Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wenye kilo chini ya 50 watakiwa kujifungia ndani kisa upepo mkali

Muktasari:

  • Mamlaka za mitaa zimeonya juu ya dhoruba adimu kuikumba China huku upepo ukifikia kasi ya kilomita 150 kwa saa, upepo huo umelikumba eneo la Kaskazini mwa China.

Shanghai. Serikali nchini China imetoa wito kwa wakazi wa Kaskazini mwa nchi hiyo walio na uzito wa chini ya kilo 50 kujifungia ndani ya nyumba, huku wakionya kuwa wanaweza kupeperushwa kwa urahisi na upepo mkali unaovuma katika eneo hilo.

Shirika la Habari la Reuters limeripoti leo Jumatatu Aprili 14, 2025 kuwa, Mamlaka ya hali ya hewa ya China imetoa tahadhari mara tano juu ya dhoruba hiyo katika kipindi cha wiki mbili zilizopita (Jumamosi na Jumapili) ambapo upepo, mvua, theluji, na radi zimekuwa zikipiga eneo la Kaskazini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo upepo unaopuliza umefikia kiwango cha 13, nguvu ya upepo hupimwa kwa kipimo cha kutoka daraja la kwanza hadi la 17.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo ya hali ya hewa ya China, upepo wa daraja la 11 unaweza kusababisha uharibifu mkubwa kwenye miundombinu na maisha ya watu, huku wa daraja la 12 ukileta uharibifu wa kiwango cha juu kabisa.

Tahadhari ya upepo wa kiwango cha kati ambayo ni ya pili kwa ukubwa katika mfumo wa tahadhari wa ngazi nne nchini China, ilitolewa mjini Beijing siku ya Ijumaa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Dhoruba hiyo, iliyosababishwa na uwepo wa vichocheo vya upepo vinavyopuliza  kutoka Mongolia kuelekea Kusini, ilisababisha upepo uliofikia kasi ya kilomita 150 kwa saa katika maeneo ya Beijing, Tianjin na sehemu za Hebei.

Mamlaka za serikali katika maeneo hayo ziliwaonya wakazi kuwa upepo huo ulikuwa na nguvu ya kung’oa miti yenye mashina yenye kipenyo cha hadi sentimita 30.

Ili kupunguza madhara, bustani za jiji zilifungwa na miti ya zamani ilikatwa matawi ama kuimarishwa.  Hata hivyo, licha ya hatua hizo, takriban miti 300 iliangushwa, na kusababisha uharibifu kwa magari kadhaa.

Hakuna majeruhi walioripotiwa. Maofisa pia waliwashauri wakazi milioni 22 wa Jiji la Beijing kuepuka safari zisizo za lazima.

“Watu wote mjini Beijing walikuwa na wasiwasi mkubwa. Leo hakuna watu wengi mtaani. Hata hivyo, haikuwa mbaya kama nilivyotarajia,” mkazi mmoja aliambia shirika la habari la Reuters.

Mkazi mwingine, mwenye umri wa miaka 30 aitwaye Li, aliongeza: “Haikuwa mbaya kiasi cha kutotoka nje kabisa lakini imeathiri shughuli za kila siku kwa kiasi fulani.”

Dhoruba hiyo pia ilivuruga usafiri. Zaidi ya safari 400 za ndege zilifutwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beijing Capital na huduma kadhaa za reli zilisitishwa. Ingawa maduka ya rejareja yalibaki wazi, bidhaa ziliondolewa haraka kutoka kwenye maeneo ya wazi.

Katika miji ya Shijiazhuang na Mji wa Laiyuan, jimbo la Hebei, miti iliyoanguka na mabaki mengine ilisababisha kufungwa kwa barabara, huku dhoruba za mchanga zikiwalazimu maofisa kufunga barabara nyakati za usiku.

Katika maeneo ya magharibi, Gansu na Ningxia pia ziliripotiwa kuwa na dhoruba za mchanga, huku mwonekano ukishuka hadi mita 50 katika baadhi ya maeneo.


Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.