Maalim Seif: Siwezi kamwe kurudi CCM hii ya sasa

Maalim: Sikuamua kuja upinzani, bali CCM walinisukuma kwenda upinzani. Kama wanavyofanya sasa kwa Mansour (Yussuf Himid), they do the same thing (wanafanya kitu kilekile) na Mansour anapitia process (njia) hizohizo. Mimi nimefukuzwa CCM na zikatafutwa sababu nikawekwa ndani bila kosa lolote.PICHA|MAKTABA
Muktasari:
Mfumo haukufafanuliwa vizuri katika Katiba. Katiba yetu imefafanua tu kwamba rais, makamu wake na mawaziri watapatikana vipi na kwa uwiano upi, lakini baada ya hapo kwenda chini Katiba haikueleza.
Ni mengi yamesemwa kuhusu mwanasiasa huyu, Maalim Seif Shariff Hamad ambaye kwa sasa ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar. Yeye, ameshikilia nyadhifa mbalimbali tangu akiwa chama tawala, CCM hadi sasa akiwa Chama cha Wananchi (CUF). Ni nini zaidi anacho Maalim Seif? Endelea…
Swali: Unapoelekea kumaliza kipindi chako cha uongozi katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), ni changamoto gani umezipata?
Maalim: Tukumbuke kwamba Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ni mfumo mpya katika nchi yetu na hata katika kura za maoni kuwauliza Wazanzibari waukubali au waukatae, wapo walioukataa. Waliukataa kwa hofu tu maana mara nyingi ukianzisha jambo jipya watu wengi lazima wawe na hofu. Bahati nzuri, asilimia 66 wakakubali mfumo huu.
Tumeanza vizuri na tumepata mafanikio, lakini na changamoto zipo. Changamoto ya kwanza ni mfumo kuzoeleka kwa watu, watu kujua serikali hii itaendeshwa vipi. Walizoea chama kimoja kuongoza serikali, walihoji katika Baraza la Wawakilishi mambo yatakuwaje, na wapo waliodhani kuwa hatutafanikiwa.
Nashukuru chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na busara zake tumeweza kwa kiasi kikubwa kushinda changamoto nyingi.
Katika ngazi ya kitaifa, hasa katika uhusiano wa kikazi kati ya rais, makamu wake wawili na mawaziri uhusiano ni mazuri, tunapata tatizo tunapoanza kuteremka ngazi za chini.
Katika ngazi za chini watu wamezoea mfumo wa chama kimoja ambapo kila kitu ni CCM, kwa hiyo wengine wanaona shida kwamba tuna kiongozi kutoka CUF, lakini lazima ukubali hali halisi.
Mfumo haukufafanuliwa vizuri katika Katiba. Katiba yetu imefafanua tu kwamba rais, makamu wake na mawaziri watapatikana vipi na kwa uwiano upi, lakini baada ya hapo kwenda chini Katiba haikueleza.
Ukiangalia ngazi za chini wengi wanaoteuliwa, pamoja na wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ambao wameteuliwa kwenye siasa, bado ni wanachama wa CCM na bado ni wajumbe wa kamati za siasa za CCM. Haya ni mambo ambayo tumeyaona na lazima tuyarekebishe.
Utakuta mkuu wa mkoa au wilaya anakwenda katika kikao cha CCM na anajisahau kabisa kuwa ni kiongozi wa serikali na hatakiwi kwenye siasa. Tumepata matatizo na masheha ambao ni kikwazo kikubwa kwa mafaniko ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na wanaona wao ni mawakala wa CCM na siyo watu wa Serikali.
Swali: Ulijisikiaje siku CCM wanakufukuza uanachama?
Maalim: Sikuamua kuja upinzani, bali CCM walinisukuma kwenda upinzani. Kama wanavyofanya sasa kwa Mansour (Yussuf Himid), they do the same thing (wanafanya kitu kilekile) na Mansour anapitia process (njia) hizohizo. Mimi nimefukuzwa CCM na zikatafutwa sababu nikawekwa ndani bila kosa lolote.
Mansour hakutoka CCM, Mansour wamemfukuza CCM na kisa cha kumfukuza ni kitendo cha kuunga mkono mfumo wa serikali tatu na baada ya kufukuzwa akaona watu walio karibu na msimamo wake ni CUF, lakini hajajiunga na CUF. Lakini, kwenye mikutano ya CUF anakuja na kuhutubia, sasa wamemtia ndani, ila ipo siku watamtoa, lakini wamemfanya kuwa shujaa, they create heroes themselves (wao wanatengeneza mashujaa).
Nakumbua Mwalimu aliwahi kuulizwa na redio moja ya Ujerumani kwamba ana regret (anajutia) mambo gani mawili aliyoyafanya; akasema moja ni kuitambua Biafra na la pili ni kuwafukuza kina Seif, CCM. Usalama wa Taifa kutoka Bara ulimwambia Mwalimu usifanye makosa ya kuwafukuza hawa, usalama kutoka Zanzibar wakamwambia Mwalimu wafukuze na ndio utakuwa mwisho wao watapigwa mawe barabarani.
