Tamthilia inayoonyesha nguvu katika sekta ya sanaa ya maigizo

Maprodyuza wa tamthilia ya Siri ya Mtungi (kushoto) wakiwa katika maandalizi ya utengenezaji wa moja ya kipande ‘scene’ cha tamthilia hiyo katika Ofisi za Media for Development International (MfDI) Msasani jijini Dar es Salaam
Muktasari:
- Inawania tuzo saba za chaguo la watazamaji Afrika kwa mwaka 2014
‘Ni tamthilia ya televisheni inayofurahisha, inayoonyesha maisha ya Cheche, mpigapicha mwenye bashasha na mmiliki wa studio ya kupiga picha ya Mtungi. Ana mke mrembo, Cheusi, aliyemzalia watoto wawili wenye afya, huku akiwa na ujauzito wa mtoto wa tatu,’ Hii ni sehemu ya kwanza ya tamthilia hiyo.
Wakati sehemu ya pili ya tamthilia hii ikitarajiwa kuanza kuonyeshwa Mei mwaka huu. Siri ya Mtungi imefanikiwa kuingia katika kinyang’anyiro cha tuzo maarufu za chaguo la watazamaji Afrika kwa mwaka 2014, tuzo zitakazotolewa Machi mwaka huu nchini Nigeria.
Siri ya Mtungi inawania tuzo katika vipengele saba vya Muongozaji Bora wa Sanaa, Mhariri Bora wa Sauti, Lugha Bora ya Asili, Tamthilia Bora, Mpambaji (Make up artist) bora pamoja na Mwigizaji Bora ambapo vipengele hivi vinazingatia nafasi ama ushiriki wa mtu mmoja mmoja na namna alivyotumia ujuzi wa ziada kufikisha kazi yake vizuri katika utengenezaji wa tamthilia hii.
Ushiriki wa tamthilia hii katika tuzo hizi za kimataifa pia ni ishara ya kutambulika na kukua kwa sanaa na wasanii wa maigizo kutoka Tanzania. Tuzo hiyo inayoitwa Africa Magic Viewers’ Choice Awards (AMVCA) au Tuzo za chaguo la watazamaji Afrika.
Sehemu ya pili ya tamthilia hii iliyojizolea umaarufu ndani na nje ya Tanzania ipo katika matengenezo na inatarajiwa kuanza kuonyeshwa tena ifikapo Mei mwaka huu, baada ya sehemu ya kwanza kuonekana kuanzia Desemba 2012.
Starehe ilifanikiwa kufika eneo ambalo tamthilia hii inayowania tuzo nne za AMVCA inatengenezwa na kushuhudia namna utengenezaji wa kitaalamu unavyofuatwa, sambamba na wasimamizi makini wa tamthilia huku vigezo na kanuni za uandaaji wa maigizo zikifuatwa.
John Riber ni Prodyuza na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Media for Development International (MfDI) Tanzania, anasema uamuzi wa kutayarisha tamthilia ya Siri ya Mtungi ya kiwango cha juu inayoongea moja kwa moja na watu wa Tanzania na Afrika Mashariki, una uwezo wa kuleta mapinduzi ya mtandao wa mawasiliano.
“Wakati ‘Media for Development International’ walipopewa jukumu na Kampuni ya Johns Hopkins Bloomberg School of Public Health Center for Communication Programs (JHU•CCP) kupitia Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) kutayarisha tamthilia ya televisheni, ilikuwa ni mwanzo wa jambo kubwa zaidi ya rasilimali fedha iliyokusudiwa.
“Tumekuwa na michezo mingi kama Wahapahapa, matangazo kadhaa ya redio na televisheni yakiwamo ‘Tupo Wangapi’ na sasa tamthilia ya ‘Siri ya Mtungi’ imeipeleka MFDI kwenye hatua nyingine. Siyo tu kuwa mradi huu umewapatia mbinu mpya na fursa wasanii, wanamuziki na wafanyakazi ambao ndiyo uti wa mgongo wa huu mtiririko wa maono wa Tanzania, lakini hadithi za hawa wahusika kwenye tamthilia hii ya televisheni zimeopolewa toka kwenye hazina ya watu milioni mia moja na hamsini wa Afrika Mashariki wanaozungumza Kiswahili,” alisema Riber.
