Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu Tanzania kuwekeza kwenye uandishi bunifu

Muktasari:

  • Mtu anaweza kuhoji faida ya uandishi bunifu katika dunia ya sayansi na teknolojia na kama kazi hizo zina mchango wa kimaendeleo.

Kwa mara nyingine, Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET),  imetoa tuzo kwa washindi wa tuzo za Mwalimu Nyerere za Uandishi Bunifu.

Katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Hussein Abdalla alitwaa tuzo ya taifa upande wa ushairi, huku Tyatawelu Kingu akiibuka wa  kwanza katika kipengele cha tamthiliya.

Tune Salim amekuwa mshindi wa kwanza katika kipengele cha hadithi za watoto, huku  Maundu Mwingizi akiwa kinara wa riwaya.

Kila mshindi katika kipengele alipewa hundi ya  Sh10 milioni, cheti na ngao na miswada yao itachapishwa na Serikali  na kusambazwa katika  shule zote nchini na kwenye maktaba.

Tuzo hiyo inalenga pamoja na mambo mengine kuenzi mchango wa kifasihi wa Rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere.  

Akizungumza na Mwananchi katika hafla hiyo, mwandishi mkongwe wa vitabu, Richard Mabala, anasema uandishi bunifu ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya kiakili, kijamii na kiutamaduni, hivyo jamii inapaswa kuutambua, kuuendeleza na kuuwezesha ili kuwa daraja kati ya sanaa na sayansi katika dunia ya sasa inayobadilika kwa kasi.

Mtu anaweza kuhoji faida ya uandishi bunifu katika dunia ya sayansi na teknolojia na kama kazi hizo zina mchango wa kimaendeleo.

Ikumbukwe kuwa ingawa uandishi huu unahusishwa zaidi na kazi za sanaa kama riwaya, mashairi, hadithi fupi, na tamthilia, mchango wake katika nyanja za kisayansi na kiteknolojia ni wa kipekee na muhimu zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote. Wataalamu wa Sana'a hii wanataja baadhi ya manufaa yake:

Kwanza, uandishi bunifu huendeleza ubunifu na fikra pevu. Katika enzi ya teknolojia ya haraka na uvumbuzi, uwezo wa kufikiri tofauti na kwa undani ni wa msingi. Wanasayansi na wahandisi wengi maarufu wametegemea ubunifu katika mawazo yao ya awali, na mara nyingi huanzia katika taswira zinazofanana na hadithi.

Mfano mzuri ni maendeleo katika teknolojia ya angani ambayo yaliwahi kutabiriwa na waandishi wa sayansi ya kubuni kama Jules Verne na H.G. Wells. Uandishi bunifu unawapa wataalamu wa sayansi uwezo wa kuota makubwa na kufikiria kwa njia isiyo ya kawaida, jambo ambalo ni muhimu katika uvumbuzi.

Pili, uandishi bunifu huimarisha mawasiliano. Sayansi na teknolojia mara nyingi hutumia lugha ngumu inayoweza kumchanganya mtu wa kawaida. Kupitia uandishi bunifu, wataalamu wanaweza kueleza dhana ngumu kwa njia rahisi, ya kuvutia, na inayogusa hisia za watu. Hii huongeza uelewa wa jamii kuhusu maendeleo ya kisayansi na umuhimu wake. Kwa mfano, uandishi wa hadithi za kisayansi au filamu za kisayansi husaidia watu kuelewa athari za teknolojia mpya katika maisha yao.

Tatu, uandishi bunifu huchochea mjadala wa kimaadili kuhusu matumizi ya teknolojia. Katika dunia ya leo ambako masuala ya akili bandia, uhandisi wa kijeni, na uchimbaji wa data yanaibua maswali mengi ya kimaadili, uandishi wa kubuni unaweza kusaidia kufungua mjadala. Kupitia hadithi au riwaya, waandishi wanaweza kuonyesha matokeo chanya au hasi ya teknolojia fulani kabla hata haijatekelezwa, hivyo kusaidia jamii kufanya maamuzi ya busara kuhusu matumizi yake.

Aidha, uandishi bunifu huendeleza uwezo wa mtu kuelewa mitazamo tofauti. Katika uandishi, hususan wa hadithi, kuna uhusiano wa karibu na wahusika tofauti wenye mitazamo tofauti. Hii husaidia wataalamu wa sayansi na teknolojia kuwa na huruma, kuelewa athari za kazi zao kwa binadamu, na hivyo kuwa wabunifu wenye maadili.

Mwisho, uandishi bunifu hutoa fursa ya kupumzika na kuimarisha afya ya akili. Katika ulimwengu unaoendeshwa na kasi ya teknolojia, watu hukabiliwa na msongo wa mawazo. Kusoma au kuandika kazi za bunifu huwapa nafasi ya kupumua, kutafakari, na kujenga ulimwengu wa ndani unaosaidia katika kuleta uwiano wa maisha.

Kwa ujumla, uandishi bunifu si tu sehemu ya sanaa bali ni kiungo muhimu katika kukuza sayansi na teknolojia ya sasa. 

Unawezesha ubunifu, hurahisisha mawasiliano, huchochea maadili, huimarisha hisia na mitazamo tofauti, na huchangia ustawi wa afya ya akili.