Kikao cha Dodoma kilichoitishwa kutuhukumu sisi kilikwenda mpaka saa 6.00 za usiku sababu siku ya pili Mwalimu Nyerere alikuwa anaondoka hivyo ilikuwa lazima tufukuzwe.
Mimi kufukuzwa hakuniuma na nikasema nitakuwa huru kwa sasa kuangalia mwelekeo wangu na hasa nilipoona nimepata support (siungwi mkono) ya Wazanzibar wengi. Never give up (kamwe usikate tamaa).
Swali: Kuna siku tutarajie unaweza kurudi CCM?
Maalim: CCM yenyewe hii! Hii siyo ile CCM yetu sisi ambayo Mwalimu alikuwa mwenyekiti, mzee Kawawa, katibu mkuu huku sekretarieti ikiwa na Kingunge Ngombale Mwiru, Salim Ahmed Salim, Mosses Nnauye na Alfred Tandau. Hiyo ndiyo ilikuwa CCM bwana. Siyo CCM hii ya sasa ya akina Nape.
Swali: Unafikiri mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa unaweza kufaa katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano?
Maalim: Wala sina shaka yoyote na wala hakuna suluhisho. Kwa mivutano iliyopo Tanzania Bara sioni suluhisho jingine isipokuwa tukubali kwamba lazima tufike mahali tufanye kazi pamoja. Faida moja ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni kuunganisha vipaji vya watu wengi.
Vipaji vipo katika nchi na ukiviunganisha kila mmoja anaona kuwa this is my government (hii ni serikali yangu). Watu wasiwe na wasiwasi kwamba Bunge litakuwa butu, si kweli sisi tuna uzoefu wa Baraza la Wawakilishi ambalo hivi sasa lina meno zaidi kuliko pale ambapo hatukuwa na upinzani.
Kwa sababu nini; mkiwa na vyama viwili, kinachoongoza serikali na cha upinzani, chama kinachoongoza serikali watakuja kutetea serikali yao hata kama watajua kama hii sera si sahihi.
Lakini, uzoefu tuliopata kwenye Baraza la Wawakilishi wao wanajua kuibomoa serikali tu na hawajui kama ni waziri kutoka chama changu. Wao wanachojua huyu ni waziri kafanya kosa na kuna upungufu wanasema wazi na wakati mwingine hupigwa kura na serikali huwa inakaribia kushindwa. Hata debate (mijadala) inakuwa mikali katika Baraza la Wawakilishi. Zanzibar hivi sasa kukiwa na Bunge na Baraza la Wawakilishi, majority people (watu wengi) wanasikiliza Baraza la Wawakilishi kutokana na kuwa na mijadala mizito.
Kwa hiyo nadhani hili ni suluhisho la matatizo na mivutano hasa kwa Tanzania Bara na tusisahau kwamba mambo yakifanikiwa Zanzibar na Bara yatafanikiwa pia.
Swali: Mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa unajumuisha vyama viwili vya siasa ndani ya serikali moja, kwa kuwa kila chama kina ilani yake ya uchaguzi, ni ilani ya chama kipi inayotumika?
Maalim: Hilo ni moja ya tatizo ambalo hatukulitazama vizuri wakati tunaandaa mawazo ya kufanya kazi pamoja na kwa sasa unatumika uzoefu tu kwamba rais ndiye mwenye mamlaka ya kutoa sera ya serikali, sasa rais anaongozwa na sera ya chama chake.
Niseme kwamba Rais (Dk Shein) alipochukua serikali alichokifanya wakati akilihutubia Baraza la Wawakilishi alieleza mwelekeo wa serikali yake kwa miaka mitano, yapo mambo alitoa katika ilani ya CUF.
Sasa tunapata matatizo katika utekelezaji kwa sababu CCM wanataka kila jambo la mafaniko lionekane limetokana na ilani yao, lakini jambo lililoshindwa hawasemi. Kuna mambo ambayo yalikuwa katika ilani ya CUF yametekelezwa vizuri.
Tunachoangalia mbele zaidi ni kuchukua mifano ya nchi nyingine ambazo ziliunda serikali na kuunda kamati ndogo ambayo inaangalia ilani zote mbili halafu wanachukua mazuri kutoka katika ilani zote mbili na kuyaunganisha katika kitu kinachoitwa minimum program. Serikali inasimamia minimum program (mipango michache) kwa hivyo tunadhani mbele ya safari tutaelekea huko.
Swali: Kuna madai kuwa ushirikiano wa CUF na CCM Zanzibar unadhoofisha upinzani, kuna ukweli wowote katika madai haya?
