiza walimu kuwa na msimamo hadi pale Serikali itakaporidhia makubaliano yao ya mwaka 1997 na kinyume cha hapo hakuna kuingia darasani.
Mgomo huu unadaiwa kuchochewa sana hatua ya wabunge wa nchi hiyo kutaka kuongezewa posho, huku kundi hilo linalotegemewa kujenga nguvu kazi ya taifa likiachwa.
Serikali ya Tanzania ina mengi sana ya kujifunza kutokana na hali hii ambayo imewafanya watoto wengi wa maskini wasipate fursa ya kuudhuria darasani.
Nasema hivyo kwa kuwa wanaoshiriki mgomo huu ni walimu wa shule za umma tu ambazo ndizo zinazofundisha watoto wa maskini.
Walimu hawa wa Kenya wameendelea na mgomo hata baada ya amri ya Mahakama ambayo kwa Tanzania iliweza kuokoa jahazi na walimu kurudi darasani.
Lakini hata baada ya kurudi darasani, wamekuwa wakidaiwa kuendelea na mgomo baridi na kuwa hiyo ni moja ya sababu zinazofanya elimu iendelee kuporomoka kila kukicha.
Hali hii inaathiri watoto wa maskini zaidi kwani sote tunajua kuwa ndio walio kwenye shule za umma, wale wa wenye nacho wanasoma katika shule hizi zinazoitwa za kimataifa.
Kabla ya walimu hawa wa Kenya kufikia hatua ya kuweka pamba masikioni kama vile ambavyo serikali yao ilifanya pale walipokuwa wanadai stahili zao hizo kwa njia ya kukaa mezani, mara kadhaa nao walijaribu kuitisha migomo lakini ikazimwa kwa njia mbalimbali.
Hivyo basi ni vyema vyombo husika vya Serikali ya Tanzania vikajua kuwa, hata walimu wake inafika siku wataweka pamba masikioni na wasisikie chochote mpaka pale madai yao yatakapofanyiwa kazi.
Kabla hatujafika huko, ambako Watanzania wote wapenda maendeleo hatuombei hilo litokee ni vyema serikali ikatumia hekima na kutimiza mahitaji ya walimu.
Kutumia mahakama, kauli za vitisho na mambo mengine kama hayo, kamwe haiwezi kuwa suluhisho kwa elimu yetu ambayo kuina kila dalili kuwa inatetereka.
Ikumbukwe kuwa hali ya Wabunge wa Kenya ambao wanadaiwa kuchochea mgomo huo kutoka na kitendo chao cha kutaka kujiongezea posho, wale wa Tanzania pia walitaka kujiongezea posho bila kujali kuwa kuna makundi mengine yanayoteseka kwa ugumu wa maisha kutoka na fedha kidogo wanazolipwa licha ya kufanya kazi kubwa.
Kwa maana hiyo, kuna viashiria vyote kuwa itafika mahali uvumilivu utawashinda na wataingia kwenye mgomo bila kujali ni nani anawaunga mkono na nani anawapinga.
Kila binadamu ana kiasi cha kuvumilia mambo, tusisubiri mpaka pale uvumilivu wa walimu wetu utakapoisha ndipo tuanze kufanyia kazi madai yao. Tuache mambo ya kutegemea Mahakama na mabavu katika kumaliza migogoro ambayo inatakiwa imalizwe kwa pande husika kukaa chini na kuelewana.
Matokeo mabaya kwa mitihani ya taifa iwe fundisho kwa wahusika, tusisubiri mambo yawe mabaya zaidi ni vyema mahitaji ya walimu yakatimizwa ili wafanye kazi kwa moyo.