 Dunia ya leo inahitaji zaidi si tu maarifa ya kiteknolojia, bali pia uwezo wa kufikiri kwa kina na kwa hisia—ambavyo vyote hupatikana kupitia uandishi bunifu.


Kisa cha Elbert  Einstein

Faida za uandishi bunifu zinajiakisi katika kisa cha mwanasayansi na mwanafalasafa maarufu duniani  Albert Einstein. Akisimulia kisa hicho, mwandishi Chambi Chachage anasema kuhusu mazungumzo baina ya mwanasayansi huyo na mama aliyetaka mwanaye awe mwanasayansi. 

Kila alipomuuliza mtoto wake asome nini inasemekana gwiji huyo alisema asome maandishi bunifu zaidi na zaidi. Kilichotokea ni kuwa mama alipinga akitaka jibu makini zaidi lakini, kwa mujibu wa blogu ya Maktaba ya Bunge la Marekani, mwanasayansi huyo alisisitiza kuwa maandishi bunifu huchochea ubunifu wa kisayansi.

Chachage katika makala yake aliyoandika katika gazeti hili hivi karibuni, anasema: 

" Inaonekana mapinduzi yote ya viwanda, kuanzia ya kwanza hadi ya tatu na ya sasa ya nne yanayohusiana na teknolojia za kiroboti na kadhalika, yameendana na kuibuka kwa aina za uandishi bunifu unaochochea ugunduzi, uvumbuzi, na ubunifu."

Anaongeza kusema: "... hili liko wazi zaidi kwenye aina ya uandishi bunifu wa kisayansi wenye tabia ya kuandika kuhusu vitu vya kiteknolojia ambavyo bado jamii hata haijafikiria vinaweza kuwepo na kutumika. Inadhihirika vitu vilivyoanza kuzoeleka sasa kama magari yanayojiendesha yenyewe na mashine zinazofikiri kama sisi binadamu kupitia akili mnemba/bandia kwa kiasi kikubwa vilianzia kwenye maandishi bunifu."


Uandishi bunifu ni nini?

Kitaalamu, hii ni sanaa inayotumia lugha kiubunifu.  Ni aina ya sanaa inayotumia lugha ili kuelezea tajriba za binadamu.

Mfano mmoja wa uandishi wa ubunifu ni uandishi wa tamthiliya . Tamthiliya zinajumuisha riwaya za kimapokeo, hadithi fupi na riwaya za picha


Profesa Mkenda ataja sababu ya tuzo

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda anasema Serikali ilidhamiria kutoa tuzo hiyo na kuipa jina la Mwalimu Nyerere, kwa ajili ya kumuenzi kiongozi huyo aliyekuwa na mapenzi makubwa na uandishi wa fasihi.

“Mwalimu Julius Nyerere  si tu mwasisi wa Taifa hili, bali ni mwanasiasa maarufu duniani na mwandishi wa vitabu vya fasihi akiandika pia mashairi na kutafsiri kazi za uandishi.

Kiongozi huyu pamoja na majukumu mazito aliyokuwa nayo katika kuliongoza Taifa na harakati za ukombozi, alitenga muda wake kwa ajili ya kazi za uandishi wa kazi bunifu,” anasema.

Profesa Mkenda anasema pamoja na kumuenzi Mwalimu Nyerere, lengo la tuzo hizi ni kuhamasisha Watanzania wengi wajitokeze kuandika, ili wajue wanapoandika wanaweza kutambuliwa.

Lengo lingine ni kukuza lugha ya Kiswahili na kuhamasisha Watanzania wengi kuweka maandishi kwenye lugha hiyo adhimu, ambayo umaarufu wake unaongezeka siku hadi siku.

Mbali na hilo Profesa Mkenda anasema tuzo hizo zimeanzishwa kwa lengo la kukuza utamaduni wa kujisomea hasa kazi za waandishi wazawa wanaoandika kuendana na muktadha wa Kitanzania.

“Mbali na mshindi kupata fedha, Serikali itagharamia uchapishaji wa kitabu kuhakikisha kinachapwa na kusomwa katika shule zote. Hii ni heshima kubwa kwa mwandishi.

Tunataka kuhamasisha usomaji, kuna vitabu vya kiada na ziada ambavyo unaweza kusoma kujiongezea uelewa. Haina maana kupata vitabu sasa viondoe vitabu vya zamani. Huenda baadaye hivi vinavyoshinda vikawa vya kiada" anaeleza.

Lengo lingine kwa mujibu wa waziri huyo, ni kuhifadhi historia na maadili ya nchi yetu kupitia maandishi ya fasihi yanayoandikwa na waandishi wazawa.

Anasema hakuna nchi inayoweza kutambulika bila utamaduni, hivyo ni muhimu  kuweka msisitizo kwenye uandishi bunifu ili maandiko yabebe taswira ya utamaduni wa Mtanzania.

“Ni wajibu wetu kukuza uandishi ambao unachambua mazingira yetu kama ambavyo tunasoma vitabu vya wenzetu wanaoeleza mambo yao na tamaduni zao ambazo na sisi tunaziiga.Changamoto kubwa ya dunia sasa ni aina ya maandishi yanayokuza baadhi ya maadili yanayokinzana na maadili yetu, " anasema na kuongeza:

"Hivyo ni muhimu kuwa na watu wanaoandika vitabu kuhusu maadili yetu kuliko kupoteza muda mwingi kuzuia vile vinavyoharibu maadili."