Maalim : Hata siku moja, kwanza watu wanaosaidia sana kujenga chama katika Baraza la Wawakilishi ni wawakilishi wenyewe. Wawakilishi wetu wa CUF wana sauti (they are very vocal) na wanazungumza kwa hoja na hata wananchi wengi wakiwa na matatizo yao wanawaendea wawakilishi wa CUF ili wawasemee katika Baraza la Wawakilishi.Pili, sisi siyo kwa sababu tupo katika serikali tutakaa tu, tunaendelea kufanya mikutano ya hadhara na kuendeleza sera zetu.
Swali: Kwa nafasi yako ya Makamu wa Kwanza wa Rais, unaweza kuichambua serikali kama ilivyokuwa awali?
Jibu: Unakuwa umefungwa kwa sababu upo ndani ya serikali kwa hiyo criticism zako zote unatakiwa uzitoe mnapokutana katika cabinet (baraza la mawaziri).
Sasa, kutokana na majukumu yangu inakuwa vigumu kutoka nje na kuanza kuipinga serikali.
Niliwahi kufanya mara moja tena kwa sababu maalumu. Baada ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Bububu, mimi sikuwepo, ila niliporudi nikakuta hali mbaya na watu wanateswa na kupigwa, kwa kweli sikuvumilia nilisema hadharani na kukemea. Nina ruksa ya kuzungumza na Rais muda wowote na hata kuzungumza na Makamu wa Pili wa Rais kwa sababu yeye ndiye msimamizi wa shughuli za rais za kila siku na pale mambo hayatakwenda vizuri namwambia makamu hapa look at it (hebu liangalie hili).
Swali: Kwanini Chama cha CUF siku zote kipo chini ya CCM licha ya kuwepo kwa madai kuwa CUF huwa kinashinda katika Uchaguzi Mkuu?
Maalim : Binafsi, maslahi ya wananchi yapo juu zaidi kuliko maslahi yangu binafsi, nikihisi naweza kuchukua uamuzi, lakini watu wengi wakapoteza maisha yao huwa nina sacrifice (najitoa) kuliko kuwaambia watu waingie barabarani. Najua wazi kuwa vikosi vimeshapewa amri ya piga ua, sasa kwa nini upoteze maisha ya watu 10 au 20 kwa kuingia madarakani tu?
Utafika wakati nitapata free and fair election (uchaguzi huru na wa haki) na uamuzi wa wananchi utaheshimiwa na tunaelekea huko sasa hivi.
Soma mahojiano zaidi Ndani ya habari katika toleo letu la kesho
Swali: Unaamini vipindi vyote ulivyogombea urais Zanzibar ulishinda?
Maalim: Hiyo haina mjadala na Wapemba wanasema hiyo haina ‘kitochi’.
Swali: Katika uchaguzi mara zote nne ulizoshiriki ni uchaguzi gani unaoamini kuwa ulishinda bila kitochi?
Maalim: Uchaguzi uliopita, yaani wa mwaka 2010 nilishinda. Hata matokeo yalivyotangazwa walisema Rais Shein kanipita kwa kura 3,000 lakini kuna watu zaidi ya 18,000 ambao wamenyimwa haki ya kupiga kura na more than 80 per cent of them (zaidi ya asilimia 80) ni supporters (mashabiki ) wa CUF.
Swali: Nini mikakati ya CUF kushinda Uchaguzi Mkuu mwaka 2015
Maalim: Sasa hivi tunajipanga vizuri na wiki iliyopita wajumbe wa Kamati ya Utendaji kutoka Zanzibar tulijifungia kwa siku nne kupanga mikakati madhubuti kabisa wa kuhakikisha zile kasoro zote za nyuma hazirudi na kuhakikisha kuwa haturudii makosa. Kuna baadhi ya maeneo hatukuwa mawakala wa kutosha.
Swali: Ungetamani rais ajaye wa Tanzania awe na sifa zipi?
Maalim: Rais ni rais. Rais, kwanza awe na uwezo wa kuunganisha wananchi kwa sababu huyu ni rais wa Watanzania wote, wale waliompigia kura na wale waliompinga, akishachaguliwa yeye ni rais wa wote.
Jukumu lake la kwanza ni kuwaunganisha wananchi wote na aonekane wazi kuwa yeye ni rais wa watu wote na hana upendeleo. Ukishakuwa rais pamoja na kuwa na chama chako, lakini chama kwanza kinakaa pembeni, kwanza uwatumikie Watanzania.
Pili, rais ambaye atakuwa karibu na wananchi kwa sababu sifa ya uongozi ni kujua hali halisi ya wale unaowaongoza na huwezi kujua hali halisi kama hauko karibu nao.
Tatu, rais lazima awe na maamuzi, awe very strong (awe thabiti) katika uamuzi. Sisemi uwe dikteta, una vyombo vyako una cabinet (baraza la mawaziri) na kila kitu lakini kama rais mimi nina malengo yangu. Una mawaziri wako na kila waziri unamwambia mimi nataka katika sekta yako tu- archive this (kufanikisha hiki). Waziri anakaa na kupendekeza kwenye cabinet mnajadili katika cabinet the best way (njia mwafaka) kufikia pale ambapo mnataka kufika.