Hata hivyo MfDI ina rekodi ya kutengeneza filamu zinazopendwa Afrika – kama vile Consequences, More Time (Poa Mambo Bado), It’s not Easy, Yellow Card, Chumo na Neria.
Utengenezaji wa filamu
Mratibu wa Uzalishaji Mathew Gugai huku akionyesha chumba kinachohifadhiwa nguo zilizokwishatumika chenye ukubwa wa mita 100 za mraba, alifafanua kwamba nguo hizo zilizowekewa nembo iliyoandikwa maelezo ya matumizi yake.
“Unaona kuna hizi karatasi ‘tag’ zilizoning’inizwa kwenye nguo, hizi zinamaanisha kwamba nguo hii imevaliwa kwenye kipande kipi ha tamthilia ‘scene’ na iwapo kuna mwendelezo (continuity) kumalizia kipande kilichobaki basi mhusika atalazimika kuivaa tena nguo hii na kumalizia kazi iliyobaki,” anasema Gugai na kuongeza kuwa nguo nyingi ni nyeusi kutokana na ubora wake kwenye kamera.
Gugai anaonyesha namna nyumba za kuigizia zinavyojengwa kwa kutumia mbao maalumu zilizopakwa rangi mbalimbali sambamba na picha, samani mbalimbali zinazoweza kutofautisha nyumba ya mwalimu na nyumba za watu wengine zinazoonekana ndani ya tamthilia hiyo.
Rehema Samo anayewania tuzo za mpambaji bora (make up artist) anasema anatumia akili kubwa, kuhakikisha anamtengeneza mhusika kutokana na kile kilichopo katika muswada (script).
Mmaliziaji na msimamizi wa muswada Pricilla Mlay, maarufu Cece, anasema kuna ukakasi sana katika uandaaji wa tamthilia hiyo hivyo wanatumia mtu wa mwisho kuikamilisha kazi, anatakiwa kuwa bingwa wa lugha ya Kiingereza na Kiswahili.
“Muswada umeandikwa katika lugha ya Kiingereza na tamthilia inaonyeshwa kwa lugha ya Kiswahili hivyo inahitajika mtu makini wa kuweza kutoa mwongozo unaofaa,” anasema Cece na kubainisha kuwa Siri ya Mtungi ina zaidi ya wafanyakazi 46 wanaotengeneza mandhari na waigizaji.
Tamthilia na wahusika
Siri ya Mtungi imewakusanya wasanii wengi akiwamo Cheche, maarufu Zoba, Yvone Cherrie ambaye anafahamika kwa jina la Lulu huku jina lake la kisanii likiwa ni Monalisa na wengineo.
Mhalifu wa mjini ni Masharubu, tajiri mwenye nguvu anayemiliki mabanda na biashara za kitapeli. Baada ya kuvumilia matusi kwa muda mrefu, mkewe alimkimbia na kumwachia binti yao mrembo anayeitwa Nusura. Nusura ni ua la yungiyungi lililochanua. Ni mjanja, mwanamke shupavu ambaye udhaifu wake ni uhusiano wake na Duma, mmoja wa wapangaji wa Masharubu. Duma ana moyo wa dhahabu (mtu mwema), lakini anahangaika kimaisha kama DJ mjini Bagamoyo.
Karibuni tu alimleta mdogo wake, Stephen, toka kijijini, ili mvulana huyo aingie shule ya kujitegemea na kupata fursa ya maisha bora lakini, mpaka muda huu Duma anashindwa kumtimizia mahitaji muhimu. Anashindwa kuwa mfano bora kwa mdogo wake, Stephen anayechoshwa na shule na kutaka kuwa ‘mtoto wa mjini’ kama kaka yake.
Nyendo za Nusura na Kizito zinapishana kuashiria bahati kwa Kizito, ambaye yuko tayari kuendelea mbele na maisha yake kutokana na kifo cha mkewe mdogo. Nusura kwa upande wake amechoshwa na wasiwasi katika uhusiano wake na Duma, hivyo yuko tayari kwa mambo ya kiungwana zaidi.
Nusura anajikuta yuko njia panda kati ya penzi la Duma na lile lililotulia kama maji lenye uelekeo wa ndoa na Kizito. Hana ufahamu wowote kuwa kuna dhoruba inayochemka kwani mke mdogo wa kizito amekufa kwa ugonjwa hatari wa Ukimwi.