Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Michezo ni sekta muhimu katika uhai wa Taifa letu

Muktasari:

Pia matatizo mengine ni utawala mbovu wa michezo nchini uliopo katika vyama vya michezo kwani watawala hao wanashindwa kutekeleza wajibu wao wa kuendeleza michezo, Serikali nayo haina Sera bora na mipango mizuri ya kitaifa ya kuendesha michezo vilevile hakuna muundo na utaratibu wa utawala mzuri wa kuendesha michezo nchini.

Yapo matatizo mengi ambayo yanazuia kasi ya maendeleo ya michezo nchini, ila wahusika wamekuwa wakiyafumbia macho na kuona kama ni masuala ya kawaida.

Matatizo yaliyopo katika sekta ya michezo siyo ya kawaida na kama hatutayaondoa, basi kila mwaka hatutafanya vizuri kimataifa na tutaendelea kuona michezo haina umuhimu katika uhai wa Taifa letu.

Ngoja niwaambieni Watanzania wenzangu, michezo ni sekta muhimu katika uhai wa Taifa, kama tutadharau hilo basi tujue tutaendelea kusababisha mamilioni ya Watanzania wanaotegemea michezo kwa ajili kuendesha maisha yao kuishi maisha ya dhiki.

Matatizo yanayozuia maendeleo ya michezo nchini yapo mengi na siwezi kuyataja yote katika uchambuzi huu ila matatizo mengine yapo wazi kabisa na mimi naamini sitakiwi kuyataja.

Ila baadhi ya matatizo ambayo naweza kuyataja ni uhaba mkubwa wa vyuo vya taaluma ya michezo na upungufu wa wataalamu wa michezo, kutofundishwa kwa somo la elimu ya michezo shuleni na kwenye vyuo, utunzaji na usimamizi mbaya wa viwanja vya michezo vilivyopo nchini, uvamizi wa viwanja vya michezo na burudani kwa watoto na upungufu mkubwa wa viwanja vyenye hadhi ya kimataifa.

Matatizo mengine ni ukosefu wa viwanda vya kutengenezea vifaa vya michezo nchini na gharama kubwa ya vifaa hivyo vitokavyo nchi za nje, wizara inayohusika na michezo kurundikiwa mambo mengi yasiyohusu michezo, ufinyu wa bajeti ya kuendeleza michezo, wananchi kukosa desturi ya kucheza kwa ajili ya afya zao na kushindwa kuwatumia wataalamu wachache wa michezo waliopo nchini.

Pia matatizo mengine ni utawala mbovu wa michezo nchini uliopo katika vyama vya michezo kwani watawala hao wanashindwa kutekeleza wajibu wao wa kuendeleza michezo, Serikali nayo haina Sera bora na mipango mizuri ya kitaifa ya kuendesha michezo vilevile hakuna muundo na utaratibu wa utawala mzuri wa kuendesha michezo nchini.

Hayo ni baadhi ya matatizo yanayokwamisha maendeleo ya michezo nchini na mimi naamini kabisa bila wanasiasa au Serikali kuisapoti michezo nchini au kampuni kujitokeza na kuwekeza kwenye michezo na viongozi wa michezo kukubali kutekeleza wajibu wao kikamilifu hatutaweza kuona mabadiliko kwenye michezo wala kufanya vizuri kimataifa kwani tuna matatizo mengi.

Lazima tukubali wachezaji nyota duniani katika mchezo wowote huandaliwa katika mazingira yatakayomuwezesha kuwa mchezaji nyota siyo kumuandaa mwanamichezo katika mazingira ya matatizo kama tuliyonayo hivi sasa nchini.

Ni wazi, tunatakiwa kujua umuhimu wa michezo nchini na kujua kuwa michezo ni kiungo muhimu, ni sekta muhimu kwa taifa kwa hiyo tuondoe matatizo yanayozuia umuhimu wa michezo.

Michezo ni muhimu kwani hujenga na kuimarisha afya, hujenga ushirikiano, upendo, udugu na uzalendo, hujenga taifa lenye nidhamu, uhusiano, uelewano, mshikamano, moyo wa kishujaa na kujihami, hukuza ukakamavu, ujasiri na kujiamini.

Pia umuhimu mwingine wa michezo ni kuwapatia wananchi burudani, kulitambulisha na kulitangaza taifa nje ya mipaka, kumjenga mchezaji kimwili, kiakili na kiroho na kutoa ajira pana hivyo ni chanzo muhimu cha mapato kwa Taifa.

Ili faida za michezo zipatikane nchini ni lazima kwanza tuwe na sera bora, malengo na mipango ya kuhakikisha tunaondoa matatizo ambayo ndiyo vikwazo vya mafanikio kwenye michezo.

Naamini huu ndiyo wakati muafaka wa kulikwamua taifa letu katika janga la kukosa maendeleo ya kimichezo kwa kuitambua sekta ya michezo ni muhimu katika uhai wa Taifa letu kiuchumi, kijamii na kisiasa.