Rais lazima ujue hili linatufikisha hili halitufikishi na ukishachukua maamuzi yasimamie mpaka mwisho na usiyumbe tena.
Pia, rais lazima awe na msimamo na anayekubali kushaurika pamoja na Katiba kusema kuwa yeye ndiye mwenye uamuzi na halazimiki kufuata ushauri wa mtu yoyote lakini lazima ashaurike
Jambo jingine muhimu, rais asimamie institution (taasisi) na akubali kabisa kuna executive (watendaji) ina madaraka yake, legislature (bunge) ina madaraka yake na judiciary (mahakama) ina madaraka yake na wasiingiliane hata kidogo na hizi ni checks and balances.
Kuwa na institution hata ukiwa na rais bogus (ovyo) mambo yanakwenda. Marekani anybody (yeyote) leo mweke pale Serikali itakwenda, why? (kwa nini) , kwasababu ya strong institution (taasisi imara).
Rais anayekuja tunamtaka aweze kusimamia na kujenga institution.
Swali: Madai kwamba rais awe kijana au mzee yana msingi gani katika siasa?
Maalim: Nasema kwamba kuna mwelekeo na uzoefu mbalimbali kutoka nchi tofauti. Ukweli ni kwamba majority (wengi ) ya wananchi wa Tanzania ni vijana na tukubali kwamba vijana wa sasa ‘vijana wa dot com’ (kizazi kipya) ni tofauti na vijana sisi, lakini vilevile tunahitaji uzoefu.
Kwa hiyo mimi kuliko ku-base (kuegea) katika ujana au uzee, nasema aangaliwe mtu mwenye uwezo wa kushika mamlaka ya rais na anaweza kuwa kijana au mzee as long as (ambaye) ana uwezo wa kusimamia shughuli za serikali.
Akiwa kijana asiweze ku-ignore (kudharau) mawazo ya wazee na aki-ignore (akifanya hivyo) ataharibikiwa na akiwa mzee lazima ajue matatizo ya sasa ya vijana ni nini.
Mimi zaidi naliangalia uwezo kuliko age (umri), unajua nchi kama China sasa hivi kidogo wame- reform (wamebadilika), lakini hata hivyo rais wao na Waziri Mkuu hawi chini ya miaka 50. Unajua wakati mwingine vijana wanakuwa na jazba na kazi ya urais inatakiwa uwe makini kabisa na don’t be carried by (usiongozwe) jazba, zaidi ni busara, hekima na utaalam.
Swali: Mtizamo wako ni nini kuhusu rais kupokezana kutoka kila upande wa Muungano?
Maalim: Nadhani kama ni Muungano wa nchi mbili, lazima kuwe na system (mfumo) ambapo tunajuana kabisa kwamba kipindi hiki rais atatoka upande huu na kipindi hiki rais atatoka upande huu.
Haiwezekani kama ni nchi mbili zilizoungana halafu kila siku rais ni nyinyi tu, na nyinyi kila siku ni makamu tu hapana, lazima kuwe na system iandikwe vizuri, if this ten years (ikiwa kwa miaka kumi) rais ametoka bara, another ten years (miaka mingine kumi) anatoka Zanzibar, nadhani ni fair (sawa).
Swali: Kwa muda mrefu umekuwa kiongozi wa CUF, unadhani uking’atuka kuna watu sahihi wa kuchukua nafasi yako?
Maalim: Katiba ya CUF iko very open (iko wazi) kwamba mwanachama yeyote anaweza kugombea nafasi yoyote. Mimi wakati wa kuchukua fomu nilikuwa wa mwisho kabisa na Profesa Lipumba alichelewa kuchukua fomu kwa sababu ya kuacha nafasi watu wasione kama anagombea Lipumba.
Wakati mwingine watu wana uwezo lakini wakiona Maalim Seif na Profesa Lipumba wamechukua fomu wana-respect (wanaheshimu) na kuona kwamba bado tunaweza kuongoza hivyo wanaacha kuchukua fomu.
Mimi nikifa leo atapatikana Seif kuliko mimi wa kuongoza CUF, vijana wapo tunawa-prepare (tunawaanda) na wako madhubuti mimi ninawamini sana, Kamati ya utendaji, Baraza Kuu majority (wengi wao) ni vijana kutoka Zanzibar na Bara.
Swali: Mchakato wa Katiba umewagawa Watanzania, hivi ungekuwa na mamlaka ya juu ya nchi ungechukua uamuzi gani kunusuru huu mchakato?
