Mambo manne yanayochangia kuimarika kwa thamani ya sarafu, shilingi nchini

Muktasari:
Kati ya masuala muhimu ya kiuchumi yanayopaswa kujadiliwa na kufuatiliwa kwa umakini ni thamani ya sarafu ya nchi ikilinganishwa na zile za mataifa mengine. Hii ni kwa sababu thamani ya sarafu ina maana kubwa katika uchumi wa nchi.
Kila taifa ulimwenguni lina sarafu yake inayotumika kufanikisha miamala tofauti kila siku; baina ya wananchi wake au kimataifa. Tanzania tunayo shilingi tunayoitumia kuuza na kununua bidhaa au huduma. Au kufanikisha mzunguko wowote unaohusu fedha.
Kati ya masuala muhimu ya kiuchumi yanayopaswa kujadiliwa na kufuatiliwa kwa umakini ni thamani ya sarafu ya nchi ikilinganishwa na zile za mataifa mengine. Hii ni kwa sababu thamani ya sarafu ina maana kubwa katika uchumi wa nchi.
Thamani ya sarafu ni muhimu kwa mustakabali wa biashara, deni la taifa, pato la taifa na wananchi, uwekezaji na mambo mengine yahusuyo uchumi wa nchi. Uimara wa shilingi ya Tanzania unapaswa kujadiliwa ili kujua mambo mbalimbali yanayoiyumbisha na kuathiri uchumi.
Thamani ya shilingi
Kama ilivyo kwa sarafu nyingine mfano Kwacha ya Zambia, Rand ya Afrika Kusini, Naira ya Nigeria, Dola ya Marekani na Paundi ya Uingereza, thamani ya Shilingi ya Tanzania inapimwa kwa kulinganishwa na nyingine duniani.
Kiwango cha kubadilisha sarafu moja kwa nyingine ndicho kipimo kikuu cha kuangalia thamani ya fedha ya taifa moja na jingine. Katika muktadha huu, ni jambo la kawaida kuilinganisha Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani. Hii inatokana na ukweli kwamba Dola hiyo ndiyo sarafu imara zaidi inayotumika katika miamala ya kimataifa.
Thamani ya shilingi inakuwa imeshuka pale zinapohitajika nyingi zaidi ili kupata Dola chache na inapotokea kinyume chake basi inakuwa imeimarika.
Katika soko huru, ambapo bei za bidhaa na huduma hutegemea nguvu za ugavi na uhitaji, thamani ya shilingi hutegemea nguvu za soko. Tanzania, tangu katikati mwa miaka ya 1980 ipo katika hali hii ya soko.
Katika soko ambalo serikali huingilia nguvu za soko kwa mkono wake usioonekana, thamani hii haitegemei nguvu za soko bali maamuzi mbalimbali yakiwamo ya kisiasa. Kwa kiasi kikubwa Tanzania ilikuwa katika hali hii mpaka miaka ya 1960 kabla mageuzi ya uchumi ya miaka ya 1980 hayajafanyika.
Mauzo ya nje
Kiuchumi, mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi ni muhimu sana katika uimara wa sarafu. Tanzania inasafirisha bidhaa za madini, pamba, korosho na inategemea kuanza kuuza gesi licha ya kuendelea kuutangaza utalii na huduma zake.
Mauzo ya nje huingiza fedha za kigeni, Dola na nyinginezo. Kunapokuwa na fedha nyingi za kigeni katika uchumi, bei yake au kiwango cha kuibadili hushuka. Bei hii inaposhuka shilingi inakuwa imeimarika. Uimara wa shilingi unategemea kiasi cha bidha na huduma zinazouzwa nje ya nchi na thamani ya mauzo hayo.
Pale thamani ya mauzo ya nje inapokuwa kubwa kuliko ile ya manunuzi toka nje, thamani ya sarafu ya ndani huimarika. Hivyo ni muhimu kuongeza kiasi cha bidhaa na huduma zinazouzwa nje ili kuimarisha shilingi.
