Mchungaji Msigwa adai CCM inakwepa kodi ya majengo

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa
Muktasari:
Adai mbali na wafanyabiashara chama hicho kinaongoza kutolipa kodi za majengo Iringa
Iringa. Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa ameituhumu CCM kuwa ni miongoni mwa taasisi zinazokwepa kulipa kodi ya majengo na kuisababishia hasara Serikali.
Mchungaji Msigwa alitoa tuhuma hizo juzi, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Mwembetogwa jimboni mwake ulioandaliwa na chama chake kwa lengo la kuwashukuru wananchi kutokana na ushindi walioupata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Katika uchaguzi huo, Msigwa alitetea kiti cha ubunge, huku Chadema ikipata madiwani wa kata 14 kati ya 18 zilizopo jimboni humo na kuandika historia kwa halmashauri za mkoa huo kuongozwa na chama cha upinzani.
Alisema yeye na chama chake wanaunga mkono jitihada za Rais John Magufuli kukusanya kodi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kwamba, kwa muda mrefu wananchi wa kipato cha chini wamekuwa wakibanwa huku matajiri wakikwepa kodi.
Alisema CCM hakilipi kodi ya Uwanja wa Michezo wa Samora inaoumiliki, jengo la ofisi za mkoa na wilaya zilizopo Sabasaba, Shule ya Sekondari ya Wazazi ya Mwembetogwa na vibanda vya biashara maarufu kama vibanda vya kiti moto.
“Kama wao wanakwepa kodi, wanapata wapi uhalali wa kukusanya kodi?” alihoji Msigwa.
Mbunge huyo alisema wanamuunga mkono Rais Magufuli na wanataka aendelee na kazi ya kutumbua majipu.
“Kwa bahati nzuri mengi yako CCM. Wakati akifanya hivyo sisi tutamsaidia kukamua na kumuonyesha majipu mengine huku chini,” alisema.
Hata hivyo tuhuma hizo yalipingwa na Kaimu Katibu wa CCM wa mkoa huo, Elisha Mwampashi ambaye pia ni Katibu wa CCM wa Manispaa ya Iringa akisema kila mwaka wanalipa kodi kulingana na eneo ambalo jengo lao lipo.
Alisema wanamiliki majengo katika maeneo mengi ambayo yamekuwa yakilipiwa kodi kwa mujibu wa sheria.
“Msigwa siyo mkweli, katika hili kwa kuwa amekuwa katika nafasi ya ubunge kwa miaka mitano ana taarifa za Manispaa ya Iringa juu ya mapato yatokanayo na kodi ya majengo, yakiwamo majengo yetu,” alisisitiza Mwampashi.
Awali, Msigwa aliwataka wamiliki wa mashamba makubwa ndani ya manispaa hiyo kuanza utaratibu wa ama kuyapima viwanja wao wenyewe na kuviuza kwa wananchi au kuyaacha yachukuliwe na Serikali kwa kuwa sheria ya mipango miji hairuhusu mtu kuwa na shamba ndani ya mji.
Alisema wapo matajiri wanaomiliki ekari nyingi kwa ajili ya mashamba, jambo ambalo halikubaliki kuwa na eneo kwa ajili ya shamba mjini na kuwa, vikao vya baraza la madiwani linaloongozwa na chama chao vitakapoanza vitalishughulikia suala hilo.
Akizungumza katika mkutano huo, Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe alisema imejipanga kukusanya kodi na kuongeza mapato kutoka Sh2.4 bilioni zilizokuwa zikikusanywa awamu iliyopita hadi Sh7 bilioni.