Maalim: Katika hili sipendi kutafuna maneno na mtu ambaye anaweza kunusuru mchakato huu ni Rais. Suala la kuangalia ni kwanini huko nyuma Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) walikuwa na confidence (walimwamini) na yeye, mnakumbuka wakati wa kutunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, wakati wa kufanya marekebisho walikuwa wanakwama, lakini Rais (Kikwete) anawaita na anawasikiliza na anawaita CCM wanakaa pamoja kutafuta suluhisho, sasa nini kimetokea ni ile kukubali kushawishiwa na chama chake.
Chama kimeshawishi, kwa sababu mwanzo kanuni zilivyotungwa kwanza alikuwa anakuja rais kulizindua Bunge Maalum la Katiba, halafu ndio anakuja Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwasilisha rasimu, lakini wao wakaibadilisha na kulazimisha lazima kwanza aje Warioba na walitaka kumpa one hour kuzungumza.
Mtu ambaye katembea Tanzania nzima kuchukua mawazo ya Watanzania wengi unampa one hour (saa moja), halafu anakuja Wako (Amos, Mwanasheria Mkuu (AG) mstaafu wa Kenya) unampa the whole day (siku nzima).
Kulikuwa na mvutano mkubwa na mpaka wapinzani wakatishia kugoma lakini baadaye walikubaliana kwamba Jaji Warioba apewe four hours (saa nne), lakini aje mwanzo kabla ya Rais.
Sasa, Rais haikuwa jukumu lake kuja ku -criticize (kukosoa) aliyosema Warioba. Nakumbuka alivyozungumza na Baraza la Vyama vya Siasa alini- impress (alinifurahisha) sana, Rais Kikwete kwa sababu alizungumza as a state man (kama mkuu wan chi) na hakuegemea upande wowote na akasema waziwazi kwamba wala tusidhani wingi ndiyo utapitisha Katiba, Katiba ni maridhiano.
Sasa what happened (nini kilichotokea), anafungua Bunge la Katiba anachukua moja wa moja msimamo wa chama chake, pale ndipo mambo yalipoanza kuharibika.
Lakini, nasema pamoja na hayo yote mimi nasema bado anayo opportunity (nafasi) kwa sababu Ukawa wanachotaka ni kuhakikisha kuwa tunakwenda katika Bunge kujadili rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Swali: Bunge la Katiba linaendelea na Ukawa hawaendi, mfano Rais asipoingilia kati tutegemee Katiba Mpya?
Maalim: Wanaweza waka-force (kulazimisha), lakini hata hiyo Katiba wanayopitisha wao kama wakifuata sheria inavyotaka hawatapata theluthi mbili ya wabunge kutoka Zanzibar. Kwa hiyo ni kupoteza fedha za umma, sasa hivi shughuli nyingi za serikali zimesita kwa sababu ya mchakato wa Katiba.
Ndiyo maana nikasema tunataka Rais ambaye atakuwa wa Watanzania wote na lazima a consider (afikirie) kwamba hawa Ukawa wana point (wana hoja) wasingetoka. Rais ni mtu mzima si lazima aje atake radhi, lakini kuna lugha ya kiutu uzima atasema na watu watamwelewa bila kutaka radhi. Ukawa wanachotaka ni kuhakikishiwa kuwa inajadiliwa rasimu ya Warioba.
Swali: Kwa dhamana uliyo nayo hujawahi kupata nafasi ya kushauriana na Rais kuhusu jambo hili la Katiba?
Maalim: Baada ya Ukawa kutoka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu alinifuata na kuniomba busara zangu, lakini nikamwambia busara katika mazingira ambayo busara zimeshaharibika haziwezi tena kutengenezwa hapa.
Lakini, maoni yangu yakawa haya haya, kubwa ni ku compromise na hawa Ukawa muone jinsi gani mnaweza ku- accommodate matakwa yao kuliko ku- insist kuwa sisi si majority hatuwezi kufika mahali.
Usisahau kwamba Katiba ni maridhiano hata hao wachache wana haki zao na wanawakilisha wengi katika nchi, hiyo ndio ilikuwa first step (hatua ya awali) iliyochukuliwa.
Second step (hatua ya pili), tulijaribu sisi kama viongozi wa Zanzibar (sisi watatu) kukaa na kuzungumza how we can help (ni jinsi tunaweza kusaidia), lakini hatimaye suala la serikali mbili au tatu likaibuka na hatukupata solution (suluhisho).
Niseme kwamba anytime (muda wowote), Rais Kikwete akisema tuzungumze I am prepared (niko radhi, tayari) na nitampa general view (mtazamo wa jumla).
Swali: Kwanini wewe usianze kumtafuta?
Maalim: Sasa, nikianza mimi wakati nimeanza kuzungumza na wenzangu, Dk Shein na Balozi Seif nitaonekana kama ninatapatapa.
Swali: Ukawa mtaachiana majimbo mwaka 2015?
