Ugonjwa wa macho mekundu husababisha uoni hafifu

Muktasari:
Maradhi haya hutokea baada ya kuvimba kwa ukuta na mishipa midogo ya damu iliyo kwenye ukuta huu.
Macho mekundu au conjunctivits kwa kitaalam ni maradhi yanayohusisha ukuta wa nje wa sehemu ya mbele ya jicho ijulikanayo kama conjunctiva. Conjuctiva ni ukuta ambao hulinda sehemu nyeupe ya jicho pamoja na ukuta wa ndani wa ngozi ifunikayo jicho, yaani kope.
Maradhi haya hutokea baada ya kuvimba kwa ukuta na mishipa midogo ya damu iliyo kwenye ukuta huu.
Kuna mambo mengi yanayosababisha macho yawe mekundu. Sababu hizi ni pamoja na maambukizi ya virusi au vimelea vya maradhi aina ya bakteria (mfano bakteria wanaosababisha kisonono).
Kemikali zinazosababisha mzio kwa mfano sabuni, mafuta ya kupaka, vumbi au moshi. Inaelezwa, moshi ni sababu kubwa kwa wazee wanaoishi vijijini.
Maradhi haya hutokea pale vyanzo hivi vinapotoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Maradhi haya husambaa kwa urahisi bila haja ya kugusana bali hata kwa njia ya hewa.
Maradhi haya hushambulia watu wa umri wote ingawa wazee na watoto wachanga hudhurika zaidi kutokana na maradhi haya. Mgonjwa hasa mtoto mchanga anapopata maradhi haya ni vyema kwa mzazi au mlezi kuhakikisha anampeleka kwenye kituo cha afya kwa ajili ya matibabu.
Maradhi haya kwa wengi yanayohitaji huduma ya dharura lakini ni vyema kuhakikisha kuwa mtaalam wa afya anachunguza ili kufahamu chanzo kabla ya matibabu.
Dalili
Maradhi haya huwa na dalili na miongoni mwake ni sehemu nyeupe ya jicho yaani sclera na ngozi ya ndani ya kope kubadilika rangi na kuwa nyekundu, macho kuwasha na kutoa machozi.
Baadhi ya wagonjwa huhisi kama vile macho yanaungua na baadhi hushindwa kuona vizuri, hii hutokana na kuvimba kwa sehemu ya ukuta wa mbele wa jicho yaani conjunctiva.
Dalili nyingine ni macho kutoa matongotongo kwa wingi hasa mgonjwa akiwa amelala kiasi cha kushindwa kuyafungua kutokana na wingi wake. Wapo wanaoshindwa kuona vizuri kwenye mwanga mkali.
Inashauriwa kumuona daktari wakati wowote moja ya dalili hizi zinapojitokeza au unapohisi jicho au macho yako hayako sawa ili kubaini tatizo na kulitibu kwa muda muafaka kabla athari zake hazijawa kubwa.
Mara baada ya kuona dalili hizi za maradhi, inashauriwa kumuona mtaalamu wa afya ambaye atasikiliza historia ya maradhi na kufanya vipimo ambavyo vitasaidia kugundua chanzo na kushauri matibabu yanayofaa.
Matibabu
Matibabu ya macho mekundu hutegemea chanzo. Kama chanzo cha maradhi ni bakteria basi daktari hupendekeza antibaiotiki (antibiotics). Dawa hizi huwa kwenye mfumo wa matone au za kupaka kwenye macho. Kutegemea na ukubwa wa maradhi daktari pia huweza kutoa vidonge.
Kama macho mekundu yamesababishwa na virusi, kwa bahati mbaya, huwa hakuna dawa ya kuyatibu. Habari njema ni kuwa kama ilivyo kwa maradhi ya mafua, mara nyingi maradhi ambayo husababishwa na virusi huisha yenyewe baada ya siku chache kwani kinga ya mwili huwa na uwezo wa kuua virusi hivi na hivyo mgonjwa kupona.
Endapo chanzo cha macho mekundu ni kemikali basi daktari atashauri mgonjwa aoshe macho na maji safi na kuhakikisha jicho au macho yanakuwa safi muda wote kwa kuyasafisha mara kwa mara mpaka atakapopata nafuu au kupona kabisa.
Wapo wanaougua kutokana na mzio. Kwa chanzo hiki, atatoa dawa za kupunguza madhara ya mzio ili kukabiliana maradhi husika.
Kinga
Kama yalivyo magonjwa mengi, zipo namna za kuepuka macho mekundu. Inashauriwa kuepuka kufikicha macho mara kwa mara kwani hii ni namna inayosambaa kirahisi zaidi ugonjwa huu.
Macho mekundu yanayosababishwa na virusi husambaa kwa haraka na kwa njia nyepesi zaidi. Kwa maana hii, ni vyema kwa wagonjwa kuhakikisha hawashikani mikono wala hawatumii vifaa vya kujiremba vinavyotumiwa na watu wengine.
Kwa wagonjwa, inashauriwa kuhakikisha wananawa mikono kwa maji safi muda wote ili kuzuia uwezekano wa kuwaambukiza watu walionao karibu.
Safisha macho yako kwa maji safi na salama mara kwa mara. Hii husaidia kuondoa vyanzo vya maradhi au kupona upesi kama umeshaambukizwa. Ni vyema kuhakikisha unaosha mikono mara zote unapomaliza kusafisha macho.
Kama unatumia vifaa vya urembo basi hakikisha mtu mwingine yoyote hatumii vifaa hivyo kwa wakati huo ili kuzuia kusambaa kwa maradhi hayo.
Kama unaweza kuvaa miwani maalum ya kuzuia mwanga mkali wa jua (wengi tunaita miwani ya jua) basi unashauriwa kuitumia ili kupunguza macho yasiumie zaidi.
Inashauriwa, usihamishe dawa ya macho kutoka kwenye jicho lenye maradhi na kuipeleka kwenye jicho salama kwani unaweza kuliambukiza wala kufikicha jicho lenye maambukizi halafu lisiloathirika.
Kwa wanafunzi, uongozi wa shule unatakiwa kumshauri mtoto kukaa nyumbani mpaka atakapopona ili kuepuka uwezekano wa kuwaambukiza wengine.
Madhara
Mara nyingi maradhi haya hayana madhara makubwa. Wagonjwa wengi hupona kabisa isipokuwa wachache ambao hupata makovu yanayobaki kwenye conjunctiva. Makovu haya husababisha changamoto ya kuona vizuri.
Kwa watoto wadogo ni vyema kuwapeleka hospitali mara tu mzazi au mlezi anapoona moja ya dalili zilizotajwa.