Kiuhalisia, mauzo ya nje huleta mapato madogo kuliko fedha zinazolipwa nje katika manunuzi ya bidhaa na huduma kama magari na vipuri vyake, mafuta, matibabu, masomo na ukandarasi.
Manunuzi toka nje
Kama zilivyo nchi nyingi, Tanzania haiwezi kuishi kama kisiwa bila kutegemea bidhaa na huduma toka nje ya mipaka yake. Katika nadharia na uhalisia wa uchumi wa kimataifa, hakuna taifa lililojaliwa rasilimali zote zinazohitajika kuzalisha bidha na huduma zinazohitajika.
Tanzania inahusika katika hili hivyo ili kukidhi tusivyozalisha nchini au ambavyo ni ghali zaidi kuzalisha, tunafanya manunuzi kutoka nje. Manunuzi ya nje hulipwa kwa fedha za kigeni. Kwa Tanzania takribani asilimia 60 ya manunuzi ya nje hulipwa kwa Dola na yanayosalia hulipwa kwa sarafu nyinginezo.
Manunuzi haya hupunguza akiba ya fedha za kigeni. Akiba ya fedha za kigeni ikipungua huathiri soko la fedha na kama ilivyo kwa bidhaa na huduma nyingine, bei yake hupanda. Hilo likitokea, thamani ya shilingi hushuka kwani shilingi nyingi huhitajika ili kupata Dola moja, kwa mfano.
Hivyo ni muhimu kwa nchi kujitahidi kupunguza manunuzi ya bidhaa na huduma kutoka nje ili kuepuka kushuka kwa thamani ya sarafu yake na badala yake kuongeza uzalishaji utakaozidisha kiasi cha bidhaa zinazouzwa nje.
Wananchi waishio ughaibuni
Licha ya bidhaa na huduma zinazouzwa nje, fedha za kigeni zinaweza kupatikana kwa wananchi walio ughaibuni (diaspora) kutuma nchini mwao (remittances). Umuhimu wa wananchi hawa kiuchumi pamoja na mambo mengine ni kutuma fedha za kigeni nyumbani.
Wananchi hawa wanaweza wakawa huko kwa sababu mbalimbali mfano masomo ya juu, ajira na shughuli yoyote inayowaingizia kipato cha ziada wanachoweza kukihifadhi na kukituma.
Fedha zinazotumwa na ndugu hawa waishio nje ya nchi hupitia benki au taasisi yoyote ya fedha na kuingia kwenye mzunguko. Idadi yake huongezeka na kuimarisha sarafu ya ndani ikiwa mambo mengine yamekaa sawa.
Baadhi ya nchi mfano za Afrika Magharibi, Asia (India na Pakistani) mapato yao makubwa ya fedha za kigeni hutokana na watu wao wanaofanya kazi nje ya nchi husika na kutuma fedha nyumbani kwa ndugu, jamaa na marafiki.
Pamoja na umuhimu wa watu hawa katika mchango wa fedha za kigeni, kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania siyo afya kiuchumi kwa nguvu kazi kubwa namna hii kuwa nje ya nchi japokuwa uwepo wao huko unapaswa kueleweka.
Misaada na Uwekezaji
Misaada na uwekezaji ni chanzo kingine cha fedha za kigeni. Taifa linapopokea msaada au kukaribisha wawekezaji, utekelezaji wake hufanywa kwa fedha za kigeni. Misaada ikiwa mingi maana yake fedha hizo zimeongezeka kwenye mzunguko. Vivyo hivyo kwa uwekezaji.
Tanzania inapokea misaada toka nchi mbalimbali duniani. Misaada hii huwa katika fedha za kigeni kama vile Dola. Japokuwa siyo jambo jema kwa taifa kutegemea misaada, ukweli unabakia kuwa inapokuja kwa fedha za kigeni, inachangia kuimarisha shilingi yetu.
Hali hii pia hujitokeza kwenye uwekezaji hasa kutoka nje. Yeyote anayekuja nchini huleta fedha za kigeni. Jambo la msingi hapa ni kuwa misaada na uwekezaji huu vinaongeza fedha za kigeni hasa Dola sokoni hivyo kushusha bei yake na hivyo kuimarisha Shilingi.