Maalim: Final decision (uamuzi wa mwisho) haijachukuliwa bado, lakini maoni yaliyopo Ukawa waende beyond Katiba (mbali zaidi), kwamba tuone jinsi tunavyoweza kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu unaokuja, lakini hili nataka liwekewe mikakati yake kwa sababu huko nyuma tulishajaribu, lakini tukaachana njiani sasa hatutaki tena hayo yatokee na tuliachana njiani kwasababu hatukujiandaa vizuri.
Lazima tufanye uamuzi na tujue formula (kanuni) ipi tutaitumia na tukubaliane, mimi nadhani itasaidia sana.
Swali: Mmoja wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba alikutuhumu kwamba miaka ya ‘80 ulimchongea Mzee Abdu Jumbe kwa Mwalimu Nyerere kwamba alitaka serikali tatu na baadaye walimshughulikia. Awali, CUF mlitaka serikali ya mkataba, lakini baadaye mkabadilika na kutaka serikali tatu, kama uliona serikali tatu ni tatizo leo hakuna utata wowote?
Maalim: Sikupinga serikali tatu wakati wa Jumbe. Wakati ule Wazanzibari katika chama walikuwa divided (wamegawanyika), kuna ambao walikuwa waasisi, wakijiita liberators (wakombozi) na hawakutaka mabadiliko yoyote kabisa na hata Mzee Abdu Jumbe alipoleta Katiba ya mwanzo liberators waliipinga. Sisi vijana tukijiita front liners (msitari wa mbele) hata katika kugombea nafasi za NEC kutoka Zanzibar makundi haya mawili yaligongana.
Liberators walikuwa wamepanga kuhakikisha kwamba front liners hawaingii katika NEC hasa kwa kutumia wenyeji wao lakini bahati nzuri wajumbe wa Mkutano Mkuu kutoka Bara waliangalia uwezo wa mtu na finally mwishowe) , front liners walikuwa wengi zaidi katika NEC kuliko wao.
Sasa hii iliwashtua liberators na wakahisi vijana wanaingia watachukua nafasi zao na walimlaumu sana Rais Jumbe kwanini alituridhia sisi katika serikali wakati ni vijana.
Na ndio sisi vijana tumemsaidia Rais Jumbe kupitisha Katiba ya kwanza sababu wote tulikuwa tunataka mabadiliko. Fitna zikaanza na Jumbe akaambiwa vijana hawa itafika wakati watakuondosha na wewe.
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa chama uliofanyika Chamwino, Dodoma, Abdu Jumbe akaitisha kikao kwa wajumbe wote wa NEC, wa Unguja wa Unguja wa Pemba kwa Pemba, na hotuba yake ndiyo iliyotushtua sisi na alimalizika kwa kusema lazima twende kwenye revolutionally justice (mapinduzi ya haki) na tulikuwa na kumbukumbu ya watu kupoteza maisha katika siku za nyuma.
Alivyosema hivi tukasema hapana hili jambo haliwezekani, mimi, Dk Salmin Amour, Dk Salim Ahmed Salim na wakateuliwa wajumbe wa sekretarieti ya NEC tukakutana na tukasema tuna jukumu la kuwalinda Wazanzibari na kuamua kama ni revolutionally justice, lazima tujue what is behind it (nini siri yake).
Tukaenda kwenye sekretariet tukalizungumza vizuri, wakati ule Mzee Rashid Kawawa ndiye Katibu Mkuu wa chama, CCM alituambia tukamweleze mwenyekiti, yaani Mwalimu Nyerere ambaye alisema kiitishwe kikao maalum cha Halmashauri Kuu ya Taifa.
Sasa kwa sababu liberators walishindwa kutuzuia kuingia katika NEC ndipo walipokuja wakati ule na kutumia suala la serikali tatu ili kutimiza malengo yao. Sisi tukasema hapana, nakumbuka Edward Sokoine (marehemu) alimwambia Mwalimu Nyerere kwamba vijana hawa wakipoteza maisha you are responsible (utahusika) na akataka kuachiwa jambo hilo ili yeye awe responsible (awajibike).
Ilipoitishwa NEC yakaja mambo mengi sana pamoja na mpango ambao ulikuwa umeandaliwa wa kudai serikali tatu.
Hatukupinga principle (kanuni) za serikali tatu na mpaka leo ukiniuliza nitakuambia kuwa nataka Serikali ya Mkataba, lakini baada ya Warioba kupendekeza mfumo wa serikali tatu uliotokana na maoni ya wananchi niliyaheshimu.
Swali: Nini maana ya Serikali ya Mkataba?
Maalim: Ni kwamba Tanganyika inakuwa na serikali yake with full authority (yenye mamlaka kamili) na Zanzibar ina serikali yake na mnakaa pamoja na kuona mambo gani tuyaendeshe pamoja.
Mnaorodhesha mambo ambayo kwa maslahi yenu ni lazima myafanye kwa pamoja. ni vigumu kusema muungano usiwepo maana miaka 50 si kidogo na watu wameshaoana sana.
Kinacholalamikiwa ni Wazanzibari kubanwa na koti la Muungano na kinachotakiwa ni kupimwa upya na kupatikana koti ambalo halimbani mtu.
