Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MIAKA 20 KATUNI YA KIPANYA: Itaishi milele kutetea wanyonge (2)

Masoud akichora katuni. Picha na Kelvina Matandiko. Picha na Maktaba

Muktasari:

Ufuatao ni mwendelezo wa mahojiano baina ya mchora katuni huyu Ally Masoud na mwandishi wa habari.

Dar es Salaam. Baada ya kuanzishwa kwa gazeti huru la Majira mnamo mwaka 1994,Kipanya alifanikiwa kupata nafasi ya kuanzisha safu ya katuni katika gazeti hilo na kutoa mchora wake wa kwanza.

Ufuatao ni mwendelezo wa mahojiano baina ya mchora katuni huyu Ally Masoud na mwandishi wa habari.

Swali: Ni harakati gani, ulizofanya kabla ya kuondoka Majira kwa kipindi cha miaka 10?

Jibu: Kwa bahati nzuri nashukuru nimepitia magumu katika msingi wa maisha ya sanaa tu, sikuwahi kubadilisha kazi za hapa na pale lakini nakumbuka mwaka 1997, nikiwa na kundi la wachoraji wenzangu tulianzisha jarida letu kwa ajili ya michoro ya Katuni lililojulikana kwa jina la Risasi.

Safari ya jarida hilo ilitokea ndani ya gazeti la Sanifu ambalo lilikuwa na nguvu sana kabla ya kufungiwa na serikali. Risasi nayo ikawa ngumu sana katika soko na usimamizi likavunjika.

Swali: Katika kipindi hiki cha miaka 20 ukiwa kwenye kazi yako ya uchoraji, umewahi kukutana na kesi yoyote?

Jibu: Hapana, sijawahi kufikishwa mahakamani wala kushtakiwa kwa mchoro wowote wa Kipanya lakini malalamiko ni mengi sana hususan kwa wanasiasa. Wanapolalamika inawezekana ujumbe ndiyo ukawa unafika kama nilivyodhani lakini inawezekana ikawa ni mapokeo yao tu tofauti mimi ninavyofikiri.

Ninapochora mchoro wowote huwa ninafikiria zaidi kufikisha ujumbe ili yafanyike mabadiliko sehemu yenye dosari na sijawahi kufikiri kama nitamuudhi au kumuumiza mtu kwa nia mbaya.

Swali: Unadhani katika mazingira hayo, haiwezi kuwa dosari ya kupunguza uhusiano wako kwa wanasiasa?

Jibu : Eeee, hapana tena kwa bahati nzuri mimi ni rafiki mzuri sana kwa wanasiasa, nimekuwa nikiwashambulia zaidi CCM lakini huwezi kuamini ukinikuta nimesimama na viongozi au wanachama wake. Kinachoweza kutokea huwa ni malalamiko tu kama nilivyosema.

Swali: Umechora kwa miaka 20 lakini sijawahi kukuona hata siku moja umepigania Tuzo za MCT, kwa nini?

Jibu: Ni kweli sijafanya hivyo na sababu zinatokana na tafsiri yangu juu ya tuzo. Ninachoamini kama nitakuwa ninastahili kutunukiwa tuzo, haiwezi kuja kwa kupeleka kwenye ushindani. Waandaaji wanapaswa kuwatambua bila kukusanya kazi zao.

Sikiliza mwandishi, nikipeleka au nisipopeleka jamii bado itakuwa na majibu sahihi kama Kipanya ni mchoraji bora au siyo. Nadhani hiyo ni sehemu ya changamoto kwa waandaaji wa tuzo za hapa Tanzania.

Simaanishi kama wamepotoka ila kwa upande wangu ndivyo ninavyoamini, ni utamaduni na falsafa ninayoishi.

Swali: Tofauti na tuzo hizo, kuna mafanikio gani ambayo unaweza kujivunia zaidi kupitia mchoro wa Kipanya?

Jibu : Ni mengi sana, muhimu zaidi ni kukomaa kifikra, kazi hii imenifanya kuwa msomi, kila siku nimekuwa nikiongeza vitu vingi akilini mwangu.

Kipanya imenifanya kuwa na mamilioni ya falsafa za maisha, yaani kwa sasa hivi ninaweza kuishi maisha yoyote ninayochagua.

Pia, Kipanya ndiyo imetengeneza mawazo yote yanayoonekana kwa sasa ikiwamo Maisha Plus na mawazo mengine mengi ambayo bado sijayafungulia.

Mtandao nilionao kwa sasa ni mkubwa sana, nimeanza kuchora wakati wa Rais wa Pili Ali Hassan Mwinyi mpaka leo Rais Kikwete ambaye kwa wakati huo hakuwa hata bungeni, ni furaha kuona uhusiano wenye mtandao huo.

Swali: Kitu gani ambacho huwezi kusahau katika maisha yako?

Jibu: Aisee acha, nakumbuka wakati nikitafuta kazi miaka ya 1988, siku moja nilitembea kwa miguu kutoka Magomeni mpaka Ilala Boma kabla ya kupata ofisi katika jengo la ‘Peugeot house’, Posta.

Kilichonisaidia mimi kuwa tofauti na wenzangu ni ile ‘passion’ kali iliyokuwa ikinisukuma ndani ya nafsi yangu, sikuwa ninatafuta kazi kwa sababu ya kuingiza kipato ila nilifikiria zaidi kutimiza haja ya nafsi yangu.

Namshukuru Mungu kwa sasa nimeona matunda yanayotokana na msukumo ule, ila kumbuka kutokata tamaa kwani kila kitu kinawezekana.

Swali: Nini hasa unachotamani kukiona siku moja katika maisha ya kijana huyu wa Kitanzania?

Jibu: Nimwone akianza kutumia akili yake ya kuzaliwa na siyo kula na kuamka, kutazama jinsi jua linavyozama na linavyoibuka, hiyo sipendi.

Nataka aanze kufikiria kwa kiwango cha juu zaidi kwamba, je ikitokea dunia ikamaliza sumaku yake binadamu tutakwenda wapi au jua likipoteza joto na mwanga wake itakuwaje, kufikiri kwake kumwogopeshe ili wakati wote afikirie kufanya jambo fulani.

Ni dhambi kubwa kukosa umuhimu katika eneo, ofisi au kwa jamii inayokuzunguka, yaani ukikosekana au kuwepo haina madhara.

Changamoto kubwa ni kuhakikisha unapigana ili uwepo wako uwe ni muhimu zaidi ya wenzako ulionao. Mwanadamu ana uwezo mkubwa sana wa kubadilisha jambo.

Fikiria tangu tumepata uhuru mbuzi na simba hawajahi kufikiri kuvaa viatu wala nguo kujisitiri lakini mwanadamu amefanya mangapi kupitia teknolojia tunayoona. Naogopa kusema vijana wengi hawajafungua fikira zao.

Swali: Unaonekana una mambo mengi sana kaka ambayo una tamani kuyatimiza, ikitokea umepata nafasi ya kukutana na Rais Kikwete kwa mazungumzo utatumia muda gani?

Jibu: Itabidi anitafutie chumba cha jirani ili tunapositisha mazungumzo iwe ni kulala tu halafu tukiamka tunaendelea na mazungumzo yetu.