Swali: Kuna jambo gani ambalo limekuumiza tangu ulipojikita katika siasa?
Maalim: Wakati damu inanichemka wakati mwingine nilikuwa too emotional (nina jazba) na sikuwa nikificha hisia zangu, niliweza kumjibu mtu yoyote awe Mwalimu Nyerere au mtu yoyote na si kujibu kwa ujeuri na kutukana, nilikuwa nikijibu kwa hoja.
Nakumbuka siku moja katika Kamati Kuu tulikuwa tukizungumzia masuala ya fedha na madeni na ikaja hoja kwamba Zanzibar inadaiwa na Mwalimu akasema lazima Zanzibar walipe.
Nikamwambia Mwalimu, samahani tena samahani sana, wewe umetoa kauli kwamba hauko tayari kuona Watanzania wanakufa ili ulipe madeni na sisi Wazanzibari hatuko tayari kuona Wazanzibari wanakufa kulipa madeni na wakati huo katika Kamati Kuu nilikuwa Mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango ya chama.
Hali ilikuwa mbaya mpaka rais wangu Mzee Idrisa Abdulwakil (marehemu) akaniambia chief (mkuu) hapa tumeshakwama, na yeye akapendekeza kwamba tumuombe Mwalimu Nyerere hili suala tuachiwe sisi Zanzibar tulizungumze harafu tulete majibu. At that time I can say anything. ( Kwa wakati ule ningeweza kusema chochote)
Swali: Ungetamani mambo gani yafanyike na kukupa raha?
Maalim: Hakuna jambo linaloniudhunisha kama kuona maisha ya watanzania wanavyoishi hasa ukienda vijijini. Rais lazima awe karibu na watu wake na ukienda vijijini kuona maisha wanayoishi wananchi halafu ukaja Oysterbay ukaona ma- palace (mahekalu) inanisononesha sana. Kumbe nchi hii ni tajiri lakini tatizo ni jinsi utajiri huu unavyoweza kumnufaisha kila mtu.
Swali: Unafikiri tatizo ni nini?
Maalim: Ukweli ni kwamba yale malengo ya kupigania uhuru tumeyasahau ambayo yalikuwa wazi kabisa kwamba aondoke mkoloni tujiletee maendeleo, ndio malengo ya Afro Shirazi na TANU.
Wakati wa Mwalimu Nyerere tulifuata hayo. Lakini, hivi sasa viongozi tunajali maslahi yetu sisi wenyewe. Hasa lilipokuja suala la madini tunaingia mikataba hovyo na Tanzania hainufaiki na inafaidika kampuni.
Huwa napenda kutolea mfano katika mikutano ya hadhara kwamba sisi tumekuwa kama kivuli cha mvumo ambao majani yake yapo juu sana, ukiwa chini yake hunufaiki, lakini ukiwa mbali ndipo unafaidika na kivuli. Watanzania hatunufaiki na wanaonufaika ni wageni, policy (sera) na sera zetu hazikuangalia maslahi ya wananchi.
Swali: Kitu gani kilichokufurahisha?
Maalim: Hakuna jambo linalonifurahisha kama la maridhiano ya Zanzibar. Ule uhasama uliokuwepo wa watu kupigana haupo tena hivi sasa kila mtu na chama chake lakini tunafanya kazi kwa pamoja.
Swali: Huoni kama uhasama unaweza kurudi kutokana na tetesi zilizopo kwamba Pemba wanataka kupunguza majimbo na Unguja waongeze majimbo?
Jibu: Hizo ni rumours (uvumi) tu, sasa hivi Tume ya Uchaguzi Zanzibar ipo katika process (mckato) ya kukusanya maoni ya wananchi juu ya ugawaji upya wa majimbo. Vyama ndivyo vya kwanza kupewa nafasi ya kutoa maoni, tumeshatoa na wametupa muda mpaka mwezi Septemba kama kuna jambo lililobaki. Ninaamini tume watayazingatia maoni ya wananchi.
Wanaosema tupunguze majimbo Pemba wana-base (wanatumia kigezo) juu ya population (idadi ya watu), tu lakini Katiba inasema kuna mambo mengi, kuna njia za usafiri, suala la mazingira ya miji na vijiji, kuna suala la hali ya maisha ya watu. Kuna combination of things (mkusanyiko wa vitu) na sio kuangalia jambo moja tu.
Swali: Muungano wetu una shida gani kubwa?
Maalim: Shida yake kubwa ni Tanganyika kuvaa koti la Muungano. Ikilivua koti hilo mambo yatakuwa sawa.
Swali: CUF ilipoanza ilikuwa na nguvu Zanzibar na Bara, lakini kwa sasa haina nguvu upande wa Bara, kuna mikakati gani ya kuirejesha katika chati?
Maalim: Ni kama kupokezana tu, ilikuwa NCCR-Mageuzi, lakini ikarudi nyuma, ikaja CUF lakini baadaye ikarudi chini, ikaja Chadema lakini nayo isipoangalia itarudi chini.
Kule Zanzibar CUF ina nguvu ile ile, kwanza Zanzibar ni ndogo na Wazanzibari wamechoka na utawala wa CCM na wanaona hawana mbadala mwingine zaidi ya CUF, kule kazi kidogo ni rahisi, huku kazi ni kubwa kwasababu ndugu zetu bado hamjaelimika vizuri katika masuala la kisiasa.
Siwezi ku imagine (kufikiria) mtu miaka mitano anapata taabu unafika uchaguzi anapelekewa chumvi, kanga anabadilisha mawazo kwa usiku mmoja tu wakati amesota miaka mitano. Mzanzibari anachukua fedha zako na atapiga kura anapotaka mwenyewe.
Tuna tatizo watu wa Bara, tunahitaji kuwaelimisha Wabara ndio maana kuna tofauti kati ya mijini na vijijini. Vyama vya upinzani vina nguvu mijijini kwa sababu tayari watu wameelimika, lakini vijijini kazi bado ipo.
Bahati mbaya, sisi wapinzani hatufiki vijijini kwa sababu ya ukosefu wa fedha. CUF ruzuku yetu ni Sh116 milioni, just imagine (hebu fikiria) utakwenda wapi kwa hivyo tuna upungufu wa resources (rasilimali) kuwafikia watu, ambao ukiwaelemisha wanaelimika.
Swali: Ni jambo gani ambalo hatujakuuliza ungepende kulizungumza?
Maalim: Lazima katika masuala la kitaifa tuongozwe na utashi wa maslahi ya taifa na tuache hizi ego (nafsi) za kibinadamu. Watanzania wana maisha magumu na wame-suffer (wameteseka) vya kutosha. Maana ya vyama vingi sio magomvi, na lengo letu wote ni kufika sehemu moja, CCM wanasema watapita njia hii na CUF wanasema tutapita njia hii, lakini lengo ni kufika sehemu moja.
Washawishi wananchi kwa sera zenu na si kwa kulazimisha kwani huko Uingereza hakuna upinzani, lakini kuna mambo ya kitaifa na wote wanakuwa wamoja.
Watanzania tufike hapo, yapo mambo ya kitaifa yanatakiwa yatuguse. Hivi sasa kuna suala la ugaidi na hili suala kila mtanzania alipige vita kwasababu ugaidi hauna mipaka. Yanayowapata wenzetu tusidhani kwamba Tanzania hayawezi kufika na wala tusiwaendekeze vijana kujiingiza katika makundi yasiyo mazuri.
Tuna kazi ya kuwaelimisha vijana na njia nzuri ni kuweka maslahi ya nchi mbele. Tumekalia bomu kwani Watanzania bila ajira ni bomu linalosubiri kulipuka wakati wowote.
Vijana wanaoijiingiza katika ugaidi ni vijana wa aina hii. Nadhani katika Mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambayo Rais Kikwete ameuanzisha ni kuwapatia gainfully employment (ajira zenye manufaa) vijana na kama hatukulipatia ufumbuzi suala hili tutapata matatizo.
Vijana wa sasa ni tofauti na zamani, vijana ambao hawana kazi wamemaliza vyuoni. Huwezi kumfundisha kijana na kupata shahada ya uzamili halafu anazurura tu mtaani kwani kikitokea kikundi na kumtaka huyo kijana kwa kuahidi kumlipa, inatakiwa mtu makini sana akatae.
Vijana wanatakiwa kuelimishwa, jinsi ya kuweka nguvu zote kuwasaidia vijana ni kuweka maslahi ya nchi mbele na tuwafikirie wananchi zaidi kwasababu uongozi ni utumishi na ukiwa kiongozi ni lazima ukubali kuwatumikia watu.
Swali: Je, wewe unamiliki nyumba ngapi?
Maalim: Mimi wananilaumu watu kwamba maskini, sina nyumba. Mimi sina nyumba na ninayoijenga iko Pemba mwaka wa 20 huu haijaisha. Hata Unguja nyumba niliyokuwa nikikaa kabla ya kuwa Makamu wa Kwanza wa rais ni ya Shirika la Umeme (Zeco).
Siyo kama sitaki kujenga, mimi sijawahi kufanya biashara sasa fedha za kujengea nitazipata wapi, unless you are corrupt (Labda kama wewe fisadi).
Swali: Unalipwa mshahara iweje ushindwe kujenga nyumba?
Maalim: Mshahara napewa, lakini unajua familia yangu watu wangapi mimi. Nakwambia mshahara wa makamu wa kwanza wa rais ni mdogo kuliko wa mbunge au mwakilishi.
Swali: Unapenda Simba au Yanga
Maalim: Mimi wala sifichi mimi ni mpenzi wa Simba SC bwana.